Sunday, November 15, 2015

MAKALA MAALUM KUHUSU AMANI TANZANIA

 Na Eleuteri Mangi-MAELEZO

Nuru inapoiangazia dunia, huwaangazia viumbe vyote vilivyo hai na visivyo na uhai, viumbe vyenye uhai, hao hufurahia nuru hiyo kwa kuruka ruka na kucheza kufurahia nuru hiyo.

Kila ifikapo asubuhi na mapema, utasikia sauti na mili­o ya ndege wa angani, wanyama wa kufuga na waishio mwituni, milio na sauti za viumbe hao wakati mwingine kuashiria kuwa kumekucha ili waendelee kufurahia nuru inayowanaagazia kwa manufaa ya maisha yao. 

Wanadamu nao wakiwa kama viumbe hai wengine, huanza kujiandaa asubuhi na mapema kuelekea huku na kule kutafuta riziki ya kila siku ili maisha yao yaendelee kusonga mbele baada ya nuru kuwangazia.

Mwandishi wa makala haya anaifananisha nuru hiyo inayoiangazia dunia na Amani. Amani ni tunu adhimu, ni tunu yenye Baraka na fanaka, amani inapotamalaki duniani, binadamu na kila kiumbe chenye uhai huonesha furaha yake kwa namna kiumbe hicho kinavyoguswa na amani hiyo.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Sheria Na.15 ibara 3 ya 1984 nayo inajali na kuzingatia amani hiyo ndiyo maana inatamka kuwa “Sisi Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu na amani”.

Katika maisha ya kawaida ya kijamii amani ni ile hali ya raha na usalama bila ugomvi wowote ambapo kinyume chake ni fujo au vita.

Ndiyo maana Rais wa Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete aliwahi kusema “Amani yetu tuitunze kwa nguvu zote, maana haina mbadala wake, mbadala wa amani ni vita, mbadala wa upendo ni chuki, mbadala wa umoja ni mfarakano, amani siyo mboga ambayo utaitafuta kiurahisi”



Kwa umuhimu huo, kila mwaka Tanzania huungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku ya amani kila ifikapo Septemba 21, ambapo mahitaji ya matumaini ya amani yameonekana kuwa mbali katika dunia ya sasa iliyokumbwa na mizozo na mapigano.

Katika kuadhimisha siku hiyo mwaka huu, Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa (UN) Ban Ki- moon alitoa ujumbe wa siku hiyo ya amani duniani ambapo alisema kuwa hakuna kundi linaloweza kufanikisha kufikia ndoto ya amani zaidi ya vijana ambao alisema kwa sasa ni wengi.

“Viongozi hawana budi kuwekeza kwa vijana katika ujenzi wa amani, Aidha alisema sote tunaweza kuimarisha amani, Mashirika ya kiraia, kampuni na hata taasisi za kidini wote wanaweza kujenga dunia yenye amani zaidi”alisema Katibu Mkuu huyo wa UN.

Aliendela kusema kuwa ubia huo katika ujenzi wa amani ndio msingi wa ujumbe wa siku ya amani mwaka huu unaongozwa na na kauli ya mbiu isemayo “Ubia kwa amani utu kwa wote”.

Vijana ni nguzo imara ambayo inayoweza kujenga amani ya dunia ya leo, kuwekeza kwa vijana ni kupanda mbegu inayoota na kusitawi ikipandwa kwa muda mwafaka na kupata mahitaji yake kwa wakati ikiwemo maadili mema na wazazi, walezi, jumuiya, taasisi, na taifa kwa ujumla. 

Tanzania ikiwa sehemu ya dunia hii, haiwezi kujitenga na suala la amani siku zote kwa wakati wote miongoni mwa wananchi wake na hata mataifa mengine.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika nchini 2012, watu milioni 19.7 sawa  na asilimia 44 ya watu wote nchini ni watoto wenye umri chini ya miaka 15, vijana kuanzia miaka 15 hadi 35 wakiwa milioni 15.6 sawa na asilimia 35.
Mchanganuo huo unaashiria kuwa kundi la vijana kati ya miaka 18-35 lina watu milioni 11.8 sawa na asilimia 26, ambalo linakuwa na umuhimu wa kipekee nchini kisiasa na kiuchumi.

Kama nchi, Tanzania imeendelea kuwa ya mfano bora miongoni mwa mataifa ambapo zoezi la Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu nchini la kumchagua Rais, Wabunge na Madiwani umekamilika kwa amani na utulivu wakati wote tangu kuanza kwa michakato ya kuwapata wawakilishi wa vyama katika nafasi hizo, wakati wa kampeni ambapo wagombea wa nafasi mbalimbali walinadi sera za vyama vyao ili waweze kupewa ridhaa ya kuongoza katika nafasi zao kwa miaka mitano.

Zoezi la uchaguzi limekamilika ambapo Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amechaguliwa kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wake Samia Suluhu Hassan ambao walitangazwa washindi na kupewa Hati ya Ushindi huo na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) mnamo Oktoba 30, 2015 mbele ya viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, waangalizi wa Kimataifa, Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa Tanzania, waangalizi wa ndani ya nchi na wananchi kwa ujumla.

Zoezi la kuwapata viongozi lilifanyika kwa amani ambapo hata hali ya hewa ilikuwa ya kufurahisha na kuipamba siku hiyo kwa kuwa na mvua ilinyesha ambayo ni kielelezo cha amani ambayo hufurahiwa na viumbe vyote.

Kuonesha umhimu wa amani nchini, kila kiongozi na wananchi kwa nafasi zao wanaendelea kusisitiza amani, Mkuu wa Jeshi la Polisi Ernest Mangu kwa nafasi yake kama mkuu wa ulinzi na usalama kwa raia na mali zao wakati wote husisitiza na kuwahimiza Watanzania kwa ujumla kwa kuwasihi wadumishe amani na utulivu kama ilivyokuwepo wakati wote wa kampeni za uchaguzi mkuu kabla, wakati na baada ya uchaguzi huo Oktoba 25 mwaka huu.

Katika kudumisha amani nchini, kila mtu anajukumu la kutimiza ili kuimarisha amani kama ilivyojengwa na kuimarishwa na viongozi wa Serikali kwa Awamu zote tangu kupatikana kwa uhuru Disemba 9, mwaka 1961 na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili 26, 1964.

Awamu hizo za uongozi ni ile ya kwanza ilioongozwa na Muasisi wa taifa hili Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Awamu ya Pili ya Alhaji Alli Hassan Mwinyi, Benjamini William Mkapa Awamu ya Tatu, Dkt. Jakaya Kikwete Awamu ya Nne.

Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano nchini ambao uliyoingia madarakani rasmi Novemba 5, 2015, umepewa dhamana ya kuliongoza taifa hili wakati suala la amani ni la muhimu kwa maendeleo ya Watanzania kwa ujumla wao kwa kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025.

Dira hiyo ya Maendeleo Tanzania ilianza mwaka 1994 na hatimaye serikali ilizindua rasmi dira hiyo, mwaka 1999 nchini kwa lengo la kuhamasisha maendeleo endelevu yenye tija kwa jamii. 

Msingi wa Dira ya 2025 nchini ni kuhimiza Watanzania kuwa ifikapo 2025, Tanzania iwe imepitia katika mabadiliko makubwa ya kiuchumi na maendeleo ili kufikia kipato cha kati, ikiwa na viwango vya juu vya viwanda, ushindani, maisha bora, utawala wa sheria na kuwa na jamii iliyoelimika na inayopenda kusoma waweze kujipatia maendeleo yao wenyewe kwa kutumia mazingira yao. 

Kimsingi, Dira ya maendeleo nchini imeeleza matarajio ya kijamii, kiuchumi na kisiasa nchini ambapo katika robo ya kwanza ya karne ya 21 lengo lake ni Watanzania kufikia hali ya kipato cha kati.

Malengo hayo yanaweza kufikiwa ili kuifanya nchi iweze kuingia katika soko la ushidani kwa kusimamiwa na kuongozwa na amani iliyojengwa katika misingi imara ya utaifa kwa kuzingatia Katiba ya nchi, sheria, kanuni na taratibu ambazo kila mdau wa maendeleo na mpenda amani anapaswa kuzingatia.   

Wakati Umoja wa Mataifa unasisitiza kwa kauli mbiu yake ya amani mwaka 2015, inayosema “Ubia kwa amani utu kwa wote”, kauli mbiu hiyo ni muhimu kwa musatakabali wa taifa hili ndiyo maana wimbo wa kujenga na kudumisha uzalendo wa Tanzania unahamasisha watu kuipenda nchi kwa moyo wote.

“Nchi yangu Tanzania, Jina lako ni tamu sana, Nilalapo nakuota wewe, Niamkapo ni heri mama wee, Ninapokwenda safarini, Kutazama maajabu, Biashara nayo makazi, Sitaweza kusahau mimi, mambo mema ya kwetu kabisa, Watu wengi wanakusifu, Siasa yako na desturi, Ilikuletea uhuru, Hatuwezi kusahau sisi, Mambo mema ya kwetu hakika, Tanzania, Tanzania, Nakupenda kwa moyo wote”.

Wimbo huo wa uzalendo kwa taifa umeudhihirishia umma wa Watanzania, Afrika na ulimwengu kwa ujumla kuwa Watanzania wanaipenda nchi yao kwa kutunza heshima ya taifa na ndiyo maana watu wengi wanaisifu Tanzania kwa siasa na desturi yake imara wakati wa kupata viongozi wapya kwa amani.

Miongoni wa waangalizi wa kimataifa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu 2015 ni shirika lisilo la kiserikali la nchini Afrika ya Kusini la “Afican Policing Oversight Forum” ambalo lilikuwa na waangalizi wawili Sean M. Tait na Eric W. Pelser, nao walitoa maoni yao kwa kusema jukumu lao lilikuwa kuangalia utendaji wa Jeshi la Polisi na namna lilivyofanya kazi wakati wote wa uchaguzi.

Waangalizi hao walisema wameridhishwa na utendaji wa polisi nchini na kusema kuwa kila kituo cha kupigia kura, wapiga kura walipiga kura kwa amani na walikuwa huru katika zoezi la upigaji kura, polisi kwa nafasi yao, walifanya kazi yao bila kuwabughudhi wapiga kura wakizingatia kanuni zao za kazi. 

Naye Balozi wa Norway nchini, Mhe. Hanna-Marie Kaarstad alisema kuwa Tanzania ni nchi ya kuigwa na mataifa mengi duniani jinsi inavyoendesha uchaguzi na kuwapata viongozi wake kwa amani.

“Uchaguzi umefanyika kwa amani, wapiga kura wamefuata mistari bila bughudha yeyote katika maeneo yote, kuanzia kwa wazee, akina mama, wanawake kwa wanaume na vijana, hili ni suala jema la kuigwa” alisema Balozi Hanna.

Hayo ni matunda mema ya Tanzania ambayo hata wimbo wake wa taifa umekuwa sala ya Watanzania kila wanapokuwa katika tukioa la kitaifa au mikusanyiko rasmi ambapo wimbo huo huimbwa ili kuliweka taifa mikononi mwa Mungu kwa kuwaombea baraka viongozi wake, Hekima, Umoja na Amani kwa watu wake wote, wake kwa waume na watoto ili taifa liweze kudumisha Uhuru na Umoja kwa watu wake kwa maslahi ya taifa.

Kila mdau wa amani amekuwa mstari wa mbele katika kuilinda amani nchini, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ni mmoja wa wadau hao wa amani ambapo wao walianzisha kampeni ya kuhamasisha amani kwa kipindi chote cha maandalizi ya uchaguzi na wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi iliyopewa jina la “AMANI YETU FAHARI YETU” na kuongozwa na Mabalozi wake wa amani katika kampeni hiyo ambao ni wasanii Mrisho Mpoto (maarufu kama Mjomba) na Christina Shusho.

Kampeni hiyo ilikuwa na lengo la kuhamasisha Watanzania wabaki na Amani wakati kampeni za Uchaguzi Mkuu, siku ya kupiga kura ambayo ndiyo siku ya uchaguzi wenyewe na baada ya uchaguzi ambapo suala la amani lilihimizwa kwa kuzingatia kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi. 

Kampeni ilihamasisha Watanzania kutambua kwamba utofauti wa itikadi wa vyama ndio ukomavu wa demokrasia nchini hali ambayo Rais wa Awamu ya Tano mara baada ya kuapishwa wakati akiwashukuru Watanzania na wananchi kwa ujumla pamoja na wageni waliofika kwenye sherehe hiyo aliwasihi washindani wake watambue kuwa nchi ni kubwa kuliko vyama, hivyo hakuna sababu ya kuendelea kukuza malumbano ambayo hayawezi kusadia nchi na wananchi.

Wananchi walivumiliana na walifanya siasa za kistaarabu na walitambua kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi, hivyo kipindi chote cha uchaguzi watanzania walibaki imara na kuitunza Amani ya nchi ambayo imeendelea kuwa tunu iliyotukuka ndani na nje ya Tanzania.   

Ni dhahiri madhara yatokanayo na vurugu ambayo siyo tunda la amani kwa jamii yanaweza kuwa na athari mbalimbali ikiwemo ulemavu, vifo, ukimbizi, njaa na maradhi mengine ya kisaikolojia kwa watu wasio na hatia wakiwemo wanawake, wazee na watoto.

Ili kuhakikisha amani inaendelea kuimarika nchini, Kampuni ya Msama Promotions Limited ya Dar es Salaam iliandaa tamasha la amani kuombea Uchaguzi Mkuuu nchini ambapo Mgeni rasmi alikuwa Rais Dkt. Jakaya Kikwete (kwa sasa Mstaafu) kwa nia ya kuendelea kuwakumbusha na kuwahimiza Watanzania umuhimu wa kudumisha amani wakati uchaguzi huo ikizingatiwa kuwa baada ya uchaguzi, Tanzania itabaki na maisha yanapaswa kuendelea.

Ni jukumu la kila mtu kwa nafasi yake kutetea na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa. Amani na utulivu ni jina jipya la maendeleo endelevu ya binadamu maana bila amani hakuna maendeleo. Kila mwananchi apanie kusimamia misingi ya haki na amani, ili waweze kufurahia maisha kwa kujipatia maendeleo.

Rais Dkt. Magufuli aliwashukuru watangulizi wake Marais Wastaafu Julius Kambarage Nyerere, Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Benjamini Mkapa, Dkt. Jakaya Kikwete na wageni mbalimbali waalikwa alisema “Napenda kutumia nafasi hii kutoa shukrani zangu kwa kupata nafasi ya kuwa Rais, lakini nawahakikishia nitafanya kazi kwa nguvu zangu zote na nipotayari kushirikiana na washindani wangu kujenga nchi ambayo ina maendeleo na amani”. 

Serikali ya Awamu ya Tano imeingia madarakani ambapo kielelezo cha amani kinaendelea kujitokeza kila mara ikizingatiwa wakati Dkt. Magufuli alipokuwa na tukio kubwa la kitaifa na mihadhara yake ilipambwa kwa kunyesha mvua.

Kunyesha kwa mvua kila mara kumeonesha uhai ikizingatiwa mvua hizo zilinyesha akiwa nahitimisha kampeni Oktoba 24, 2015 mkoani Mwanza katika wilaya ya Ukerewe ambapo hata Mtangulizi wake Dkt. Jakaya Kikwete alishindwa kwenda kuhutubia visiwa hivyo kwa kuwa mvua kubwa ilinyesha na kuahirisha safari hiyo.

Vivyo hivyo mvua ilinyesha wakati wa kupokea Hati ya Ushindi Oktoba 30, 2015 iliyoandaliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na wakati wa kuapishwa kwa viongozi hao wapya Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Makamu wake Samia Suluhu Hassan Novemba 5 mwaka huu.

Kwa maneno ya wahenga wetu, kuna usemi unaosema kuwa mvua ikinyesha wakati wa tukio muhimu linafanyika kama ilivyokuwa Novemba 5, mwaka huu, mhusika wa tukio hilo “anakichwa kizuri” maana yake ni mtu mwenye bahati nzuri siku zote za maisha yake na dalili yake kubwa ni amani ambayo katika ulimwengu wa leo amani ni tunu muhimu katika kuwaletea maendeleo wananchi. 

Nao viongozi wa dini waliowakilisha dini zao wakati wa sherehe za kuapishwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano wa Jamhuri Muungano wa Tanzania na Makamu wake, viongozi hao waliongoza sala maalum na kuwaombea baraka viongozi wapya walioko madarakani ili waweze kuiongoza nchi katika misingi ya haki na amani.

Viongozi hao walikuwa Askofu Mkuu wa  Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es salaam, Muadhama Polycarp Kardinali Pengo, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Askofu Dkt. Alex Malasusa pamoja na Mufti wa Tanzania Abubakar Zuber ambao waliwaombea viongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano waongoze taifa kwa haki na amani wakimtegemea Mungu katika utendaji wao wa kazi.

Tanzania imeendelea kutoa hamasa kwa nchi za Afrika na dunia nzima, kwa kitendo chake cha kubadilishana madaraka kwa amani, hatua hiyo kubadilishana madaraka imeendelea kuwa ni ya kiungwana na kwa namna ya pekee nchi nyingi zinapaswa kuiga mfano huo mwema wa Tanzania.

Salamu zilizotumwa na viongozi mbalimbali Afrika na duniani kote za kumpongeza Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Makamu wake Samia Hassan Suluhu kwa kushika nyadhifa hizo za juu kitaifa ni ishara kuwa mataifa hayo yanaunga mkono kitendo cha Tanzania cha viongozi wake kuachiana madaraka kwa amani.

Ndiyo maana viongozi wa mataifa jirani waliamua kuja kushudia na kujionea demokrasia ya kweli ilivyoshika mkondo wake ambapo amani inaheshimiwa na kutunzwa Tanzania kwa viongozi wake kuachiana madaraka hadharani na kushudiwa na wanachi ndani na nje ya kupitia njia mbalimbali za mawasiliano ikiwemo simu, radio, mitandao ya kijamii, TV na magazeti.

Baadhi ya viongozi hao ni pamoja na Rais wa Uganda Yoweri Museveni,  Uhuru Kenyatta wa Kenya, Paul Kagame wa Rwanda,  Robert Mugabe wa Zimbabwe,  Jacob Zuma wa Afrika Kusini, Fillipe Nyusi wa Msumbiji, Joseph Kabila wa DRC na Edger Lungu wa Zambia.

Wengine ni kutoka Falme za Kiarabu, Waziri wa Utalii Oman, Mkamu Mwenyekiti wa Chama Tawala cha China Ziang Piang, Mwakilishi kutoka  Saudi Arabia na viongozi wengine waliowakilisha nchi mbalimbali wakiwemo Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini nao walishiriki katika sherehe kuapishwa na kuingia madarakani Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Magufuli kwa awamu ya kwanza ya miaka mitao hadi 2020.

Mwandishi wa makala haya anaungana na maandiko matakatifu ambayo yanakiri, kutambua na kulilipa suala la amani kipaumbele ambapo tunasoma ushuhuda wa Yesu alipowaambia wanafunzi wake “Amani yangu nawapa” Yohana 14:27

Kwa Tanzania, amani ni zawadi yenye thamani inayolinganishwa na hali ambayo kiongozi wa Ukristo (Yesu) aliwaambia wafuasi wake siku ya mwisho alipokuwa pamoja nao ambapo hakuwapa amani tu bali aliwapa amani yake mwenyewe. 

Watanzania ni jukumu letu wote kuweka mkazo katika maisha ya siasa shirikishi, kujenga imani miongoni mwa jamii, amani, uaminifu na kuimarisha taasisi zinazo unga mkono suala la amani na demokrasia nchini ikiwemo taasisi za elimu ya juu na asasi za kiraia.

Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki inaguswa kwa namna ya pekee na suala la amani, ndiyo maana inaungana na nchi washirika kuimba wimbo wa jumuiya hiyo unaotaka tuilinde, tuwajibike, tuimarike na kuishi kwa amani ili kutimiza na malengo tuliyojiwekea kama jumiya yakiongozwa na uzalendo ili kulinda Uhuru, Amani, Mila na desturi zetu.

Amani ni ngao yetu sote, uchaguzi wa mwaka huu umekuwa wa amani, shirikishi na wenye uwazi pamoja na kuimarisha demokrasia ya vyama vingi ambavyo kwa ujumla wao vitaendelea kuhakikisha historia ya kujivunia ya Tanzania ya kiuongozi, kikanda, barani Afrika na duniani inaendelea kukua na kuimarika sanjari na kuboresha maendeleo ya Watanzania kwa ujumla wao kwa kuzingatia kauli mbiu ya Rais Dkt. Magufuli ya “Hapa Kazi Tu” katika kuinua sekta za elimu, maji viwanda, afya, miundo mbini ya barabara, umeme, kilimo, uvuvi, mifugo na biashara.

Hayo yote yanawezekana ikiwa Watanzania tutaendelea kuungana kwa pamoja kwa umoja wetu kuilinda, kuidumisha na kuijenga amani yetu, “Mungu ibariki amani yetu iendelee kutawala, Mungu ibariki Tanzania”.

No comments: