Sunday, October 11, 2015

BENKI YA DUNIA NA JAPAN (JICA) KUBORESHA MAZINGIRA YA BIASHARA NCHINI TANZANIA

  Katibu Mkuu Wizara ya Fedha  na Mlipaji Mkuu wa Serikali Dr. Servacius Likwelile katika majadiliano na Bw. Hiroshi Kato ambaye ni Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo ya Japan (JICA).
 Baadhi ya Ujumbe wa Tanzania na Ujumbe wa Japan wakiwa kwenye majadiliano. Katikati ni Katibu Mkuu na Mlipaji Mkuu wa Serikali Dr. Servacius Likwelile, kushoto kwake ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Zanzibar Bw. Khamis Mussa na Kamishna wa Fedha za Nje Bw. Said Magonya na kulia kwake ni Rais wa JICA Bw. Hiroshi Kato. Katibu Mkuu Wizara ya Fedha  na Mlipaji Mkuu wa Serikali.
 Katibu Mkuu Wizara ya Fedha  na Mlipaji Mkuu wa Serikali Dr. Servacius Likwelile wa kwanza kulia akiendelea  kufanya majadiliano na ujumbe wa JICA ukiongozwa na Rais wa JICA Bw.  Hiroshi Kato wa pili kulia.
Ujumbe wa Tanzania na Ujumbe wa JICA wakimsikiliza kwa makini Katibu Mkuu Wizara ya Fedha  na Mlipaji Mkuu wa Serikali Dr. Servacius Likwelile wakati wa majadiliano ya kuwekeza katika sekta ya umeme, utalii na kuboresha mazingira ya biashara.

JAPANI YAKUBALI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA TANZANIA KATIKA KUCHANGIA BAJETI YA MAENDELEO KATIKA MIKUTANO YA WB & IMF  HAPA NCHINI  PERU - LIMA

Serikali ya Jumhuri ya Muungano wa Tanzania yapata dola milioni 280 kutoka Benki ya Dunia na Japani, fedha hizo zitatumika kusaidia mipango mbalimbali nchini Tanzania. Akiongea  na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia ukanda wa Afrika Bw. Makhtar Diop na Rais wa Shirika la Maendeleo ya Japan-JICA Bw. Hiroshi Kuto, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali Dkt. Servacius  Likwelile alisema dola milioni 230 zimetolewa na Benki ya Dunia. Kiasi cha  Dola milioni 100 ni kwa ajili ya kuhimiza mambo ya uwazi katika utawala, dola milioni 80 ni kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kufanya biashara na dola milioni 50 ni kwa ajili ya kuboresha sekta ya hifadhi ya jamii yaani  pensheni.

Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) wamethibitisha kuendelea kuunga  mkono Serikali ya Tanzania  katika mipango ya maendeleo. Wakiwa katika kikao na ujumbe kutoka Tanzania, Bw. Hiroshi Kato ambaye ni Makamu wa Rais wa shirika hilo alisema  kuwa , Serikali ya Japan kupitia shirika lao la maendeleo ( JICA) lina mipango ya kuunga mkono Tanzania   na Kenya watajenga barabara ambayo itaunganisha  Arusha na Mombasa kwa kiwango cha juu ili kuweza kurahisisha mazingira ya biashara na utalii. Bw. Kato katika mazungumzo yake aliongeza kuwa bado wao wako tayari kusaidia kupitia bajeti kuu ya Serikali kama vile ambavyo wamekuwa wakifanya  miaka ya  nyuma.

Akifafanua kuhusiana na sekta ya hifadhi ya jamii Dkt. Likwelile alisema kuwa uboreshaji wa pension umeahirishwa kwa sasa na wameomba Shirika la kazi la Kimataifa (ILO) wafanye mapitio ya sekta hiyo na baada ya mapitio hayo ndio tutajua ni masuala gani tunaweza kuyazingatia ili kuboresha sekta yetu ya hifadhi ya jamii.

Katika majadiliano na viongozi wa benki ya Dunia  Dkt. Lilkwelile aliwaeleza kuwa, Tanzania kuna changamoto kubwa kwasababu uzalishaji wa umeme kupitia maji umepungua kutokana na kina cha maji kupungua katika maeneo ya uzalishaji hivyo tunategemea gesi.

“Tunategemea gesi ya Kinyerezi One ambayo inatupatia megawatts 405-407, na vilevile tunapata umeme kutokana na matumizi ya mafuta ambapo ni gharama kubwa na uzalishaji haujafikia lengo ambalo ni mahitaji yetu ya siku ambayo tunapata. Tuna mapungufu ya megawatts160, suala hili limeleta shida sana  kwenye bajeti yetu”. Alisisitiza Likwelile

Benki ya Dunia watashirikiana na Idara ya Serikali ya Uingereza ya maendeleo ya Kimataifa (DFID) pamoja na Japan kuwekeza katika reli ya kati ili kuunga mkono jitihada zetu za kuboresha huduma ya reli nchini Tanzania, Likwelile aliendelea kufafanua.

Kwa upande wa maendeleo ya uchumi wa Tanzania ni kwamba uchumi bado unakuwa kati ya asilimia 6.5 mpaka 7, mfumuko wa bei umeshuka japokuwa unapanda kidogo kufikia asilimia 6.4, akiba ya fedha za kigeni bado inawezesha Tanzania kuingiza bidhaa za karibu miezi minne, aliongeza Dkt. Likwelile.

Katika majadiliano hayo Rais wa Benki ya Dunia kanda ya Afrika Bw. Diop alisisitiza kuwa Tanzania iweke msisitizo mkubwa kwenye kilimo chenye tija na cha kibiashara pamoja  na kuwekeza kwenye miundombinu ambayo itasaidia uchumi kuimarika hasa kwenye nishati, reli, barabara, mawasiliano pamoja na kuwekeza kwa vijana  kwani ni wengi sana na  wanahitaji uhakika wa kupata ajira. Tukiweza kufanya kilimo kikawa cha tija na kuwekeza kwenye viwanda vidogovidogo na kuwapa vijana elimu ambayo itawasaidia kuweza kujitegemea, Tanzania itaweza kusonga mbela.

Akiendelea kufafanua Bw. Diop alisema, kutokana na uchumi wa Tanzania ulivyo hakuna sababu ya kukusanya mapato yetu ya kodi kwa kiwango cha sasa, tuna uwezo wa kwenda hadi asilimia 12 ya pato la Taifa. Naye Dkt. Likwelile alimuhakikishia Rais wa Benki ya Dunia kanda ya Afrika Bw. Diop kuwa lengo la Tanzania ni hili ila tunahitaji uwekezaji ili tuweze kufikia lengo tuulilokusudia,  maana tumeweka ukomo wa fedha angalau tufikie mpaka asilimia14.5 lakini tunaweza kwenda mpaka asilimia 17 – 20 katika miaka mitatu ijayo.

Katika kuhitimisha majadiliano hayo Dkt. Likwelile alisema kwamba ushirikiano kati ya Tanzania na Benki ya Dunia ni mzuri na mkubwa sana. Kiwango cha fedha ambacho tunakipata kutoka kwao kinazidi kuongezeka na wameweza kuturuhusu kuwekeza kutumia mlango  mwingine mfano kwenye Chama cha Maendeleo ya Kimataifa(IDA) na pia kwa sasa tumeweza kupata fedha kupitia Benki ya Kimataifa ya ujenzi na maendeleo(IBRD) kwa ajili ya upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam.
Hali ya hewa mjini hapa ni baridi sana.

Imetolewa na: Bi. Ingiahedi Mduma
     Msemaji wa Wizara ya Fedha
                                                                    Peru – Lima

                                                            

No comments: