Friday, October 23, 2015

TAMKO LA TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA


TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Kitalu Na. 8, Mtaa wa Luthuli
S.L.P 2643, DAR ES SALAAM
Simu: +255 22 2135747/8; 2137125; 2135222
Faksi: +255 22 2111281
Barua Pepe: chragg@chragg.go.tz
Tovuti: www.chragg.go.tz

Oktoba 23, 2015

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI              
Tamko la Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria kwa ajili ya Uchaguzi Huru, wa Haki na Amani

TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB)  imekuwa ikifuatilia kwa karibu matamshi mbalimbali ya wanasiasa, viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa Serikali, Tume ya Uchaguzi, na Jeshi la Polisi kuhusu nini kifanyike baada ya kupiga kura siku ya uchaguzi mkuu, Oktoba 25, 2015. Matamshi haya yamesababisha mkanganyiko na malumbano miongoni mwa viongozi na wananchi pia.

THBUB inapenda kusema kwamba, licha ya changamoto kadhaa zilizojitokeza katika baadhi ya maeneo, wakati wa kampeni za uchaguzi, kwa ujumla kampeni za uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani zimefanyika nchi nzima kwa amani na utulivu. Ni wajibu wetu sote kudumisha amani katika nchi yetu muda wote, wakati wa uchaguzi na baada ya kutangaza matokeo ya uchaguzi mkuu.

Tume (THBUB) inawashukuru na kuwapongeza wananchi kwa jinsi walivyoonyesha utulivu wakati wa mikutano mikubwa ya kampeni, ambayo imekuwa ikivuta maelfu ya wananchi.

Tume (THBUB) inatoa pongezi kwa Jeshi la Polisi kwa ulinzi ambao umekuwepo katika mikutano hiyo. Aidha, inavipongeza vyombo vya habari kwa kazi nzuri ya kuwapasha wananchi habari mbalimbali za uchaguzi.

Tume (THBUB) inatambua na kupongeza jitihada zinazofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, na Tume ya Uchaguzi Zanzibar kwa maandalizi ya uchaguzi.

Tume (THBUB) inapenda kutahadharisha kwamba malumbano haya ambayo yanaendelea hayaonyeshi dalili nzuri, pamoja na jitihada za wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini kuhubiri umuhimu wa uchaguzi wa amani. Malumbano haya yasipotafutiwa ufumbuzi wa haraka, kwa kutumia busara na kuzingatia sheria, haki za binadamu, na misingi ya utawala bora, kuna dalili kubwa ya kuwepo vurugu, uvunjifu wa sheria na amani, kwani pande zote hizi zimeendeleza malumbano na kushikilia misimamo yao.

Tume (THBUB) inaonya kwamba vurugu zinaweza kutokea, ama kwa makusudi, au kwa bahati mbaya, iwapo wananchi na wafuasi wa vyama vya siasa watashikilia misimamo yao, ama watagoma na kukaidi amri ya Polisi. Lolote katika hayo likitokea, kuna uwezekano mkubwa wa kuvurugika kwa uchaguzi, na haki za binadamu zitaathirika.

Vile vile, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imesikitishwa na matamshi yanayoashiria kutoiamini Tume ya Uchaguzi, na hata tuhuma za uwezekano wa wizi wa kura. Pia kumekuwa na matamshi ya kuwataka wananchi walinde kura, jambo ambalo halina msingi wowote wa sheria.

Ni vyema ifahamike kuwa, wajibu wa ulinzi wa kura upo kisheria, na ni wajibu ambao wamepewa mawakala wa vyama vya siasa na wagombea, ama wagombea wenyewe, wanaoruhusiwa kuwa ndani ya vituo, wakisaidiana na wasimamizi wa Tume ya Uchaguzi na Jeshi la Polisi kuhakikisha kwamba taratibu zote zinazosimamia upigaji kura zimefuatwa.

Kwa mujibu wa Vifungu vya 48(2) na 49 vya Kanuni za Uchaguzi (Urais na Ubunge) za mwaka 2010, Tanzania Bara, vyama vya siasa vinavyoshiriki katika uchaguzi vinatakiwa kuteua mawakala wao wa uchaguzi kwa kila kituo, jambo ambalo Tume (THBUB) inaamini limefanyika. Mawakala wanatakiwa kula kiapo cha uaminifu.

Vifungu vya 59 na 60 vya Kanuni za Uchaguzi vinaeleza jinsi wakala wa chama au mgombea, atakavyoshiriki katika taratibu za kuhesabu kura, na jinsi malalamiko yatakavyo shughulikiwa na Msimamizi wa Uchaguzi.

Vifungu vya 61 hadi 66 vya kanuni hizo vinaeleza utaratibu wa kujumlisha kura za wagombea, na kutangazwa matokeo. Kanuni zinazungumzia pia uhusika wa mawakala katika hatua zote. Mawakala watapewa nakala za fomu mbalimbali husika, zikiwemo zenye malalamiko yaliyowasilishwa, na matokeo. Utaratibu huu wa sheria ndiyo unaotoa ulinzi mahususi wa kura.

Tume (THBUB) inawataka mawakala wafanye kazi zao kwa uadilifu na weledi. Mawakala wasiende kwenye vituo wakiwa na nia potofu (bad faith/malafide) ya kuharibu zoezi la kupiga kura. Tume (THBUB) inalisema hili kwa kuwa imebaini kuwepo matamshi yanayoonyesha hisia za kutoiamini Tume ya Uchaguzi. Tume (THBUB) inasisitiza umuhimu wa kuiamini na kuipa ushirikiano Tume ya Uchaguzi ili itekeleze majukumu yake bila ya kuingiliwa ama kubezwa.

Kwa hiyo Tume (THBUB) inapenda kutamka kwamba mlinzi mkuu wa kura ni wakala wa chama cha siasa, mgombea, na siyo mpiga kura au mwananchi wa kawaida ambaye hajapewa majukumu hayo kwa mujibu wa sheria.

Tume (THBUB) inatahadharisha kuwa ni vyema kila mdau wa uchaguzi atimize majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kanuni za uchaguzi. Jeshi la Polisi liendelee kutumia weledi katika kutoa ulinzi siku ya uchaguzi, kama lilivyofanya wakati wa kampeni za uchaguzi ambapo tulishuhudia mikutano mikubwa ikimalizika kwa usalama.

Kwa maana hiyo wananchi wanawajibu mkubwa wa kuwa watulivu  wakati wa zoezi zima la uchaguzi kuanzia kupiga kura na kusubiri matokeo kwa amani.

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inaamini kuwa utawala wa sheria lazima uheshimiwe na kila mtu, vikiwemo vyombo vya dola na mamlaka za Serikali.

Hivyo basi Tume (THBUB) inatamka:
1.    Viongozi wa vyama vya siasa na wagombea waepuke lugha zinazoweza kusababisha hofu, vurugu na uvunjifu wa amani.

2.    Inazishauri  Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Tume ya Uchaguzi Zanzibar, na Jeshi la Polisi kuzingatia sheria na kudumisha misingi ya utawala bora, mambo ambayo ndiyo msingi wa kulinda haki za binadamu.

3.    Aidha, THBUB inawataka wananchi kupiga kura kwa amani na kuheshimu sheria zinazoongoza zoezi zima la uchaguzi.

4.    Vyama vya siasa vihakikishe kuwa Mawakala wao wanafanya kazi zao kwa uadilifu na wahakikishe kuwa wanatambua wajibu wao na wanazingatia taratibu za uchaguzi.

5.    Jeshi la Polisi litoe ulinzi mahsusi, bila vitisho, ili kuhakikisha kwamba zoezi la kupiga kura linafanyika kwa amani na kwa kuzingatia haki za binadamu na misingi ya utawala bora.

6.    Viongozi wa vyama vya siasa na wafuasi wao wawe wavumilivu na wajiepushe na matamshi au matendo yanayo weza kusababisha uvunjifu wa sheria, haki za binadamu, misingi ya utawala bora na kusababisha vurugu na kutoweka kwa amani.

7.    Tume ya Uchaguzi na Wasimamizi wa uchaguzi, na mawakala wa vyama wahakikishe kuwa zoezi zima la kupiga kura, kuhesabu kura, kubandika na kutangaza matokeo linafanyika kama sheria inavyotamka.

Tume ya Haki za Binadamu itaendelea kufanya ufuatiliaji wa mchakato wa uchaguzi nchini kote ili kuimarisha ulinzi wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora.

Tume inawataka wananchi watakaobaini uvunjifu wowote wa haki za binadamu, au uvunjifu wa sheria ya uchaguzi, kuzijulisha mamlaka husika zinazosimamia zoezi la uchaguzi.
Aidha, wanaweza kutoa taarifa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kupitia ujumbe mfupi wa simu ya kiganjani (SMS) kwenda Na. 0754 460 259.

Ujumbe lazima uanze na neno 'TAARIFA' au ' RIPOTI' kisha andika taarifa yenyewe. Namba hii inapokea ujumbe mfupi tu. Kwa taarifa zaidi piga Na. +255 22 2135747-8.
  
Kauli mbiu ya THBUB katika kuelekea Uchaguzi Mkuu ni “Watanzania wote tufanye Uchaguzi Mkuu kwa utulivu ili uwe Huru, wa Haki, na Amani.”

Imetolewa na:

(SIGNED) 
Bahame Tom Nyanduga
                                                   Mwenyekiti

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA 

Oktoba 23, 2015

No comments: