Katibu wa soko la Tabata Muslim lililopo Manispaa ya Ilala, John Nombo (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), Dar es Salaam leo asubuhi, kuhusu kupungua kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia katika soko hilo baada ya Shirika la Equality for Growth (EfG), kutoa mafunzo ya kupinga ukatili huo katika masoko sita ya Manispaa hiyo. Kulia ni Mwezeshaji wa Sheria wa Soko hilo, Aisha Juma na Saada Ngunde.
Mwezeshaji wa Sheria katika soko hilo, Saada Ngande akizungumza katika mkutano huo.
Mwezeshaji wa Sheria, Irene Daniel (kushoto), akizungumza kuhusu kazi alizofanya za kusaidia watu kujua haki zao. Kulia ni Mwenyekiti mstaafu wa Umoja wa Wanawake katika Soko hilo, Happyness Urono.
Mwenyekiti mstaafu wa Umoja wa Wanawake katika Soko hilo, Happyness Urono, akizungumzia changamoto walizokuwa nazo katika soko hilo.
Mwezeshaji wa Sheria, Irene Daniel akionesha mabango yanayohamasisha masuala ya haki ya mwanamke katika soko hilo.
Na Dotto Mwaibale.
UJASIRI wa Wawezeshaji Sheria wanawake katika soko la Tabata Muslim lililopo Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam umesaidia kupunguza vitendo vya ukatili wa jinsia katika soko hilo.
Hayo yalielezwa na Mwezeshaji wa sheria katika soko hilo, Irene Daniel wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi ambao wapo katika ziara ya kutembelea masoko ya manispaa hiyo kuona jinsi vitendo vya ukatili wa kijinsia vilivyopungua baada ya Shirika la Equality for Growth kutoa mafunzo ya kupinga ukatili huo katika masoko hayo.
"Ujasiri tuliofundishwa sisi wawezeshaji wa sheria katika masoko na EfG wa kufuatilia matukio ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia umesaidia sana kupunguza vitendo hivyo katika soko letu" alisema Daniel.
Akitolea mfano alisema mbali na kufuatilia masuala hayo ya ukatili katika soko hilo pia aliweza kuisaidia familia moja baada ya baba wa familia hiyo kutaka kumfanyia kitendo cha udhalilishaji mke wake ambapo alikwenda kuzungumza na baba huyo ambaye alikubali kubadilika.
Alisema baba huyo ambaye alikuwa anashinda vijiweni baada ya kujitambua alimpatia mtaji wa fedha ambapo alianzisha biashara ya maji na sasa msuguano na mke wake umekwisha na wamefikia hatua ya kuwa na eneo lao la biashara ya mama lishe na uuzaji wa maji.
Katibu wa soko hilo John Nombo alisema changamoto kubwa waliyokuwa nayo katika soko hilo ni lugha za matusi, wateja kuvaa nguo fupi zilizokuwa zikionesha miili yao hivyo kuwafanya vijana kuwa na matamanio na kuanza kuwatomasa lakini hivi sasa vitendo hivyo havipo tena.
Mwezeshaji wa sheria Saada Juma alilalamikia jeshi la polisi kituo cha Tabata kushindwa kushughulikia kesi ya mdogo wake aliye dhalilishwa na kijana mmoja katika soko hilo ambapo licha ya kijana huyo kufahamika alipo lakini polisi wameshindwa kumtia nguvuni.
Mwenyekiti mstaafu wa Umoja wa Wanawake katika soko hilo, Happyness Urono alisema vitendo vya udhalilishaji katika soko hilo hakuna kwani mafunzo waliopatiwa na EfG yamewafanya wajitambue na kuzijua haki zao ambapo ametoa mwito kwa wanawake kuzidisha umoja wao katika kila jambo.
(Imeandaliwa na mtandao wa www. habari za jamii.com.
No comments:
Post a Comment