Friday, December 4, 2015

KANUNI MPYA ZA HUDUMA ZA ZIADA ZA MWAKA 2015 ZA SHERIA YA MAWASILIANO YA KIELEKTRONIKI NA POSTA YA MWAKA 2010

Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Sayansi na TekinolojiaPriska Olomi (kushoto) , akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) Dar es Salaam leo, kuhusu kutungwa kwa kanuni za huduma za ziada kwa makampuni ya simu nchini zitakazo walinda watumiaji wa huduma hizo,kulia ni Mkuu wa kitengo cha Sheria wa Wizara hiyo,Veronika Sudayi. 
(Picha na Hassan Silayo).

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAWASILIANO, SAYANSI NA TEKNOLOJIA

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KANUNI MPYA ZA HUDUMA ZA ZIADA ZA MWAKA 2015 ZA SHERIA YA MAWASILIANO YA KIELEKTRONIKI NA POSTA YA MWAKA 2010 

(THE ELECTRONIC AND POSTAL COMMUNICATION ACT 2010 (VALUE ADDED SERVICES) REGULATIONS 2015) 

Ndugu Waandishi wa Habari 
1. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutupatia uhai na afya njema na kutuwezesha kukutana leo kupeana taarifa kuhusu Kanuni Mpya za Huduma za Ziada za Mwaka 2015 ambazo zinatokana na Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya Mwaka 2010. Napenda pia kuchukua nafasi hii kuwashukuru kwa kukubali mwito kushiriki nasi katika siku hii ya leo. Karibuni sana. 

Ndugu waandishi wa Habari.
2. Sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) imeendelea kukua kwa kasi duniani na hapa nchini kwetu na imeleta mafanikio mengi katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, kisiasa na kijamii kwenye ngazi ya kitaifa na kwa mwananchi mmoja mmoja katika maisha ya kila siku kwa waishio mijini na vijijini. Idadi ya watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini imeendelea kuongezeka kutoka line za simu za viganjani milioni 2.96 mwaka 2005 hadi kufikia milioni 32.1 mwezi Desemba 2014. Watumiaji wa mfumo wa intaneti nao wameongezeka kutoka milioni 3.56 mwaka 2008 hadi kufikia milioni 11.34 mwaka 2014.

 Mafanikio haya yanathibitika nanyi mmekuwa ni mashahidi kwa kuongezeka kwa huduma za mawasiliano na huduma za ziada za matumizi ya mitandao ambapo imerahisisha kutoa na kupata huduma kwa haraka na kwa wakati; na wananchi hawalazimiki kusafiri; na kupunguza urasimu kama vile huduma za kutuma na kupokea pesa; kulipia ankara za maji, umeme, ada; ukusanyaji wa mapato; kulipia leseni; kusafirisha taarifa na data; huduma mtandao kama vile Serikali mtandao, biashara mtandao, shule mtandao na tiba mtandao.

 Kwa mfano kuna ongezeko kubwa la huduma za ziada kupitia mawasiliano ya simu za kiganjani. Huduma hizo ni pamoja na miamala ya kifedha ambayo ina watumiaji wapatao 12,330,962 na ununuzi wa huduma na bidhaa kwa kutumia miamala ya kibenki. Hivi sasa, wananchi wanaweza kufanya malipo ya huduma mbalimbali wanazozitumia kupitia simu za kiganjani ambapo katika kipindi cha Julai, mwaka 2013 hadi Aprili, mwaka 2014 jumla ya miamala 972,641,605 yenye thamani inayofikia shilingi Trilioni 28.3 imefanyika. Maendeleo haya yamesaidia kuokoa muda na kupunguza msongamano sehemu za kulipia na kupata huduma hizi. 

3. Aidha, mafanikio hayo yameleta changamoto mbalimbali kwenye Sekta na katika jamii yetu. Kwa leo tunazungumzia uwepo wa changamoto ya utoaji wa huduma za ziada kwa watumiaji wa huduma za ziada bila kuwa na utaratibu unaoeleweka kati ya mtoa huduma na mpokea huduma au mlaji. Baada ya kujitokeza kwa changamoto katika utoaji wa huduma za ziada, Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano Sayansi na Teknolojia ilitunga Kanuni Mpya za Huduma za Ziada za Mwaka 2015 (Value Added Services - VAS Regulation 2015).

 Kanuni hizo zimetangazwa kwenye Gazeti la Serikali la tarehe 7 Mwezi Agosti mwaka huu 2015 na kupewa GN. Namba. 320. Kanuni hizo zimetokana na Sheria ya Mawasiliano ya kielektroniki na Posta ya Mwaka 2010 (The Electronic and Postal Communication Act 2010) iliyotungwa na kuridhiwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo tarehe 29 Januari 2010 na badae kusainiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo tarehe 20 Machi 2010. 

Ndugu Wananchi 
4. Lengo kuu la Kanuni za VAS ni kuweka utaratibu mahususi unaoleweka wa utoaji na upokeaji wa huduma za ziada. Huduma za ziada ni huduma za mawasiliano za kielektroniki zinazotolewa kupitia mitandao zaidi ya huduma za msingi za mawasiliano. Kanuni za VAS zimeweka utaratibu kwa mlaji kujiunga na kujiondoa kupata huduma za ziada; wajibu wa mtoa huduma na mlaji wa huduma za ziada; pamoja na adhabu pindi matakwa ya kanuni yatakapokiukwa. Kimsingi kanuni hizi humlinda mlaji wa huduma za mawasiliano asipewe huduma ambazo hajaridhia kupitia huduma za ziada zinazotolewa na watoa huduma za mawasiliano. 

Ndugu Waandishi wa Habari 
5. Kanuni za VAS zinamtaka mtoa huduma za ziada kutoa taarifa kamili na sahihi kuhusu huduma za ziada katika lugha rahisi na ya uwazi. Lugha zinazotakiwa kutumika kwa mujibu wa Kanuni zetu Mpya ni Kiswahili na Kiingereza tu. Mtoa huduma za ziada atakuwa na wajibu ufuatao katika kutoa huduma kwa mlaji; 

i. Kutoa masharti na vigezo vya huduma zote ikiwemo gharama, kwa njia ya kielektroniki na kudurufu (printed and electronic formats); 

ii. Ikiwa mhusika mwingine atahusishwa katika utoaji wa huduma hiyo (third party), mlaji anapaswa kujulishwa kuhusu hitaji ama utegemezi wa huduma hizo kutoka kwa mhusika mwingine; 

iii. Kuzingatia matakwa ya Kanuni za Viwango vya Huduma (Quality of Service - QoS) za Sheria ya EPOCA; 
iv. Ikiwa kutakuwepo na mabadiliko katika huduma, mlaji apatiwe taarifa kamili kuhusu masharti ya uhamaji, ikiwa ni pamoja na mabadiliko katika utoaji wa huduma hizo na gharama endapo zitajitokeza; 

v. Kumjulisha mlaji juu ya waranti za bidhaa zilizotolewa kwa ajili ya kutumika pamoja na huduma ikiwa ni pamoja na jinsi ya kupata waranti hizo. 

Ndugu waandishi wa habari 
6. Kanuni zinamtaka mtoa huduma za ziada, kuweka mfumo wa kuwezesha huduma za ziada kwa mlaji kujiunga (opt in / activation) au kujiondoa (opt out/de-activation) ambao ni rahisi na wa uwazi kwa kutumia teknolojia inayofaa ikiwemo ujumbe wa meseji (SMS), Huduma ya sauti (Interactive Voice Request – IVR), namba maalum (Unstructured Supplementary Service Data – USSD) ama mchanganyiko wa teknolojia hizi.Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania itawajibika katika kutoa namba (short code) kwa watoa huduma za ziada ili kuwezesha huduma hizo kupitia teknolojia zilizotajwa. 

7. Mlaji anaweza kujiunga (opt in/activation) ili kupatiwa huduma za ziada kwa njia tajwa hapo juu. Ili kujiunga kwa njia ya SMS, mtoa huduma za ziada atatoa taarifa ya uwepo wa huduma za ziada kupitia menyu ya huduma, meseji wakati wa maulizo ya salio, ama meseji ya uthibitisho wa kuongeza salio. Ili kusajili huduma ya ziada katika namba yake, mlaji atachagua kutoka katika menyu ya huduma au kutuma ujumbe mfupi wenye chaguo la huduma anayoihitaji. 

Mlaji atapokea ujumbe kutoka kwa mtoa huduma za ziada ikieleza masharti na vigezo vya huduma hiyo, ikiwemo gharama za huduma; kipindi ambacho huduma imewezeshwa; na namna ya kujiondoa katika huduma hiyo. Baada ya kuridhika na masharti na vigezo, mlaji atathibitisha ili huduma hiyo kuwezeshwa katika namba yake. Baada ya hapo, mtoa huduma za ziada atatuma ujumbe wa kuthibitisha kuwezeshwa kwa huduma iliyoombwa (activation). 

8. Aidha, kwa kutumia njia ya sauti (IVR) na namba maalum (USSD), pindi mlaji atakapopiga namba ya IVR ama USSD, mlaji atapokea tangazo lililorekodiwa ama orodha ya huduma za ziada zinazopatikana pamoja na masharti na vigezo ikiwa ni pamoja na gharama na kipindi cha huduma hizo. Baada ya mlaji kuchagua kwa kubonyeza kitufe kinachohusika, atapokea uthibitisho ndani ya dakika 15 kwamba maombi ya kuwezeshwa kwa huduma yamepokelewa na yanashughulikiwa. Mlaji atapokea tangazo lililorekodiwa kwamba huduma iliyochaguliwa imewezeshwa. Ikiwa amekosea kubonyeza kitufe, mlaji atataarifiwa na orodha kurudiwa tena. 

9. Kanuni zinamtaka mtoa huduma za ziada, kuweka mfumo wa kumuwezesha mlaji kujiondoa katika huduma za ziada (opt out/de-activation) ambao ni rahisi na wa uwazi kwa kutumia ujumbe wa maandishi (SMS) ama Huduma ya sauti (Interactive Voice Request – IVR). Mamlaka inawajibika kutoa namba (short code) kwa watoa huduma za ziada ili kuwezesha mlaji kujiondoa katika huduma hizo. 

10. Ili kumuwezesha mlaji kujiondoa kwenye huduma za ziada kwa kutumia njia ya SMS, mlaji atatuma ujumbe mfupi wa maandishi; au kutumia njia ya sauti kwa kupiga namba ya IVR au USSD ambapo mlaji atapokea ujumbe unaomjulisha orodha ya huduma za ziada zilizowezeshwa katika namba yake na kuchagua huduma anayohitaji ili iweze kuondolewa. Mtoa huduma atatuma ujumbe wa maandishi unaohitaji mlaji athibitishe nia yake ya kutaka kujiondoa katika huduma husika. Baada ya kupokea uthibitisho wa kujiondoa kutoka kwa mlaji, mtoa huduma za ziada ataondoa huduma hiyo katika namba ya mlaji. Endapo ikitokea mlaji amekosea, mtoa huduma za ziada atatuma ujumbe mfupi wa maandishi ili kumjulisha mlaji kuhusu kosa lililopo na chaguo la kurudia zoezi husika. Baaada ya mlaji kufanikisha kujiondoa, mtoa huduma za ziada atatuma ujumbe kuthibitisha kwamba huduma iliyochaguliwa imeondolewa katika namba ya mlaji. 

11. Aidha, Ili mlaji aweze kujiondoa katika huduma za ziada kwa njia ya sauti (IVR), baada ya kupiga namba ya IVR, mlaji atapata tangazo lililorekodiwa lenye orodha ya huduma za VAS zilizowezeshwa katika namba yake. Baada ya kukubaliana na masharti na vigezo, mlaji atachagua huduma ya ziada ya kuondolewa kwa kubonyeza kitufe kinachohusika na atapokea uthibitisho ndani ya sekunde sitini kwamba ombi la kujiondoa limepokewa na linafanyiwa kazi. Iwapo atakuwa amebonyeza kitufe kisichohusika, mlaji atajulishwa na orodha ya huduma za ziada itarudiwa ili zoezi hilo liweze kurudiwa. Ikiwa mlaji atakosea kwa mara nyingine simu yake itahamishiwa katika kituo cha huduma kwa mteja (call centre) cha mtoa huduma za ziada. 

Ndugu waandishi wa habari 
12. Katika kutoa matangazo ya promosheni ya huduma za ziada, mtoa huduma za ziada atazingatia Kanuni za Sheria ya EPOCA za kumlinda mteja (Consumer Protection) za mwaka 2011. Mtoa huduma atatangaza kwa mlaji aidha wakati wa kuuliza salio, ama kupitia meseji ya uthibitisho baada ya kuongeza salio ama katika menyu ya mtoa huduma. 

Mtoa huduma za ziada hatajihusisha katika kutoa matangazo yasiyoombwa na mlaji kwa njia ya kielektroniki ila tu pale ambapo aidha mlaji ameridhia, ama mwanzoni mwa mawasiliano ataweka wazi utambulisho wa mtoa huduma za ziada (ama mhusika aliyepo kwa niaba) na madhumuni ya mawasiliano hayo; ama mawasiliano yanatoa mchanganuo wa gharama za bidhaa ama huduma ambayo inahusika katika mawasiliano. 

Ndugu wananchi 
13. Kwa mujibu wa Kanuni Mpya za Huduma za Ziada za Mwaka 2015, Mlaji anawajibu ufuatao; 

i. Kuridhia huduma kwa kukubali masharti na vigezo vya huduma kama ilivyoelekezwa katika kanuni hizi; 

ii. Baada ya kuridhia masharti na vigezo vya huduma kutoka kwa mtoa huduma za VAS, mtumiaji atabanwa na masharti na vigezo hivyo. 

14. Aidha, ni vema ieleweke kuwa kwenye Kanuni ya kumi (10) ya Kanuni hizi Mpya za Huduma za Ziada Kanuni hiyo inaelekeza kuwa mtu yoyote atakayekiuka vipengele vya Kanuni hizi anatenda kosa kisheria na atawajibika kulipa faini ambayo si chini ya shilingi milioni tano ama kifungo kisichozidi miezi mitatu ama vyote kwa pamoja. Kanuni Mpya inapatikana kwenye tovuti ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia www.mst.go.tz

15. Natoa rai kwa watoa huduma za ziada kuwa waendelee kuzingatia Kanuni hizi katika kuwapatia wateja wao huduma za ziada zenye bora na viwango vinavyotakiwa na walaji kuhakikisha kuwa wanapatiwa huduma za ziada inayostahili na waliyoomba kwa kuwa teknolojia imerahisha utaratibu wa utoaji na upokeaji wa huduma za ziada. 

Imetolewa na; 
Prisca J. Ulomi 
Msemaji 
Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia 
Asanteni kwa kunisikiliza. 

No comments: