Sekta
ya ardhi nchini ni ya kipekee katika uthibiti wa mabadiliko ya tabia nchi kwa
kuwa ndiyo sekta pekee ambapo ndipo uzalishaji na uondoaji wa kaboni hutokea.
Mfumo
wa matumizi mapana ya ardhi ambao siyo endelevu unapaswa ubadilishwe ili nafasi
yake ichukuliwe na matumizi ambayo ni sahihi na endelevu zaidi tofauti na hali
ilivyokuwa mwanzo. Hatua hiyo ni pamoja na kutumia vyema ardhi iliyopo kwa
kupunguza uzalishaji wa gesi joto unaotokana na ardhi.
Mnamo
mwaka 2009, Ubalozi wa Ufalme wa Norway nchini Tanzania ulianza kuwa chachu ya uhifadhili
wa miradi saba ya majaribio ya Mkakati wa Kupunguza Ukataji Hovyo na Uharibifu wa Misitu (MKUHUMI) kwa kutoa dola
za Kimarekani zipatazo milioni 100 kufadhili mradi huo.
Fedha
hizo zilipelekwa kwenye taasisi za elimu ya juu nchini ambazo zinajukumu la
kuandaa wataalamu mbalimbali.
Taasisi
zilizopata fedha hizo ni pamoja na Chuo Kukuu Cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kwa
lengo la kuendesha mafunzo na utafiti.
Fedha
nyingine zilipelekwa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, kitivo cha Tathmini ya
Rasilimali ambako huko pia waliingia mkataba na Asasi zisizo za Kiserikali (NGO’s)
za hapa nchini ili kutekeleza mkakati wa MKUHUMI vijijini.
Mkurugenzi
wa Idara ya Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt Julius Ningu hivi karibuni
alibainisha kuwa MKUHUMI ni moja ya maeneo ya utekelezaji wa mkataba wa
mabadiliko ya tabia nchi ambao unalenga kupunguza uzalishaji wa gesi joto katika
sekta ya misitu, mkataba huo uliosainiwa katika mkutano uliofanyika nchini
Indonesia mwaka 2008.
“Gesi
joto ni mchanganyiko wa gesi mbali mbali zinazozalishwa kutokana na shughuli anazofanya
binadamu kama vile viwanda, kilimo, sekta
ya usafirishaji, magari, na mitambo inayotoa gesi mbalimbali ambayo hupanda
hadi kufikia umbali wa kilometa moja hadi moja na nusu kutoka uso wa dunia na huko
hutengeneza utando mzito (tabaka la gesi joto)”, alisema Dkt Ningu.
Ongezeko
la hewa ukaa unasababishwa na uharibifu wa misitu kutokana na shughuli za kilimo
cha kuhama hama na upanuzi wa makazi ya watu na miji ambapo maeneo ya misitu
yanabadilishwa na kuwa makazi ya watu, ufugaji huria usio endelevu, uchomaji moto wa
misitu unaofanywa kwa makusudi kutokana na mila na desturi pamoja na shughuli
za viwanda zinazofanyika katika nchi zinazoendelea.
Madhumuni
ya mkakati MKUHUMI ni kushughulikia masuala ya ardhi, misitu na usimamizi wa
kaboni wenye tija kwa namna mbalimbali ikiwamo ushirikishwaji mpana wa wadau
katika ngazi mbalimbali.
Aidha,
mkakati huo unalenga kupunguza uzalishaji wa kaboni itokanayo na matumizi ya
ardhi kwa kiwango kinachoweza kuhakikiwa na kuzisaidia kaya masikini kuainisha
vyanzo mbadala vya kujipatia mapato ambavyo havitegemei uvunaji wa misitu usio endelevu.
Ili
kuwa na maendeleo endelevu ya nchi, mradi wa MKUKUMI umeainisha malengo mengine
ambayo ni kujenga utayari wa wananchi katika shughuli zake nchini, kufanya
majaribio ya kisera kupata matokeo ya bora ya MKUHUMI na kuwezesha wadau mazingira
kuwa na ushirikiano wenye tija.
Katika
kuimarisha juhudi hizo za kuboresha mazingira na kupunguza hewa ya kaboni, zipo
pia Asasi zisizo za kiserikali (NGO’S) zinazotekeleza mradi wa MKUHUMI hapa
nchini.
Asasi
hizo ni pamoja na shirika la kimataifa la CARE, Taasisi ya Jane Goodall,
mradi wa kaboni wa shirika la The African
Wildlife Foundation, shirika la World Wildlife Foundation na shirika la World
Wildlife Fund.
Asasi
nyingine zinazojishughulisha na kupunguza hewa ya kaboni ni Shirika la
Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania, Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu
Tanzania (MJUMITA), Shirika la Uhifadhi wa Mpingo na maendeleo na Taasisi ya Wildlife
Conservation Society.
Asasi
hizo zinafanya kazi hiyo kupunguza hewa ya kaboni katika maeneo ya Kusini
Magharibi mwa Tanzania, Kigoma na Uvinza, wilaya za Lindi, Kigoma, Mpwapwa,
Kondoa na Zanzibar.
Maeneo
mengine ambayo miradi ya MKUHUMI inatekelezwa hapa nchini ni zile sehemu yenye
aina nyingi za misitu kama vile nyanda za juu milimani, misitu ya miombo kwenye
maeneo yenye ukame na maeneo ya maji maji, misitu ya ukanda wa Pwani, mapori ya
acacia, na maeneo yenye misitu ya mikoko.
Akizungumzia
suala hilo hivi karibuni jijini Dar-es-Salaam, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa
Rais Bw. Sazi Salula alipokuwa katika mkutano wa wadau wa mazingira uliohusu
utekelezaji wa miradi ya majaribio ya MKUHUMI, alisema kuwa Watanzania hawana
budi kuzingatia namna bora ya kuhifadhi mazingira, upangaji wa matumizi bora ya ardhi na utekelezaji wa mipango ili
kuleta tija na maendeleo endelevu nchini.
Naye
kiongozi wa miradi ya majaribio ya MKUHUMI ndugu Merja Makela alisema kuwa
taasisi yake imesifika kutokana na kutekeleza na kusimamia miradi hiyo kwa
makini katika maeneo husika nchini.
Athari
zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi kwenye misitu ni pamoja na hali ya
hewa kutofautiana kwa hali mbalimbali ikiwemo urefu wa msimu wa kiangazi au
masika ambayo huchangia uharibifu wa uzalishaji mazao, uwepo wa njaa na upotevu
wa amani ambapo baadhi ya makabila huingia kwenye mapigano ya kugombea ardhi.
Mbali
na hayo, athari nyingine inayotokana na mabadiliko ya tabia nchi ni pamoja na
kuwepo kwa mvua nyingi mfano El nino ambazo husababisha mafuriko, uharibifu wa
mali, upotevu wa maisha ya watu na mali zao pia ongezeko la fukuto la joto
katika uso wa dunia linasababisha ongezeko la ukame unaoathiri mazingira ambayo
ni mahali pao pa makazi.
MKUHUMI
katika kutekeleza majukumu yake imekuwa na faida nyingi zinazopatikana kutokana
na miradi hiyo ikiwa ni pamoja na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania
kwa kushirikiana na MJUMITA kuweza kutoa kiwango cha kaboni kilichohakikiwa kwa
ajili ya mauzo.
Aidha,
miradi MKUHUMI imeleta manufaa muhimu yasiyo ya kaboni yakijumuisha ongezeko la
usalama wa jamii wa kufanya maamuzi juu ya usimamizi wa maliasili zao pamoja na
msitu wa Masito Ugalla ulioko mkoani Kigoma wenye ekeri 93,000 uliokuwa
umesambaratika ulifanikiwa kurudishwa na wanyamapori walirudi na shughuli za
ufugaji ya nyuki ulianzishwa.
Kiasi
cha uzalishaji wa kaboni kimepunguzwa
kwa nchini kutoka tani 39,896 kwa mwaka
mmoja kuanzia 2012 katika eneo la Lindi, na tani 27,600 zimepunguzwa kwa mwaka
mmoja Kusini Mashariki mwa Tanzania katika misitu 10.
Manufaa
mengine ya mradi huo ni kuwa watu zaidi ya 50,000 nchini wamefikiwa na elimu ya
mazingira katika eneo la Kusini Magharibi
mwa Tanzania kupitia mradi wa Taasisi ya Wildlife Conservation Society.
Aidha,
miradi hiyo imewanufaisha wananchi maskini kwa kuhakikisha zinaongeza ufikaji
na ufanisi wa shughuli za mazingira zinawafikia kwa usawa pia kuwepo kwa mgawanyo sawa wa faida za kifedha
katika ngazi mbali mbali.
Miradi
hiyo imekuwa na manufaa makubwa ya ziada ya kaboni ikiwemo ulinzi zaidi wa haki
za miliki za ardhi na misitu, uboreshaji wa usimamizi wa maliasili, vyanzo vya
maji na kupunguza upotevu wa bioanuwai.
Katika
kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, shirika la mabadiliko ya tabia nchi
kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es salaam kupitia mkutano wa kimataifa
wa 21 uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es salaam ilikubalika kuwa Afrika
iwe na kauli moja ya kuwahamasisha
vijana wa jinsia zote washiriki kutoa
maoni na kuchangia masuala ya mabadiliko
ya tabia nchi.
Katika
mkutano huo, Makamu wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. Mohamed Gharib Bilali alisema kuwa kuna kila dalili ya maeneo ya ukame
kuongezeka kwa asilimia 5 hadi 8
barani Afrika ifikapo mwaka 2080
kutokana na matumizi ya nishati ambayo husababisha joto la dunia kuongezeka kwa
asilimia zaidi ya 0.74.
Miradi
ya MKUHUMI inakabiliwa na changamoto mbalimbali zilizojitokeza ikiwa ni pamoja
na kiwango cha chini cha uzoefu na uelewa wa taasisi zinazotekeleza au
kushughulikia masuala ya mazingira na fikra dhaifu miongoni mwa wananchi,
zinazohusisha usimamizi endelevu wa uvunaji wa misitu na ufuatiliaji dhaifu wa
matokeo.
No comments:
Post a Comment