Saturday, December 12, 2015

MAANA HALISI YA KIFASIHI NA FALSAFA YA MSEMO WA "KUTUMBUA MAJIPU"

 
Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli (pichani) Malitoa msimamo kwa Serikali yake anayotaka kuiongoza ikiambatana na kauli mbiu ya “Hapa Kazi tu”. 
Katika utekelezaji wa kauli mbiu hiyo alitumia falsafa ya msemo wa “kutumbua majipu” ikiwa ni silaha ya kuongoza utendaji wa kazi kwa Serikali ya Awamu ya tano. 
Maneno hayo ya hekima na ya kijasiri yalitolewa katika hotuba ya ufunguzi wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Novemba 20, 2015 Mjini Dodoma. Aidha, maneno hayo ni ya kijemedari katika medani ya kivita ya mapambano dhidi ya ufisadi uliokubuhu kwa baadhi ya watendaji wa Serikali ili kuwakomboa wananchi katika dimbwi la umaskini.
Nukuu ya falsafa ya msemo wa kutumbua jipu: “Mheshimiwa Spika; mimi nimewaahidi wananchi na nataka niirejeree ahadi yangu kwao mbele ya Bunge lako tukufu kwamba, nitapambana na rushwa na ufisadi bila kigugumizi na bila haya yoyote. Dawa ya jipu ni kulitumbua, na mimi nimejipa kazi ya kuwa mtumbua jipu. Najua kutumbua jipu kuna maumivu lakini bahati mbaya halina dawa nyingine”
Maana ya Jipu, kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu toleo la tatu (TUKI, 2014) ni uvimbe mkubwa unaotunga usaha.
 “Kutumbua majipu”ni kitendo cha kuondoa usaha uliopo katika uvimbe. Falsafa ni elimu ya asili, maana na sababu za mambo au vitu. Pia falsafa ni busara, hekima, au mtazamo. Lugha iliyotumika hapa ni jazanda/taswira yaani lugha ya picha ya mahali au kitu fulani inayojichora mawazoni mwa msomaji au msikilizaji kutokana na maelezo anayoyapata”. 
Visawe vingine vinavyohusiana na neno “kutumbua majipu” ni; Kukamua, kuminya na kutumbua.
Kukamua maana yake ni kuminya kitu ili kutoa kilichomo ndani yake; filisi mtu 
Kuminya maana yake ni kubana kwa nguvu kitu kilicho laini kama vili jipu.
Kutumbua maana yake ni toboa kitu kilichovimba kama vile jipu kwa kutumia kifaa chenye ncha kali au kwa kuminya.
Aina za majipu
Kuna aina tatu za majipu ambazo ni: Vijipu Uchungu, Jipu na jipu Tambazi.
“Vijipu uchungu” ni majipu yanayoota kwa wingi lakini ni madogomadogo na huuma sana yakiminywa. Kwa kawaida majipu haya huwapata watoto wadogo hasa maeneo ya joto huku yakiambatana na homa kali.
“Jipu” ni jipu kubwa ambalo huwa na usaha mwingi sana, hutumbuliwa kwa kutumia kifaa chenye ncha kali kama vile sindano na utambi na huakikisha mpaka kiini kimetoka (moyo wa jipu).
“Jipu Tambazi” ni jipu kubwa linalotambaa sehemu kubwa ya mwili. Jipu tambazi mara nyingi huchomwa kwa mionzi mikali au huwekwa dawa ili kulizuia lisienee mwilini (hunywea).

Tabia ya baadhi ya Majipu
Baadhi ya majipu yana tabia ya kuota kama uyoga mwilini ikiwa na maana likitumbuliwa sehemu moja baadaye huota sehemu nyingine. Majipu mengine huwa yana midomo miwili hadi mitatu lakini yote hutumbuliwa, hukamuliwa au kuminywa.

Tafsiri ya  kimuktadha wa kifasihi kuhusu dhana ya kutumbua majipu
Maana ya msingi na ya kimuktadha na kifalsafa kuhusu “dhana ya kutumbua majipu” ni kuwaondoa baadhi ya watumishi wa umma wanaokiuka sheria, kanuni na taratibu za maadili ya utumishi wa umma kwa kujiingiza katika mtego wa rushwa na kusamehe kodi, kuhujumu uchumi kwa kurubuniwa na baadhi ya watu wenye uwezo wa kifedha.

Kutumbua majipu ni sawa na kazi ya kujitoa muhanga kwa Kupambana, kufichua na kubainisha hadharani wahujumu uchumi, wezi wa mali ya umma pamoja na kuondoa/kutatua matatizo makubwa yanayolikabili taifa kwa sasa. “Jipu” linawakilisha matatizo, kero, adha, udhalimu na uovu unaokandamiza na kunyonya maisha ya wananchi wa kawaida.
 Matatizo/ majipu hayo ni pamoja na:

Vitendo vya rushwa na mianya yake, Wizi, ufisadi uliokubuhu, ubadhirifu wa mali za umma, urasimu, huduma duni kwa wananchi, ukwepaji wa kodi hasa kwa wafanya biashara wakubwa,  migogoro ya mipaka ndani ya maeneo ya makazi na hifadhi, ukosefu wa madawa, huduma mbovu kwenye vipimo, kutoa hovyo vibali vya uraia na hati za kusafiria,  kushindwa kusimamia ajira za wageni, uhaba wa vifaa vya kujifunzia, michango isiyo ya lazima, kubambikiana kesi, wenyeji kutofaidi uchimbaji wa madini, uhaba wa pembejeo za kilimo, tatizo la masoko, uwiano wa watendaji kazi na huduma inayotolewa, upotevu wa rasilimali za taifa, matumizi mabaya ya fedha, uporaji wa rasilimali zetu za asili, uingizaji na usambazaji wa madawa ya kulevya, n.k.

Halikadhalika, kuutumbua majipu ni kupambana na kuondoa au kufichua uozo uliokubuhu na mizizi yake, ili kuokoa rasilimali za taifa kwa lengo la kuwafanya wananchi wawe na imani na Serikali yao. Hapa kwa maneno mengine ni “vita kama zilivyo aina nyingine za vita kwani kupambana na ufisadi na mafisadi ni sawasawa na vita vikubwa na vizito vya kujitoa muhanga, hivyo inahitaji ujasiri na ukakamavu wa hali ya juu sana. Aidha, ni vita vya kupambana na wahujumu uchumi ili kunusuru upotevu wa mali za umma. Vita hivi vinahitaji nguvu ya umma kuokoa mali za umma na kumpa ushirikiano mwasisi wa vita hivi vinavyopiganwa kizalendo na vyenye maslahi mapana kwa taifa letu.

 Mwana fasihi Nguli, Shaaban Robert alisema, “mvunja nchi ni mwananchi”, ni vema wananchi tukatoa ushirikiano wa dhati ili kufikia ushindi wa vita hii ya ukombozi dhidi ya mali za umma.

“Jipu” linapotumbuliwa linahitaji ujasiri kwa sababu linamaumivu makubwa kwa anayekamuliwa. Kwa mantiki hiyo majipu yanayotakiwa kukamuliwa ni zile kero zinazolalamikiwa na wananchi dhidi ya Serikali yao. Kiini kikubwa cha majipu hayo ni watumishi wa Umma kutofuata sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma pamoja na dhana nzima ya uwajibikaji kwa umma, ikizingatiwa kuwa ukiukwaji na uvunjwaji wa sheria wa makusudi unaowarubuni baadhi ya watumishi wa umma na kujiingiza katika vitendo viovu vya kupokea na kutoa rushwa.  Pia kusababisha kero na malalamiko kwa wananchi yasiyokuwa ya lazima. Vitendo hivyo viovu vinasababisha wananchi kukata tamaa na kukosa imani dhidi ya Serikali yao.
Lugha iliyotumika ya “kutumbua jibu”

Lugha iliyotumika katika falsafa ya kutumbua majipu ni msemo wa “tamathali ya upeo”, yenye mtindo wa usemaji wa maneno ya uneni wa fasaha, hufanya mkwezo wa mawazo. Msemaji akianza na jambo moja au jambo dogo na polepole, kama vile mpanda ngazi, hufikia kilele cha jambo kubwa. Twaweza kuulinganisha mtindo huu wa usemi na mtu ambaye ana masikitiko. 
Huzuni huingia moyoni, polepole machozi hutoka, na kisha mtu mwenye huzuni hupasua kilio ili kufichua uchungu ulio ndani ya moyo wake. Ndipo Mheshimiwa Rais alipopasua uchungu ulio moyoni mwake kwa kutumia msemo wa “kulitumbua jipu”. Ametumia mtindo huu wa “mkwezo wa mawazo kwenda juu, au mpomoko wa juu”. Kwa maana hiyo falsafa hii imetambaa ndani na nje ya nchi na kupata mashiko kwa wananchi katika utekelezaji wa kauli mbiu ya “Hapa kazi tu”, inayowataka watumishi wa umma wafanye kazi kwa uadilifu na kufuata sheria pamoja na kanuni na taratibu za utumishi wa umma ili kuboresha maisha ya wananchi na kuleta ustawi kwa jamii.  

Makala hii imetolewa na:
Idara ya Maendeleo ya Utamaduni 
Sehemu ya Lugha:
Bibi. Shani Kitogo-Mkurugenzi Msaidizi 
Imeruwazwa na 
Sefania A. Motela –Afisa Utamaduni: Lugha
Christopher Mhongole-Afisa Utamaduni: Lugha

No comments: