NA BASHIR YAKUB -
Unaposhindwa kesi sio mwisho wa kusaka haki. Hii ni kwasababu kushindwa kesi kunatokana na sababu nyingi . Si kweli kuwa kwakuwa umeshindwa kesi katika mahakama fulani basi maana yake ni kuwa ulikuwa huna haki. Yawezekana kabisa haki ilikuwa yako isipokuwa umeshindwa tu kutokana na sababu nyingine za kiutaratibu na kimbinu (procedures & technicalities). Pia waweza kuwa umeshindwa kutokana na uwezo mdogo wa kujieleza na kushindwa kugusa nukta muhimu ambazo kimsingi ndizo zilizokuwa zinabeba shauri lako.
Lakini pia waweza kuwa umeshindwa kwasababu ya hila na mbinu chafu. Na hii wakati mwingine huwahusisha hata waamuzi yaani mahakimu na majaji. Basi ifahamike kuwa ni sababu hizi zilizopelekea kuwepo utaratibu wa rufaa ili yule anayehisi kutotendewa haki aende mbele ili kuona kama anaweza kupata haki yake huko.
1.RUFAA NININI.
Rufaa ni hatua ya kisheria ya kupeleka malalamiko katika hatua ya mahakama ya juu zaidi baada ya mmoja wa wahusika katika kesi iliyoisha kutoridhishwa na hukumu/maamuzi. Ili ukate rufaa ni lazime uwe ulikuwa mhusika katika kesi iliyoisha na uwe na sababu za kwanini unadhani hukuridhishwa na maamuzi. Sababu yoyote ya msingi inakubalika.
2. NI HAKI YAKO KUAMUA KUKATA RUFAA AU KUACHA.
Suala la kukata rufaa halitegemei hisani ya mahakama. Sio upendeleo ambao mtu anapewa ili kuendelea kusaka haki. Ni haki ya msingi na ya kisheria ambayo hutumiwa na yule ambaye anahisi kutotendewa sawa katika shauri la awali lililoisha. Pia ieleweke kuwa rufaa tunazoongelea hapa ni zile rufaa katika mashauri ya madai. Rufaa katika mashauri ya madai tunaongelea mashauri ya ardhi, ndoa, mikataba, migogoro ya biashara na mauziano kwa ujumla, migogoro ya madeni na yale yote ambayo sio jinai. Kwahiyo katika malalamiko ya namna hiyo ni uamuzi wako ukate rufaa kwenda mbele au uache hata kama umeshindwa. Hii ni haki yako na katu haiondolewi na yoyote.
3. HATA ALIYESHINDA ANAWEZA KUKATA RUFAA.
Hapo juu tumesema rufaa ni kwa mtu ambaye hakuridhishwa na maamuzi ya mahakama. Sio kwa ajili ya aliyeshindwa bali ni kwa ajili ya yule ambaye hakuridhishwa. Hii ina Maana kuwa unaweza ukashinda lakini ukawa hukuridhishwa. Na kama umeshinda lakini hukuridhishwa pia waweza kukata rufaa. Kwa mfano ulifungua kesi ukiomba fidia ya milioni 50. Hukumu ikatoka kuwa umeshinda lakini ikasema kuwa utalipwa milioni kumi tu. Kwa mazingira kama haya ni kuwa umeshinda lakini waweza kukata rufaa kudai zaidi. Utakata rufaa kwakuwa umeshinda lakini hukuridhishwa na ushindi. Kinachotakiwa kueleweka hapa ni kuwa rufaa inaweza kukatwa hata yule aliyeshinda kesi na si tu kwa aliyeshindwa.
4. NAMNA YA KUKATA RUFAA.
Mara tu kesi inapoisha hakikisha unafuatilia na kupata nakala ya hukumu pamoja na tuzo( decree). Fuatilia kwa karani wa hakimu/jaji aliyesikiliza shauri lako na umwambie nia yako ya kutaka nakala ya hukumu na tuzo kwa ajili ya kukata rufaa. Huwezi kukata rufaa bila nakala ya hukumu kwakuwa ni lazima uipitie kwa umakini na kuona ni wapi palikuwa na tatizo ili iwe ndio sababu yako ya rufaa.
Ikiwa hukumu ilitolewa na mahakama ya mwanzo basi rufaa itaenda mahakama ya wilaya, na ikiwa ilitolewa na mahakama ya wilaya rufaa itaenda mahakama kuu na ikiwa ilitolewa mahakama kuu basi rufaa huenda mahakama ya rufaa ambayo ni mahakama ya mwisho kiitifaki. Pia rufaa zinazotoka katika mahakama za hakimu mkazi kama ile ya kisutu ambazo baadhi huziita mahakama za mkoa, rufaa zake huenda mahakama kuu pia.
Unapokuwa unaandaa sababu za rufaa hakikisha unamuona mwanasheria kwa ajili ya kupitia hukumu na kukusaidia kuandaa sababu za rufaa. Hii ni kwasababu ipo namna ya kisheria ya kuandaa sababu hizi kwani haziandaliwi kama barua.
Muda ni suala la msingi sana katika kukata rufaa. Hakikisha pale tu hukumu inatolewa unaandika barua mahakamani ya kuomba nakala ya hukumu. Hii itasaidia hata zile siku 30 au 45 za rufaa zikipita kabla hujapatiwa nakala ya hukumu kujitetea kuwa ulichelewa kwakuwa ulikuwa ukisubiria nakala ya hukumu ambayo uliiomba ndani ya wakati stahiki.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241 bashiryakub@ymail.com
No comments:
Post a Comment