Thursday, December 17, 2015

Prof. Muhongo Aagiza kufungwa matoleo ya umwagiliaji

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akizungumza jambo wakati wa ziara yake kwenye kituo cha kuzalisha umeme cha Kidatu. Katikati ni Meneja wa Kituo hicho cha Kidatu, Mhandisi Justus Mtolera na anayemfuatia ni Meneja wa Kituo cha kuzalisha umeme cha Mtera, Mhandisi Abdallah Ikwasa.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akimsikiliza Meneja wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Kidatu cha Mkoani Morogoro, Mhandisi Justus Mtolera wakati wa ziara yake kituoni hapo lengo likiwa ni kujionea uzalishaji umeme wa kituo hicho.
Bwawa la maji la kuendeshea mitambo ya kuzalisha umeme la Kidatu likionekana katika hali ya kupungukiwa na maji.

Serikali imeagiza matoleo ya maji ya kumwagilia mashamba  yanayotumia maji ya mito inayotiririsha kwenye mabwawa ya kuzalisha umeme ya Mtera na Kidatu yafungwe.

Agizo hilo limetolewa leo na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipotembelea Bwawa la Kidatu na kujionea namna ambavyo kina cha maji kwenye bwawa hilo kilivyopungua.

Waziri Muhongo alisema tatizo kubwa la uzalishaji mdogo wa umeme wa maji nchini ni umwagiliaji usio zingatia taratibu za matumizi sahihi ya maji.

Alisema mfumo wa umwagiliaji unaotumika ni wa kienyeji sio wa kitaalamu. "Nimeshuhudia mtu anazuia maji kutiririka kwa kutumia mawe, magogo ama viroba vya mchanga; hii sio sahihi," alisema.

Akizungumzia umeme unaozalishwa kwa nguvu ya maji, Waziri Muhongo alisema kwa hivi sasa ni asilimia ishirini tu inayozalishwa kutoka kwenye vyanzo vya maji nchini.

Alisema jumla ya uwezo wa mitambo yote ya maji (installed capacity) ni Megawati  561.84 ambapo wastani wa uzalishaji kwa sasa kutoka kwenye mitambo hiyo ni Megawati 110 hiyo ni kuanzia tarehe 13 hadi tarehe 16 mwezi huu.

"Nimetembelea Nyumba ya Mungu, Hale, Pangani, Mtera, Kihansi na Kidatu na kugundua kwamba tatizo  sugu ni umwagiliaji na siyo tabianchi," alisema.

Alisema mashamba ya umwagiliaji yanaongezeka Mikoani Mbeya, Iringa na Morogoro.

Aliongeza kuwa vibali vya umwagiliaji vimetolewa kienyeji bila kutafakari athari itakayotokea.

Profesa Muhongo alisema kipindi hiki ni cha mvua hivyo wenye mashamba ya umwagiliaji watumie maji ya mvua badala ya kuendelea kutumia mito.

Alisema wakati mazungumzo yanaendelea, Bodi ya Maji- Bonde la Rufiji wahakikishe wanakagua mifereji yote ya umwagiliaji inayoingiza maji kwenye Mto wa Ruaha mkuu na kuifunga ili kuruhusu bwawa la Mtera kupata maji.

Alieleza kwamba kwa kufunga mifereji hiyo ndani ya siku nne hadi tano maji yatakua yameingia kwenye bwawa la Mtera na hivyo kuweza kuendesha mitambo.

Awali akimueleza Waziri hali halisi ya uzalishaji umeme kwenye kituo hicho cha Kidatu, Meneja wa Kituo, Mhandisi Justus Mtolera alisema umeme unaozalishwa kituoni hapo kwa sasa ni megawati 50 wakati kituo hicho kinao uwezo wa kuzalisha jumla ya megawati 204.

Mhandisi Justus alisema kituo hicho kinayo mitambo minne ya kuzalisha umeme lakini kutokana na tatizo la maji, mitambo miwili tu inafanya kazi ambapo kila mmoja unazalisha kiasi cha Megawati 25.

1 comment:

river care initiative said...

Kweli sehemu kubwa ya upungufu wa maji siyo tabianchi. Na pia sehemu kubwa sio umwagiliaji pekee. Tatizo au changamoto ni matumizi ya maji yasioendelevu kwa watumiaji maji wa aina zote. Kutumia ukifirikilia hakuna mwingine chini yako au kutumia kufuatana na uwezo wa miundombinu yako bila kujali kiasi cha maji kilichopo au kinachotegemewa kuwapo ni hatari.Elimu inahitajika kwa wadau wote, lakini pia mfumo unganishi unaotambua hali ya maji na mahitaji ya kila mdau kwa vigezo vya ustawi wa jamii husika, uchumi wa nchi na mazingira tunayoyategemea ni muhimu kuwapo na kukubalika na wote na kufuatwa na kila mdau.