Friday, December 25, 2015

MAENDELEO NI KWA VITENDO SIO MANENO: PROFESA MUHONGO

Mbunge wa jimbo la Musoma Vijijini ambaye pia ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ameanza kwa kishindo kutekeleza ahadi zake kwa wananchi wa jimbo hilo na huku akiahidi maendeleo kwa kasi zaidi.

Profesa Muhongo alidhihirisha hayo juzi katika kijiji cha Murangi, Mkoani Mara katika kikao chake na baadhi ya wananchi wa jimbo hilo, watendaji wa Halmashauri ya Musoma Vijijini na madiwani huku lengo la kikao likiwa ni kujadili mipango na miradi ya uchumi na maendeleo ya jimbo hilo.

Katika kikao hicho, iliazimiwa kuanzishwe Mfuko wa Elimu wa Jimbo ambapo Profesa Muhongo aliahidi kutoa kiasi cha Shilingi Milioni mia moja ambazo atakopeshwa na Bunge kwa ajili ya kununulia gari.

Alisema badala ya kununulia gari, fedha hiyo ataiingiza kwenye Mfuko huo ili kuleta maendeleo kwenye jimbo hilo. “Dhamira yangu ni kuhakikisha jimbo letu linasongo mbele kiuchumi na kimaendeleo na siyo maneno bila mipango madhubuti,” alisema.
Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akizungumza jambo wakati wa kikao chake na wananchi wa jimbo hilo pamoja na wadau wa maendeleo.

Katika maelezo yake ya mikakati ya maendeleo kwa jimbo hilo, Profesa Muhongo alisema kufikia Mwezi Januari mwanzoni, ataanzisha Ofisi tano za Mbunge jimboni humo ili kufikisha huduma kwa wananchi kiurahisi.

Alisema Ofisi hizo zitakuwa na mtumishi mmoja ambaye ataajiriwa na Mbunge na atapatiwa vitendea kazi vya kuanzia ambavyo ni pikipiki ili kumuwezesha kuwafikia wananchi kirahisi na kompyuta mpakato (laptop) kwa ajili ya kutunza taarifa na mawasiliano.

Profesa Muhongo alitaja maeneo ambayo ofisi hizo zitaanzishwa kuwa ni kijiji cha Murangi ambapo ndio patakua makao makuu, Busekela, Sangana, Mugango na  Nyegine na alitoa wito kwa vijana wa maeneo hayo kuomba kazi kwa nafasi husika na kwamba watakaofaulu watatakiwa kuwepo maeneo hayo ili kila watakapohitajika waweze kupatikana kiurahisi.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria Kikao cha Profesa Muhongo (hayupo pichani).

Alisema usaili wa kuwapata watumishi hao utafanyika tarehe 26 na 27 mwezi huu na watakaofaulu wataanza kazi tarehe 1 Januari, 2016 kwa uangalizi wa kipindi cha miezi mitatu (probation period) na alitaja vigezo vitakavyotumika kwenye kuwapata kuwa  ni elimu kuanzia kidato cha nne na ujuzi wa kompyuta.

Mbali na hilo, katika kuimarisha elimu jimboni humo, Profesa Muhongo ametoa vitabu vya kujifunzia vipatavyo 20,000 (elfu ishirini) katika shule mbalimbali na huku kipaumbele kwa wakati huu ni kwa shule zilizofanya vibaya kwenye matokeo ya mwaka huu.

Alisema tayari ameagiza vitabu vingine 22,000 kutoka nchini Marekani na vitakapoingia nchini ameagiza Madiwani kuvisambaza kwenye shule ambazo hazina vitabu vya kutosha.

Mbunge huyo alisema kwa kutumia Mfuko huo wa Elimu wa Jimbo, pamoja na fedha za Halmashauri, kila shule itapatiwa huduma ya umeme, maji pamoja na kujenga na kukarabati shule hizo pamoja na nyumba za walimu.

Akizungumzia suala la miundombinu ya barabara, Mbunge huyo aliahidi kusimamia ujenzi wake ambapo alisema barabara kutoka Musoma mjini hadi makao makuu ya jimbo itajengwa kwa kiwango cha lami na alisema tayari tathmini imeanza na itakamilika mwishoni mwa mwezi huu.

Mbali na hilo, kwa barabara zilizo chini ya Halmashauri, Profesa Muhongo aliagiza madiwani wakae na kupitisha bajeti kwa ajili ya kukarabati barabara hizo na aliagiza kikao hicho kifanyike kabla mwezi huu haujamalizika.

Kuhusu suala la Afya, Profesa Muhongo alisema tayari ameagiza gari la wagonjwa ambalo linatarajiwa kuingia nchini ndani ya wiki mbili zijazo.

Kikao hicho cha maendeleo ya jimbo la Musoma vijijini kilihudhuriwa na wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi miongoni mwao kukiwa na wazawa wa jimboni humo ambao kwa sasa wanaishi nje ya jimbo hilo na wageni kutoka Ujerumani.

No comments: