Thursday, October 22, 2015

MAKAMU WA RAIS DKT. AGANA NA WATUMISHI WA OFISI YAKE DAR

 Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, Saz Salula, akizungumza kutoa shukurani wakati wa hafla fupi iliyoandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa ajili ya Mhe. Makamu wa Rais kuagana na Watumishi wa Ofisi yake. Hafla hiyo ilifanyika juzi Okt 20, 2015 kwenye Makazi ya Dkt. Bilal
  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akipokea zawadi kutoka kwa Katibu Mkuu wa Ofisi yake, Saz Salula, wakati wa hafla fupi ya kuagana na watumishi wa ofisi yake, iliyofanyika Oysterbay jijini Dar es Salaam, juzi Okt 20, 2015.

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Watumishi wa Ofisi yake (baadhi hawapo pichani) wakati wa hafla fupi ya kumuaga iliyofanyika Oysterbay jijini Dar es Salaam, juzi Okt 20, 2015.
 Baadhi ya Watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais, wakimsikiliza Dkt.Bilal, wakati alipokuwa akizungumza kwenye Hafla hiyo.



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib BIlal, akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa Ofisi yake baada ya hafla hiyo.
 Picha na OMR

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal amewashukuru watumishi wa ofisi yake kwa ushirikiano waliompa katika kipindi chote cha miaka mitano kiasi cha kuweza kutekeleza majukumu ya msingi ya ofisi hiyo ya kudumisha Muungano na uhifadhi wa mazingira kwa ufanisi mkubwa.

Akizungumuza katika hafla fupi ya kumuaga iliyofanyika jana jijini Dar es salaam Dkt. Bilal alisema kuwa, anayo furaha kufikia kipindi hiki na kwamba alifanya majukumu yake vema kutokana na kuwa na wasaidizi mahiri na waliojitoa kufanya kazi zao kwa weledi na uvumilivu mkubwa muda wote.

“Natumia nafasi hii kuwashukuru Watanzania wote. Walinisaidia sana katika kipindi nikifanya kazi ya kuitumikia nchi yangu. Niwashukuru ninyi wafanyakazi wa ofisi yangu, mlifanya kazi kwa kujituma sana na majukumu yetu kwa mujibu wa taratibu tuliyatekeleza kwa ufanisi,” alisema 

Mheshimiwa Makamu wa Rais na kuongeza:
“Nakutakieni kila la kheri katika utendaji wenu. Jitahidini kufanya kama mlivyofanya kwangu kwa yule atakayekuja baada yangu. Nakushukuruni kwa zawadi hasa ya vitabu maana mimi ni muumini wa kusoma, nitavisoma”.

Dkt. Bilal aliwaambia watumishi hao kuwa ushirikiano waliompa katika utendaji wa kazi umewezesha  kuzipatia ufumbuzi hoja mbali mbali za muungano na kusema hoja zilizobaki zinafanyiwa kazi na zitapatiwa ufumbuzi katika serikali ijayo.

Hoja ambazo zipo katika hatua mbalimbali za kutafutiwa ufumbuzi ni pamoja na Hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na Mgawanyo wa Mapato yatokanayo na Faida ya Benki Kuu; Usajili wa vyombo vya moto, Uchimbaji na Utafutaji wa Mafuta na Gesi Asili na Mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya fedha.

Kwa upande wa mazingira alisema katika kipindi chake Tanzania ilipata nafasi ya kuwa Mwenyekiti wa Masuala ya Mazingira kwa viongozi wa Bara la Afrika jambo ambalo limewezesha nchi kutoa mchango mkubwa katika suala zima la uhifadhi na usimamizi wa mazingira katika Bara la Afrika.

Hata hivyo, Dkt. Bilal alionyesha wasiwasi wake katika eneo la usafi wa mazingira na kuwataka watumishi wa ofisi hiyo kushirikiana na taasisi nyingine katika kuhakikisha usafi wa mazingira unapewa kipaumbele katika maeneo yote nchini.

Mapema, akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Sazi Salula alimshukuru Makamu wa Rais kwa uongozi wake ambao umekuwa mwongozo kwa watumishi katika utendaji wao wa kazi na kumtakia kila la heri katika kipindi cha kustaafu kwake.

Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es salaam.

No comments: