Wednesday, December 2, 2015

IJUE BIASHARA YA UWAKALA KISHERIA.

NA  BASHIR  YAKUB -
WAPO mawakala  na  wapo  wanaohitaji  kuwa  mawakala, Kwa  sasa biashara  ya  uwakala  ni  kubwa mno, wapo mawakala   mitandao  ya  simu kama tigo, Airtel, voda n.k, mawakala makampuni  ya  usafirishaji  kama mabasi,  malori n.k , na  makampuni  mengine  mengi. Mtindo  wa  biashara  ya  uwakala  umekua  sana  katika  siku  za  hivi  karibuni. 

Ni  kutokana  na  ongezeko  la  makampuni  na   kukua  kwa  biashara, Upo  umuhimu  mkubwa  wa  kuijua  biashara  ya  uwakala  kwa  undani   hasa  katika  misingi  ya  kisheria .

 Hii  itakusaidia  kuzijua  haki  zako, usipozijua  haki  zako  za  kisheria  katika  biashara  kama  hii   ni  vigumu  kunufaika. Hii  ni  kwasabbu   hutojua  unastahili  nini  na  nini  hustahili.  Ili kuliepuka hili  unajikuta katika  ulazima  wa  kuzijua  taratibu  za  kisheria  zinazohusu  uwakala. Usiingie  katika  biashara  hii  bila  kujua  japo  mambo  kidogo ya  msingi  ya kisheria  yanayohusu  uwakala.

1.WAKALA   NI  NANI.
Sura  ya  345  kifungu  cha 134  cha  sheria ya   mikataba  kinaeleza  nini  maana  ya  wakala.  Kinasema  kuwa  wakala  ni mtu   aliyeajiriwa  kufanya  kazi  au  kitu  chochote  kwa  niaba  ya  mwingine au  kumwakilisha  mtu  mwingine  katika  shughuli  fulani.  Kwahiyo  wakala  ni  mtu  anayesimama  badala  ya  mtu mwingine. 

Huyo  mtu  mwingine  huitwa  mhusika  mkuu, Kwahiyo  wakala  hufanya kazi kwa  niaba  ya  mhusika  mkuu, Humwakilisha  mhusika mkuu.

2.   SIFA  ZA  KUWA  WAKALA.
Vifungu  vya  135 na  136  vinaeleza  sifa  za  mtu  kuwa  wakala  au  kuwa  mhusika  mkuu, Vinaeleza  kuwa  mtu  yeyote  mwenye  umri  wa  mtu  mzima  yaani  mwenye  umri  wa  miaka  18  na  kwenda  mbele   anaweza  kuwa  wakala. 

Lakini  pia  ni  lazima  awe  na  akili  timamu,  Kwa  sifa  hizi  pia  unaweza  kuwa  mhusika  mkuu,,hata  hivyo  hizi  ni sifa  za  jumla  za  kisheria,  yamkini  zipo  sifa  nyingine  kutegemea  na  mhusika  mkuu  anahitaji  wakala  wa  aina  gani  kwa ajili  ya  biashara  zake.

3.  MAMLAKA   ALIYONAYO  WAKALA.
Kwa  mujibu  wa  kifungu  cha  38 wakala  anayo  mamlaka  makuu  ya  aina  mbili, Kwanza   mamlaka  ya  kutamkwa (expres) na  pili  mamlaka  ya  kumaanisha(implied). Mamlaka  ya  kutamkwa  ni  yale  yote  ambayo  ameambiwa  kwa  mdomo  au  kwa  maandishi kuyatekeleza .  
Ni  yale  yaliyo  katika  mkataba  wake  alioingia  na  mhusika  mkuu.

Pili  ni  mamlaka  ya  kumaanisha. 
Haya  hayapo  katika  mkataba  wake   na  wala hakuambiwa  na  mhusika  mkuu  lakini  ameyatekeleza. Haya    ni  yale ambayo  wakala  huyatekeleza  kwa  nia  nzuri  au  kwa  lengo  la  kuikoa  biashara  na  jambo  fulani  ambalo  limetokea  ama  kwa dharula au vinginevyo.  

Ikiwa  wakala  amefanya  jambo  jema  na  kwa  nia  njema  hata  kama  halipo katika  makubaliano  kati  yake  na mhusika  mkuu  basi  jambo  hilo  huhesabika  ni  sehemu  ya  mamlaka  yake  na  mhusika  mkuu  hawezi  kukataa  kuliwajibikia  kwa  kisingizio  kuwa  halipo  katika  makubaliano.

4.  HAKI   YA WAKALA  KUZUIA  MALIPO  YA  MHUSIKA  MKUU.
Ikiwa  wakala  anafanya  biashara  ambayo  anatakiwa  kuwasilisha  pesa  za  mauzo  kwa  mhusika  mkuu na  ikatokea  kuwa  hajalipwa  malipo  yake   basi  anaweza  kuzuia  malipo  ya  pesa  hizo  ili  kufidia  hela  anayodai. Muhimu  ni  kuwa  asizuie  pesa  nyingi  zaidi  kuliko  kiasi  anachodai.

Pamoja  na  hayo kifungu  cha  172 kinasema  hakutakuwa  na  malipo  kwa  wakala  kwa  kazi  aliyoiharibu. Wakala  anatakiwa  kuwa  mwangalifu, mtiifu  kwa  maelekezo  ya  mhusika  mkuu, na kujiepusha  na  uzembe  au  kutojali. Hasara  anayoisababisha  kutokana  na  haya itakatwa  katika  malipo  yake.

5.  WAKALA   KULIPWA   PESA   ISIYOKUWA  KATIKA  MAKUBALIANO.
Ikiwa  wakala  amefanya  jambo  jema  na  la  faida  kwa  mhusika  mkuu basi  wakala  anastahili  malipo  ya  jambo  hilo  hata  kama  malipo  hayo  hayapo  katika  makubaliano. Hii  ni  kwa  mujibu  wa  kifungu  cha  174  cha  sheria  ya   mikataba.

6.  FIDIA  KWA  KUJIONDOA  KATIKA  UWAKALA.
Yeyote  kati  ya  mhusika  mkuu  au  wakala  anaweza  kujiondoa  katika  uwakala. Yeyote  atakayejiondoa  katika  uwakala  kabla  ya  muda  wa  makubaliano  kuisha basi  atalazimika  kumlipa  fidia  mwingine.  Akijiondoa  wakala  fidia  italipwa  kwa  mhusika  mkuu halikadhalika  mhusika  mkuu  akijiondoa  fidia  italipwa  kwa  wakala.  Taarifa  ya  muda  wa  kutosha  ni  lazima  itolewe  kabla  ya  kujiondoa  la  sivyo  aliyejiondoa  atalazimika  kulipa  fidia  nyingine  zaidi  kwa madhara  yaliyotokana  na  kujiondoa  kwake  ghafla.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.    0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com

1 comment:

Unknown said...

Je kodi kwa serikali juu ya wakala ikoje?