NA BASHIR YAKUB.
NILIWAHI kueleza namna ya kuanzisha kampuni pamoja na usajili wa jina la biashara. Katika makala hayo pia nilieleza tofauti kati ya kusajili kampuni na kusajili jina la biashara.
Hii ilikwenda sambamba na maelezo ya tofauti za kiuchumi ya vyote viwili. Ifahamike kuwa hizi zote ni njia za kisasa za kujitafutia kipato. Makala ya leo yanaeleza namna ya kisheria ya kuanzisha SACCOS.
Tutaona utaratibu mzima ambao unaweza kupitia katika kulifanikisha hili. Muhimu ni kujua kuwa SACCOS nayo ni njia kati ya njia za kisasa za kujipatia na kujiongezea kipato. Aidha utaratibu mzima wa kuanzisha na kuendesha SACCOS unaongozwa na Sheria namba 6 ya 2013 ya vyama vya ushirika ambayo ndiyo msingi wa makala haya.
1.SACCOS NI NINI ?
SACCOS ni kifupi cha neno la kiingereza lijukanalo kama Saving And Credit CO-operative Society. Kwa Kiswahili kizuri ni chama cha ushirika cha akiba na mikopo.
Kwa faida tu ni kuwa, kwa mara ya kwanza SACCOS zilianzishwa Ujerumani na mtu aitwaye Fredrick Taylor. Sura ya SACCOS aliyoanzisha Taylor imekuwa ikibadilika kadri shughuli za kijamii na kiuchumi zinavyokua mpaka kufikia aina ya SACCOS zilizopo sasa.
2. SACCOS KIUCHUMI.
Saccos ni asasi ya kifedha. Ni muungano wa watu ambao lengo lao ni kukusanya fedha na kukopeshana au kufanya biashara moja kwa moja na kugawana faida. Taratibu za kukopeshana na kufanya biashara katika Saccos hufanywa na watu wenye msimamo au fungamano linalofanana.
Hii ina maana wanaweza kuwa watu wanaofanya kazi ya aina moja kwa mfano walimu, wafanyabiashara, wafanyakazi katika ofisi fulani, vijana wanaoishi eneo moja mtaani, wanawake walio katika eneo moja, waumini wanaosali katika msikiti au kanisa moja, wakulima,wavuvi, wafugaji, wanakijiji na watu wote wa aina hiyo. Watu walio katika mafungamano ya aina hiyo ndio wanaweza kuunda Saccos.
3. LENGO KUU LA SACCOS.
Lengo kuu la Saccos ni kuwa, ni ushirika ambao lengo lake ni kuondoa umasikini na kuinua uchumi wa wanachama na jamii kwa ujumla. Hii ndio sababu kubwa ya kuanzisha Saccos. Ni kukuza kipato kwa manufaa ya kiuchumi .Ni biashara ya kuongeza kipato kama zilivyo biashara nyingine za uanzishaji wa makampuni n.k.
4. MAMBO YA KUZINGATIA KABLA YA KUANZISHA SACCOS.
Kwanza kabisa ni uwepo wa hiari ya kila mwanachama. Ni kosa kumshurutisha mtu kuingia katika Saccos. Ni lazima kila anayeingia afanye hivyo kwa hiari yake. Pili ni muhimu wanaoanzisha Saccos wakawa na matatizo ya aina moja. Kama tatizo ni ajira na Saccos inaundwa ili kukabiliana na hilo basi yapasa hilo ndio liwe tatizo la wanachama wote n.k. Kwa ufupi wanachama wawe ni watu wanaoshiriki (share) tatizo.
5. TARATIBU RASMI ZA KUANZISHA SACCOS.
( a ) Kwanza kabisa hakikisha hampungui watu watano. Yaani muwe watu watano na kuendelea. Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 38(1) cha sheria ya vyama vya ushirika. Hata hivyo idadi hii ni kwa waanzishaji wa awali. Hii ni kwakuwa idadi hasa inayotakiwa ni kuanzia watu ishirini. Msajili wa vyama vya ushirika atawapa maelekezo ya idadi kwa namna anavyoona kikundi chenu.
( b ) Baada ya idadi hiyo kutimia mtamfuata msajili wa vyama vya ushirika ambaye hupatikana katika kila makao makuu ya wilaya mliyopo. Nenda makao makuu ya wilaya na uliza hapo utampata. Baada ya kusikiliza maelezo yenu msajili ataandaa mkutao ambao huitwa mkutano mkuu wa uanzishaji ambao msajili mwenyewe ndio atakuwa mwenyekiti wake. Katika mkutano huo itateuliwa kamati ya muda ya uanzishaji ambayo itakuwa na wajumbe 5 – 9 akiwemo katibu, mwekahazina, mwenyekiti na wajumbe wengine.
( c ) Baada ya kamati ya uanzishaji kuundwa itakuwa na kazi ya kushirikiana na afisa ushirika kuandaa katiba za chama, sera,miongozo, miradi ya kiuchumi, taratibu za viingilio na taratibu zote za uanzishaji na uendeshaji.
( d ) Baada ya kazi hiyo kukamilika basi maombi rasmi ya kuomba kusajiliwa yatawasilishwa kwa huyo afisa ushirika wa wilaya yakiambatana na nakala nne za sera za chama, kidadisi uchumi, makadirio ya mapato na matumizi, mikhutasari ya mikutano miwili, na ada kama itakavyoelekezwa na afisa ushirika.
Tutaeleza katika makala nyingine umuhimu wa SACCOS, tofauti za kiuchumi kati ya SACCOS na kampuni na kipi bora kati ya kuanzisha SACCOS na kampuni.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241 bashiryakub@ymail.com
No comments:
Post a Comment