Monday, November 2, 2015

WATAALAM WA TAKWIMU KUTOKA OFISI ZA TAKWIMU BARANI AFRIKA

Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Afrika Kusini Risenga Maluleke akizungumza leo na waandishi wa habari kuhusu madhumuni ya mkutano wa watalaam wa takwimu kutoka nchi mbalimbali barani Afrika ambapo wamekutana kujadili Mfumo wa Uongozi Bora katika Ofisi za Takwimu pamoja na Uboreshaji wa Mitaala ya Ufundishaji wa Masomo ya Takwimu. Mkutano huo ni wa siku tano na unafanyika katika hoteli ya Golden Tulip iliyopo Jijini Dar es Salaam. 
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akizungumza leo na waandishi wa habari kuhusu mkutano wa siku tano ambao umekutanisha watalaam wa takwimu kutoka nchi mbalimbali barani Afrika kujadili Mfumo wa Uongozi Bora katika Ofisi za Takwimu pamoja na Uboreshaji wa Mitaala ya Ufundishaji wa Masomo ya Takwimu. Mkutano huo unafanyika katika hoteli ya Golden Tulip iliyopo Jijini Dar es Salaam. 
 Baadhi ya wakuu wa Ofisi za Takwimu kutoka barani Afrika wakifuatilia kwa makini majadiliano wakati wa mkutano wa kujadili Mfumo wa Uongozi Bora katika Ofisi za Takwimu pamoja na Uboreshaji wa Mitaala ya Ufundishaji wa Masomo ya Takwimu. Mkutano huo ni wa siku tano na unafanyika katika hoteli ya Golden Tulip iliyopo Jijini Dar es Salaam.
 (PICHA ZOTE NA VERONICA KAZIMOTO)

VIONGOZI wa Ofisi za Takwimu barani Afrika leo wamekutana kujadili Mfumo wa Uongozi Bora katika Ofisi hizo pamoja na Uboreshaji wa Mitaala ya Ufundishaji wa Masomo ya Takwimu katika nchi za Afrika.

Wakizungumza katika mkutano wa wataalam wa takwimu ulioanza leo Jijini Dar es Salaam, viongozi hao wamesema ili takwimu bora zipatikane kwa wakati, ni lazima kuwepo na mfumo bora wa uongozi pamoja na wataalamu waliobobea katika fani ya takwimu.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt. Albina Chuwa amesema lengo la mkutano huo ni kujadili mfumo wa uongozi bora katika Ofisi za Takwimu pamoja na namna ya kuboresha mitaala ya ufundishaji wa masomo ya takwimu barani Afrika.

“Leo tupo hapa wataalamu wa takwimu kutoka zaidi ya mataifa 25 barani Afrika ili kujadili namna ya kuboresha mifumo yetu ya uongozi katika Ofisi za Takwimu pamoja na kujadili mbinu bora za kuimarisha utoaji wa mafunzo kwa watakwimu vijana hasa kupitia upya mitaala ya ufundishaji,” amesema Dkt. Chuwa.

Dkt. Chuwa amesema kuimarishwa kwa mfumo wa uongozi pamoja na kuboresha mafunzo kwa wakwimu kutasaidia katika ukusanyaji wa takwimu bora zitakazotumika katika kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu wa Afrika ya Kusini, Risega Maluleke amesema mataifa mengi ya Afrika yanakabiliwa na changamoto kubwa ya kutokuwa na uwezo wa kujitegemea kifedha kitu ambacho hukwamisha upatikanaji wa takwimu kwa wakati.

Amesema licha ya changamoto hiyo, kwa kiasi kikubwa kazi ya ukusanyaji wa takwimu imekuwa ikifanyika kwa ufanisi mkubwa kutoka kwa watalaam hao wa takwimu na hivyo kupitia mkutano huu, wataweza kujadili namna ya kuboresha uimarishaji wa Ofisi za Takwimu.

Maluleke amesema ni vyema Serikali zikaziwezesha ofisi za ukusanyaji wa takwimu ili ziweze kujitegemea kibajeti na kuboresha utendaji kazi wake katika kuhakikisha takwimu bora zinapatikana kwa wakati muafaka.

Mkutano huo wa siku tano unatarajia kumalizika tarehe 06 Novemba, 2015 ambapo wataalam takribani 30 wamekutana kujadili Mfumo wa Uongozi Bora katika Ofisi hizo pamoja na Uboreshaji wa Mitaala ya Ufundishaji wa Masomo ya Takwimu katika nchi za Afrika.

No comments: