Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
VIJANA wametakiwa kutokubali kutumiwa vibaya na baadhi ya wanasiasa kwa maslahi ya watu wachache huku hao wanaowatumia wanasonga mbele kimaendeleo na wao wanazidi kurudi nyuma.
Rai hiyo imetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea kwa nyakati tofauti na wananchi wa kijiji cha Kikomolela kilichopo jimbo la Mchinga na mtaa wa Likotwa uliopo Jimbo la Lindi mjini waliohudhuria kampeni ya kuwanadi wagombea wa nafasi za udiwani, ubunge na urais kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mama Kikwete ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kupitia wilaya ya Lindi mjini alisema kuna baadhi ya wanasiasa wanawatumia vijana kufanya vurugu ambazo hazina faida katika jamii zaidi ya kuleta hasara kwani wanaharibu miundombinu ikiwa ni pamoja na barabara, majengo na hivyo kurudisha maendeleo nyuma.
Kuhusu uchaguzi aliwaomba wananchi wote wa maeneo hayo wakiwemo wanachama wa vyama vya upinzani kuwachagua wagombea wa CCM ambao watazidi kuwaletea maendeleo kwani Serikali ya CCM imefanya mambo mengi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za afya, elimu, maji na barabara.
“Siku ya uchaguzi ikifika chukua kadi yako ya kupigia kura wahi mapema kituoni kachague viongozi bora utakaoona watakuletea maendeleo na viongozi hawa wanapatikana ndani ya CCM. Msiogope! siku hiyo kutakuwa na usalama wa kutosha”, MNEC huyo alisisitiza.
Kwa upande wake mgombea ubunge wa jimbo la Mchinga Saidi Mtanda alisema Serikali ya CCM imefanya mambo mengi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma ya umeme na katika eneo hilo vijiji 40 kati ya 47 vikiwemo vijiji vya Nangaru na Kitomanga karibu vitawasha umeme kwa gharama ya shilingi 45,000/=.
Mtanda alisema, “Nawaomba wenzetu kutoka vyama vya upinzani dumisheni hali ya Amani na utulivu iliyopo kwani kuna baadhi yenu mnatoa kauli za kuwatisha wanachama wa CCM kitendo ambacho siyo kizuri”,.
Naye mgombea Ubunge wa Jimbo la Lindi mjini Kaunje Selemani aliwaomba wananchi waliohudhuria mkutano huo kumpigia kura ya ndiyo na kuwaahidi kusimamia Ilani ya uchaguzi ya CCM ambayo itawaletea maendeleo katika sekta mbalimbali zikiwemo za nishati na madini, kilimo, elimu, afya, maji, umeme na barabara.
Katika mikutano hiyo jumla ya wanachama watatu walihama kutoka chama cha Wananchi (CUF) na kujiunga na CCM.
Wakati huo huo akiwa njiani kuelekea kijiji cha Kikomolela msafara wa Mama Kikwete ulisimama Shule ya Msingi Moka ambapo walimu na wanafunzi walikuwa wamesimama pembeni ya barabara wakiwa wameshika bango lililoandikwa SHULE YA MSINGI MOKA TUNAUJUMBE KWA MAMA KIKWETE.
Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo Abdala Mkanjima alimuomba Mama Kikwete ambaye kitaaluma ni Mwalimu awasaidie kufanya wire ring katika shule yao kwani umeme umepita shuleni hapo.
Mama Kikwete aliahidi kulishughulikia suala la umeme katika shule hiyo. Pia aliwaasa wanafunzi wasome kwa bidii ili waweze kujikomboa kimaisha na kuwa viongozi wazuri hapo baadaye ambao watalisaidia taifa lao na jamii inayowazunguka.
No comments:
Post a Comment