Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT), Bw. Gerald Mwanilwa akizungumza na Mgeni rasmi wa mafunzo ya program ya TEAMMATE kwa ajili ya wakaguzi kutoka NAOT na Wizara ya Fedha, Kaimu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bibi Wendy Massoy. Kushoto ni Bw. Slyvester Kibona, Mkaguzi Mkuu wa Nje wa Mkoa wa Morogoro. Mafunzo hayo yanafanyika mkoani Morogoro kuanzia tarehe 02 hadi 06 Novemba, 2015.
Mkurugenzi wa msaidizi (Mafunzo) Bibi Felister Tirutangwa akizungumza wakati wa mafunzo ya program ya TEAMMATE kwa ajili ya wakaguzi kutoka NAOT na Wizara ya Fedha. Mafunzo hayo yanafanyika mkoani Morogoro kuanzia tarehe 02 hadi 06 Novemba, 2015.
Baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) na Wizara ya Fedha wakifuatilia kwa umakini mafunzo ya program ya TEAMMATE. Mafunzo hayo yanafanyika mkoani Morogoro kuanzia tarehe 02 hadi 06 Novemba, 2015.
Mgeni rasmi wa mafunzo ya program ya TEAMMATE kwa ajili ya wakaguzi kutoka NAOT na Wizara ya Fedha, Kaimu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bibi Wendy Massoy akizungumza na wanahabari kuhusu mafunzo hayo.
Mgeni rasmi wa mafunzo ya program ya TEAMMATE kwa ajili ya wakaguzi kutoka NAOT na Wizara ya Fedha, Kaimu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bibi Wendy Massoy akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wanaohudhuria mafunzo hayo.
Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT), Bw. Gerald Mwanilwa akizungumza na wanahabari kuhusu mchango wa Serikali ya Awamu ya Nne katika kuhakikisha uhuru wa CAG unapatikana.
Na Mwandishi wetu, Morogoro
Watumishi wa umma nchini wenye fani ya ukaguzi, wametakiwa kutumia weledi katika utendaji kazi zao hali itakayoongeza ufanisi katika usimamizi wa rasilimali za umma.
Wito huo umetolewa na Kaimu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bibi Wendy Massoy wakati akifungua mafunzo ya program ya TEAMMATE kwa ajili ya wakaguzi kutoka Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi na Wizara ya Fedha.
Bibi Massoy amesema, viwango vya ukaguzi Kimataifa vinahitaji mkaguzi kuhifadhi taarifa zake za ukaguzi vizuri ili kuwezesha mkaguzi mwengine kuweza kufikia hitimisho moja kulingana na kazi iliyofanywa na Mkaguzi mwengine.
“Programu ya TEAMMATE hutoa fursa kwa wakaguzi kwa kuwawezesha kuhifadhi taarifa zake za ukaguzi vizuri hivyo kuwafanya kutii viwango vya ukaguzi Kimataifa vya ukaguzi,” alisema Bibi Massoy.
Kaimu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ameongeza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wakaguzi hao katika kazi yao ya ukaguzi.
“Nawasihi muweze kutumia fursa hii kujiendeleza na kutekeleza utaratibu wa kaguzi wa mwongozo kwa vile wengi wa hatua na taratibu wamekuwa umeboreshwa katika Teammate Programu.
Akizungumzia mchango wa Serikali ya Awamu ya Nne katika kuiboresha Ofisi ya CAG, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Gerald Mwanilwa alisema kwa kiasi kikubwa mafanikio ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi imechagizwa na uamuzi wa dhati wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete kuimarisha taasisi za utawala bora, maadili na udhibiti, ikiwemo NAOT.
Bw. Mwanilwa aliongeza kuwa Rais alifanya hivyo kwa kuboresha sheria, kuongeza uhuru wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, kuongeza uwazi wa taarifa za Ofisi hiyo kwa kupeleka Ripoti za CAG kwa mara ya kwanza Bungeni pamoja na kuboresha mazingira ya kazi.
“Kwa mara ya kwanza Rais Jakaya Mrisho Kikwete aliitisha vikao mbalimbali, kwa nyakati tofauti na Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya na Mamlaka za Serikali za Mitaa kusisitiza umuhimu wa kuzipitia na kuzifanyia kazi taarifa zinazotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Hii imeleta mwamko mpya katika kuona umuhimu wa ripoti hizi na kutumika katika kufanya maamuzi mbalimbali serikalini,” alisema.
Bw. Mwanilwa aliongeza Katika Uongozi wa Awamu ya Nne NAOT ilishuhudia uanzishwaji wa Sheria ya Ukaguzi wa Umma, ambapo serikali ilitunga Sheria ya Ukaguzi wa Umma ya Mwaka 2008 pamoja na kanuni zake za mwaka 2009. Sheria hii iliongeza wigo na uhuru wa Ofisi hii katika kutekeleza majukumu yake Kikatiba.
Kuhusu Bajeti ya uendeshaji wa NAOT, Bw. Mwanilwa aliongeza: “Rais Kikwete aliongeza Bajeti ya Ofisi ya Ukaguzi ambapo Serikali iliboresha utaratibu na mchakato mzima wa kupitisha bajeti ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali uliowezesha bajeti ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kuongezeka kwa asilimia 306% katika kipindi cha miaka mitano, kuanzia mwaka wa fedha wa 2008/9 hadi 2013/14.”
Jumla ya wakaguzi 65 kutoka Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi na kutoka 25 Wizara ya Fedha wanahudhuria mafunzo hayo ya siku tano yanayofanyika mkoani Morogoro.
No comments:
Post a Comment