Friday, November 20, 2015

SERIKALI ZA MITAA ZAONGEZA MAPATO KUPITIA MFUMO WA UKUSANYAJI MAPATO KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

 Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Waziri Mkuu- TAMISEMI Bi. Rebecca Kwandu akifurahia jambo na waandishi wa habari (hawapo pichani)leo jijini Dar es Salaam wakati akiwaeleza mafanikio ya mfumo wa ukusanyaji mapato kwa njia ya kielektroniki katika mamlaka za Serikali za Mitaa (LGRCIS). Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Mifumo ya TEHAMA wa ofisi hiyo Bw. Mtani Yangwe na kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari (MAELEZO) Bi. Zamaradi Kawawa.
 Mkurugenzi Msaidizi Mifumo ya TEHAMA kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu- TAMISEMI Bw. Mtani Yangwe akifafanua kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dar es Salaam namna mfumo wa wa ukusanyaji mapato kwa njia ya kielektroniki unavyorahisisha ulipaji wa kodi mbalimbali kwa kuhusisha mifumo ya kielektroniki ya malipo na mifumo ya kibenki. Kulia ni Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa ofisi hiyo Bi. Rebecca Kwandu.
 Afisa Msimamizi wa Fedha Ofisi ya Waziri Mkuu- TAMISEMI Bw. Elisa Rwamiago akiwaeleza waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Dar es Salaam kuhusu mikakati mbalimbali ya kuongeza mapato ya mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuondokana na utegemezi wa ruzuku kutoka Serikali Kuu. Kushoto ni Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa ofisi hiyo Bi. Rebecca Kwandu.
 Mhasibu wa Mfumo wa Mapato Jiji la Arusha Bw. Prosper Mlacha akiwaeleza waandishi wa habari leo Dar es Salaam kuhusu ongezeko la mapato katika jiji la Arusha kutokana na matumizi ya mfumo wa ukusanyaji mapato kwa njia ya kielektroniki (LGRCIS) ambapo kwa mwaka 2014/2015 zimekusanywa bilioni 10.7.
 Baadhi ya waandishi wa habari wakifuatilia mkutano wa maafisa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu- TAMISEMI uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.

Picha zote na Fatma Salum (MAELEZO)

Na Georgina Misama.
SERIKALI imeboresha matumizi ya mfumo wa ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielekitroniki katika mamlaka za serikali za mitaa.

Hayo yamesemwa na msemaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI) Bi. Rebecca Kwandu leo jijini Dar es salaam.

Bi Rebecca amesema kuwa TAMISEMI imekuwa ikiendelea kwa nyakati tofauti kufanya maboresho mbalimbali ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa jamii na kuzisaidia mamlaka hizo katika kuongeza mapato ya ndani na kuondokana na uteuzi wa ruzuku kutoka Serikali Kuu.

“Ofisi ya Waziri Mkuu –TAMISEMI iliamua kuanzisha mfuko wa Local Governement Collection Information System (LGRCIS) baada ya kufanya tafiti mbalimbali kwa nyakati tofauti na zilionyesha kuwa hakukuwa na mfumo wowote wa kielektroniki kurahisisha ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya Halmashauri” alifafanua Bi. Rebecca.

Mbali na hayo Msemaji huyo alisema kuwa miongoni mwa malengo makuu ya kuanzishwa kwa mfumo wa LGRCIS ni pamoja na kupata taarifa za walipa kodi wa mamlaka za serikali za mitaa na kuhifadhiwa kwa usahihi katika kanzi data ya mfumo.

“ Kupata takwimu sahihi ya vyanzo vya mapato na kufanya usuluhishi kati ya kilichokusanywa na kilichotarajiwa kukusanywa, kuongeza mapato kwa kasi zaidi kwa kuwa na uhakika wa makusanyo katika vyanzo vikuu, kuweka uwazi na uwajibikija katika makusanyo ya mapato,na kuhimarisha ulipaji miamala ya kodi na tozo itakayofanywa na walipakodi” aliongeza Bi Rebecca.

Pia alisema kuwa matarajio ya TAMISEMI ni kuwa mfumo wa LGRCIS utaleta mabadiliko makubwa katika Halmashaurina kuachana na utegemezi wa ruzuku kutoka Serikali kuu.

Hata hivyo teknolojia pekee ya matumizi ya TEHAMA haiwezi kuleta mabadiliko pasipo fikra za watumiaji wa mfumo wa walipakodi kubadili mazoea.

No comments: