Friday, October 23, 2015

MAKAMU WA RAIS WA ZANZIBAR AKAGUA KARO LA KUHIFADHI UCHAFU

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akifanya ziara ya kukagua maandalizi ya kazi za usafishaji wa karo zinazohudumia uhifadhi ya Uchafu katika Nyumba za Maendeleo zilizopo Mtaa wa Mtemani Mjini Wete Kisiwani Pemba. Kushoto ya Balozi Seif ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mh. Mar Khamis Othman. 
 Mkurugenzi wa Baraza la Mji wa Wete Kisiwani Pemba Ndugu Mgeni Othman Juma akitoa maelezo mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif juu ya hatua zilizochukuliwa katika kufanya usafi wa karo za Nyumba za Maendeleo Mtemani  Mjini Wete.
 Balozi Seif akiushauri Uongozi  wa Wizara ya Ardhi na Makaazi kuandaa utaratibu za kuzifanyia ukaguzi Nyumba za Maendeleo ili kukabiliana na changamoto zinazozikabili Nyumba hizo ikiwemo matengenezo ya kila mara.
Picha na – OMPR – ZNZ.

UONGOZI wa Wizara na Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Kisiwani Pemba kwa kushirikiana na Baraza la Mji wa Wete umeanza matayarisho ya kujiandaa na kazi ya usafishaji wa karo zilizotengwa kuhifadhi uchafu unaotoka katika  Nyumba za Maendeleo zilizopo Mtaa wa Mtemani Mjini Wete Kisiwani Pemba.

Kazi hiyo imeanza kwa hatua ya awali ya uchimbaji  wa mashimo yatakayotumika kufukia mabaki ya uchafu utakaosafishwa kutoka kwenye Karo  Saba  zinazohudumia Nyumba hizo zilizojengwa katika miaka ya sabini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa Kisiwani Pemba alipata fursa ya kukagua hatua iliyofikiwa ya  kazi hiyo itakayosaidia kuimarisha hali ya usafi pamoja na utunzaji wa  mazingira katika Mtaa huo.

Mkurugenzi wa Baraza la Mji wa Wete Pemba Ndugu Mgeni Othman Juma alimueleza Balozi Seif kwamba Wananchi wa Nyumba za Maendeleo Mtemani Wete wamewahi kujaribu kufanya usafi katika  eneo hilo bila ya kupata mafanikio yoyote.

Ndugu Mgeni alisema changamoto zilizowakumba wakaazi hao na kushindwa kukamilisha  kazi waliyoamua kuitekeleza zilitokana na ukosefu wa vifaa vya kufanyia kazi ambavyo vinahitaji gharama kubwa.

Naye Afisa Ujenzi Mkoa wa Kaskazini Pemba Ndugu Badru Hamad Hassan alisema kwamba kazi hiyo ingekuwa imeshamalizika kama uwezo wa kifedha ungeruhusu kuwalipa Vijana walio tayari kutekeleza jukumu hilo.

Nd. Badru alisema kazi yote inayohitaji usafishaji wa kina kwenye mashimo ya karo hizo Saba inahitaji jumla ya shilingi Laki saba ambazo kwa hivi sasa tayari Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Pemba imeshatoa ahadi ya  kuzitafuta ili kazi hiyo ianze na kumalizika mapema kabla ya kuanza  kwa mvua za Vuli.

Akitoa nasaha zake Makamu wa Pili  wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba  Nyumba za Maendeleo zilizojengwa katika maeneo mbali mbali ya Visiwa vya Unguja na Pemba  zililenga kuwapatia makaazi Bora wananchi wa Visiwa hivi.

Balozi Seif alisema wazo la Taasisi hizo mbili za Umma la kufanya usafi ni zuri kwa vile mbali ya kulinda Afya za Wananchi hasa Watoto  wadogo lakini pia  litasaidia kuimarisha mazingira mazuri katika eneo hilo la Mji.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwashauri watendaji wanaosimamia nyumba hizo kujitahidi kuweka utaratibu maalum utakaowapa muda maalum wa kufanya ukaguzi wa nyumba hizo ili kujua athari na baadaye kuitafutia ufumbuzi katika kipindi muwafaka.

Ujenzi wa Nyumba za Maendeleo  katika Wilaya zote za Visiwa vya Unguja na Pemba uliosimamiwa na Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ulifanywa ili kuwajengea mazingira bora ya Makaazi Wakwezi na Wakulima mara tu baada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.

No comments: