Tuesday, December 8, 2015

MAKALA: Zao la Karafuu laweza kuwa uti wa mgongo wa Uchumi Zanzibar

Na Pili Khatib na Zuhura Omar, MUM 

 Kuimarisha Zao la Karafuu ni sawa na kuimarisha Uchumi na Maendeleo ya nchi, jitihada za Wadau ni muihimu ili kufika lengo la Serikali la kuifanya Sekta ya Zao la Karafuu kuwa uti wa mgongo wa Uchumi liweze kufikiwa.

Kutokana na umuhimu wa Sekta ya Karafuu kwa Maendeleo ya Uchumi Serikali imefanya mageuzi makubwa katika sekta hiyo kwa lengo la kuongeza uzalishaji na tija kwa Wakulima na Taifa kwa jumla.

Katika utekelezaji wa Mageuzi hayo yaliyoanza mwaka 2011 Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar ZSTC ambalo ni mdau mkubwa katika uimarishaji wa Sekta ya Karafuu ilianzisha Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu (Zanzibar Clove Fund) ambapo ulizinduliwa rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein tarehe 28/08/2011.
Baadhi ya wafanyakazi wa ZSTC wakipita mbele ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohmaed Shein wakiwa wamebeba bango lenye ujumbe wa kuimarisha zao la karafuu.

Mfuko huo wa Maendeleo ya Karafuu umeanzishwa kwa mujibu wa Sheria mpya ya Maendeleo ya Karafuu Nam. 2 ya Mwaka 2014, chini ya kifungu Nam. 4 (1) ambacho kinaipa mamlaka Bodi ya Shirika la ZSTC kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu.  Mfuko huo upo chini ya Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la ZSTC.

Lengo kuu la kuanzishwa kwake ni Kuimarisha, Kuendeleza na Kusimamia Sekta ya Zao la Karafuu Zanzibar kwa kutoa msaada unaohitajika kwa Wakulima wa karafuu kwa lengo la kuongeza uzalishaji.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la ZSTC Mwanahija Almas Ali Sekta hiyo ya Karafuu inaendelea kuimarika zaidi hasa baada ya kuanzishwa kwa Mfuko huo wa Maendeleo ya Karafuu.

Ama kweli ‘Jembe halimtupi Mkulima’ ni zamu ya Wakulima wa zao la karafuu kunufaika zaidi na ukulima wa zao hilo kutokana na kuwepo kwa Mfuko huo wa Maendeleo ya Karafuu unaotoa huduma kwao katika kuimarisha zao la karafuu.

Bi. Mwanahija amesema utafiti ulifanyika juu ya namna ya kufanya mageuzi yenye tija katika Sekta ya Karafuu ndipo ikaoneka umuhimu wa kuanzisha Mfuko huo ambapo muda mfupi baada ya kuanzishwa unaonekana kuleta faida katika uimarishaji wa zao hilo. Mfuko huo umeongeza nguvu katika jitihada za Serikali za kuimarisha zao hilo la uchumi wa Taifa.

 “Madhumuni ya kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu ni kuhakikisha Sekta ya Karafuu inakua na kuimarika zaidi. Kuongeza idadi ya mikarafuu na uzalishaji ambapo hivi sasa Wananchi wamehamasika zaidi katika upandaji mikarafuu kwa wingi”. Amefahamisha  Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSTC Bi. Mwanahija.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo Mwendeshaji wa Shirika la ZSTC, Mfuko huo utafanya sensa ya mikarafuu sambamba na kuwasajili Wakulima na Wafanyabiashara wa zao hilo ili kurahisisha upatikanaji wa huduma.

Amefahamisha kuwa kupitia Mfuko huo na kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na Maliasili kutafanyika tafiti kwenye kila eneo linayohusu zao la karafuu kwa lengo la kugundua changamoto na kuzifanyia kazi.

Amesema Shirika la ZSTC kwa kushirikiana na Wadau wengine inakamilisha mpango maalumu wa kuziongezea hadhi na thamani karafuu za Zanzibar kupitia mradi wa ‘Branding’ ili kuongezeka kwa uzalishaji kwenda sambamba na kuongezeka kwa tija kwa Wakulima na Taifa.

Amesema hivi sasa mpango huo upo katika kutafuta vinasaba vinavyoonyesha ubora wa karafuu za Zanzibar kupitia Mkemia Mkuu wa Serikali Zanzibar.

Wakati akizindua Mfuko huo Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohmed Shein  alihimiza suala la utafiti katika kila sehemu inayohusu kilimo na biashara ya Zao la Karafuu na kusisitiza suala la kuongeza thamani ya za karafuu sambamba na kuzingatia viwango ili kulinda ubora wa Zao hilo.

Aidha, Mkurugenzi amefahamisha kuwa Mfuko huo umekuwa ni msaada mkubwa katika uimarishaji wa zao la karafuu hasa kwa Wakulima ambapo unatoa fidia kwa Wakulima wanaopata ajali wakati wa uchumaji kupitia Shirika la Bima Zanzibar.

Mfuko huo ni neema kwa Wakulima wa karafuu kwa namna unavyowanufaisha na kubadilisha maisha yao ya kila siku katika zao la karafuu. Mfuko huo inaonekana umedhamiria kuwapatia Wakulima vifaa na huduma zinazohitajika katika uzalishaji.

 Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSTC, vikundi vya uatikaji miche ya mikarafuu vya binafsi na Serikali huwezeshwa kwa kupatiwa vifaa vya uatikaji miche kama vile vifuko (Polythen bage), mabero, mipira ya maji na matenki.
Hurahisishiwa upatikanaji wa vifaa vya uanikaji na uchukuaji wa karafuu kama vile majamvi na magunia na kupatiwa ruzuku kulingana na  utaratibu maalum uliowekwa.

Amesema Mfuko huo umelipa bima ya milioni 60 kwa Shirika la Bima ili kuwafidia Wakulima 100 wanaokisiwa kupata ajali katika zoezi la uchumaji wa karafuu mwaka 2015/2016 ambapo hadi sasa tayari watu tisa wameripotiwa kupata ajali wote kutoka Pemba.

Amesema Wakulima wanaendelea kupata mikopo ya uchumaji kupitia Mfuko huo na alifahamisha kuwa katika bajeti ya 2015/2016 Mfuko umepanga kutumia milio 140 kwa ujenzi wa barabara ya Ng’omeni ikiwa ni msaada wa kusadia miundombinu ya sehemu za uzalishaji wa karafuu.

Amesema kupitia Mfuko huo Shirika limeongeza jitihada za kutoa elimu kwa Wakulima juu ya uchumaji na uanikaji unaotakiwa ili kulinda ubora wa zao hilo katika soko la nje.
Mfuko huo ni moja ya nyenzo muhimu za kuimairisha na kuendelza zao la karafuu ambapo Wananchi hasa Wakulima wa zao hilo wana kila sababu ya kujivunia mafanikio yaliyopatikana katika kulirejeshea hadhi hilo la biashara.

Pamoja na juhudi hizo bado Sekta ya Karafuu inakabiliwa na changamoto nyingi zinazohitaji kufanyiwa kazi. Moja ya changamoto hizo ni kwa baadhi ya Wakulima kuchafua karafuu kwa makusudi, kuendelea kuanika karafuu barabarani, juu ya bati na sakafuni licha ya kupewa elimu juu ya madhara ya kuanika katika sehemu hizo.

Makosa hayo ni hatari kwa vile yanaweza kusababisha Wanunuzi katika soko kuzikataa na hivyo  kupelekea hasara kwa Wakulima, Wananchi na Taifa kwa jumla.

Ni jukumu la jamii kusaidia  katika kutoa elimu juu ya umuhimu wa kulinda ubora wa karafuu zetu za Zanzibar ili kufanikisha azma ya Serikali ya kuifanya Sekta ya Karafuu kuwa ni Sekta ya kukuza uchumi wa Nchi na yenye kujenga ustawi wa wananchi wake.

“Kithamini kikutunze” ni msemo maarufu wanaoutumia wahenga wa Kiswahili juu ya utunzaji na kuthamini mambo muhimu yanayoleta tija kwa jamii. Kuna kila haja kwa Wakulima wa karafuu kuzithamini na kuzitunza karafuu kwa manufaa yao na Taifa kwa jumala.
.
Changamoto nyengine ni katika uzalishaji ambapo mahitaji ya miche ni makubwa zaidi kuliko uwezo wa kuotesha, huduma dhaifu kwa mikarafuu michanga na baadhi ya Wakulima kutaka miche mingi kuliko uwezo wa kuipanda na kuihudumia.

Mabadiliko ya tabia nchi nayo yamekuwa ni changamoto kubwa ambapo yanayosababisha miti mingi kukauka ikiwemo mikarafuu na ongezeko la mahitaji ya ardhi, majengo na kuni na upandaji usiozingatia taaluma.

Mfuko wa maendeleo ya Karafuu ni chachu ya kuongeza uzalishaji wa zao la karafuu Zanzibar ili kurudi katika kiwango cha zamani ambapo historia inaonyesha kuwa Zanzibar ilikuwa nafasi ya kwanza duniani katika uzalishaji wa karafuu nyingi ila kwa sasa ipo nafasi ya tatu.

“Karafuu ni Uhai’ Karafuu kwa Maendeleo ya Zanzibar”

No comments: