Monday, October 12, 2015

MKAPA AMPONGEZA RAIS KIKWETE, NSSF UJENZI DARAJA LA KIGAMBONI

 RAIS Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa( katikati) akiwa ameongozana na Waziri wa Kazi na Ajira, Bi. Gaudensia Kabaka (wa kwanza kulia),  Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dk. Ramadhan Dau,  Meneja Miradi wa Shirika hilo Muhandisi John Msemo (watatu kushoto) alipotembelea mradi wa ujenzi wa Daraja la Kigamboni kwa mualiko maalum kutoka NSSF mwishoni mwa wiki. Wengine ni maafisa wa serikali na NSSF.
 RAIS Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa( katikati) akipokea maelezo kuhusu mradi wa ujenzi wa Daraja la Kigamboni kutoka kwa Meneja Miradi wa shirika hilo Muhandisi John Msemo (kulia kwake) alipotembelea ujenzi huo kwa mualiko maalum kutoka NSSF.





 Muonekano wa Daraja kwa sasa.


RAIS Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Waziri wa Kazi na Ajira, Bi. Gaudensia Kabaka (wan ne kulia) pamoja viongozi na maofisa wa Shirika la NSSF wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la hilo, Dk. Ramadhan Dau (kulia kwake) alipotembelea moja ya miradi ya nyumba za makazi  zinazojengwa na shirika hilo eneo la kigamboni.

Na Mwandishi wetu
Dar es Salaam, 11th, Oct, 2015: RAIS Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa amempongeza rais anayemaliza muda wake Jakaya Kikwete pamoja na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF)kwa kusimamia utekelezaji wa ujenzi wa daraja la Kigamboni linalotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.

Mradi wa daraja hilo lenye urefu wa mita 680, unaogharimiwa kwa pamoja kati ya mfuko wa NSSF na serikali kwa gharama ya Dola za Kimarekani Milioni 143.5 (Sh. Bilioni 248), ulipangwa kumalizika ndani ya miezi 36 tangu kuzinduliwa kwake mwezi Septemba mwaka 2012.

Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya kina kuhusiana na mradi huo jana jijini Dar es salaam alipotembelea daraja hilo kwa mwaliko maalum kutoka NSSF, Mh. Mkapa alisema uamuzi wa kutekeleza mradi huo ni wa kijasiri kwa kuwa unahusisha kiasi kikubwa cha rasilimali fedha na muda.

“Pia kitendo cha Rais Kikwete kutoogopa kutumia nguvu za nje ya serikali yake ili kufikia malengo ya kimaendeleo ndio chachu ya mafanikio kama haya…ningependa sana kuona daraja hili likizinduliwa na Rais Kikwete mwenyewe,’’ alisema Mh. Mkapa.

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Meneja Miradi wa NSSF Muhandisi. John Msemo alisema kwa sasa ujenzi wa daraja hilo umekamilika kwa asilimia 94 huku akibainisha kuwa zimebaki mita 25 ili kuunganisha kabisa daraja hilo.

“Awali mradi ulipangwa ukamilike Januari mwaka huu lakini kutokana na changamoto zilizojitokeza, ujenzi utakamilika mwishoni mwa mwaka huu na daraja litaanza kutumika mapema mwezi wa kwanza hapo mwakani,’’ alisema.

Kwa mujibu wa Muhandisi Msemo, wakati wa kusimika nguzo zinazoshikilia daraja hilo, ilibainika kuwa umbali wa mita 56 kutoka sakafu ya bahari kulikuwa na uwazi ambao ungeathiri daraja hilo.

“Wataalamu ilibidi kusimama kwa muda kwa ajili ya kuziba uwazi huo, hivyo imesababisha kalenda ya mradi kubadilika ili tuweze kufanya kazi yenye ubora,” alisema huku akizitaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na kesi za fidia kwa wakazi waliokuwa wanaishi eneo la mradi, majaribio ya migomo ya wafanyakazi pamoja na malighafi za ujenzi kupatikana mbali na eneo la ujenzi.


Hata hivyo alisema kukamilika kwa mradi huo kutazaa changamoto kadhaa ambazo zinatakiwa kufanyiwa kazi na serikali mapema zikiwemo suala la msongamano wa magari kwenye makutano ya barabara za Kilwa –Mandela, Nyerere-Mandela, Veta Chang’ombe-Kawawa pamoja na uduni wa barabara unganishi zikiwemo zile za Vijibweni-Mji Mwema pamoja na Gerezani- Ohio.

“Lakini pia faida kubwa zaidi ambayo kama taifa tumeipata kwenye mradi huu ni pamoja na suala la uzoefu wa kusimamia na kuendesha miradi ya namna hii ambapo wataalamu wetu wengi wa ndani wameelimika kiasi cha kutosha kuweza kusimamia miradi ya namna hii…Kifupi kama taifa tunao wataalamu wa kusimamia ujenzi wa daraja la Dar es Salaam –Zanzibar muda ukifika,’’ alibainisha.

Kwa upande wake Waziri wa Kazi na Ajira, Bi. Gaudensia Kabaka  alitoa wito kwa wahandisi wa mradi huo kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo huku pia wakiangalia namna itakayomuwezesha Rais Jakaya Kikwete kufanya uzinduzi wa daraja hilo (Soft Opening) kabla hajamaliza muda wake.

Kwa upande wake pia, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa NSSF, Dk. Ramadhan Dau mbali na kumshukuru Mh Mkapa kwa kuasisi Mradi huo mwaka 2002 alisema daraja hilo likikamilika litaweza kuinua uchumi wa eneo la Kigamboni na kuwa sehemu nzuri ya uwekezaji, hivyo aliwataka wananchi kulitumia kikamilifu kwa ajili ya maendeleo yao.

Mbali na daraja hilo Mh Mkapa pia alipata wasaa wa kutembelea miradi mingine inayotekelezwa na mfuko huo ikiwemo ile ya ujenzi wa nyumba za makazi eneo la Kijichi na ule wa ‘Dege Eco village’ yote ikiwa eneo la Kigamboni.

No comments: