KUSOMA ZAIDI kliks goes to sheriayakub.blogspot.com
Na Bashir Yakub.
MARA kadhaa mkopaji anaposhindwa kulipa mkopo hukimbilia mahakamani ili kuona kama anaweza kupata unafuu hasa linapokuja suala la wakopeshaji wake kutaka kuuza nyumba/kiwanja alichoweka rehani. Ni ukweli usiopingika kuwa hatua hii imewasaidia wengi hasa wale wanaowahi. Yapo makala tuliwahi kuandika kuhusu hatua za kuchukua hasa inapotokea kuwa nyumba yako inataka kuuzwa.
Makala yalieleza namna na hatua za kufuata ili kuokoa nyumba. Kwenda mahakamani kuzuia nyumba isiuzwe baada ya kushindwa kurejesha kiasi cha rejesho sio ukorofi isipokuwa ni kutekeleza lililo ndani ya sheria hasa pale panapo sababu za msingi za kufanya hivyo.
Mahakama za ardhi za wilaya na mahakama kuu hasa ya ardhi ndizo mahakama zenye mamlaka katika kutoa mazuio haya kutegemeana na thamani ya nyumba/kiwanja na kiasi cha deni kilichohusishwa katika muamala huo.
Swali kwetu ni kama baada ya kuwa umeenda mahakamani na kubahatika kupata zuio la kutouzwa nyumba yako, je upande wa wakopeshaji wanaweza kukata rufaa kupinga amri hiyo na kufanikiwa. Majibu ya swali hili ndio makala ya leo.
1.HAKI YA RUFAA.
Kifungu cha 74 cha sura ya 33 Sheria mwenendo wa madai kinaeleza rufaa katika amri mbalimbali za mahakama. Kifungu kilieleza wazi kuwa kutakuwa na rufaa kutoka mahakama za wilaya na zile za hakimu mkazi ambapo rufaa hizo zitatakiwa kwenda mahakama kuu.
Kwa wasiojua maana ya rufaa, hii ni hatua ya kupeleka malalamiko mbele zaidi baada ya kuwa hukuridhishwa na uamuzi wa mahakama iliyoamua shauri lako katika hatua za awali.
Nje ya hilo kifungu cha 78 cha sheria hiyohiyo kiliruhusu pia kufanyika kwa marejeo iwapo mtu hakuridhika na maamuzi ya amri ya mahakama. Marejeo ni hatua ya mahakama kuitisha faili tena na kupitia kilekile ilichoamua ili kujiridhisha na uhalali wake. Hii hutokea baada ya upande wa pili kuomba hilo kufanyika. Kwahiyo ilikuwa ikiwezekana kutolewa amri ya kuzuia nyumba kuuzwa halafu baadae faili likaitishwa tena na kurudiwa na kutolewa amri nyingine ambayo inaweza kuwa ileile ya kutouzwa au ikabadilishwa ikawa amri mpya ya kuuza.
2. SHERIA YA UKOPAJI FEDHA NA KUWEKA REHANI.
Mwaka 2008 ilikuja sheria ambayo iliitwa kwa jina la sheria ya ukopaji fedha na kuweka rehani. Sheria hii inazungumzia masuala yote nyeti yanayohusu kukopeshwa fedha na kuweka rehani mali .
Ni sheria inayoratibu masuala yahusuyo kuuzwa kwa mali zilizowekwa rehani na kutouzwa kwake. Inazungumzia haki za mkopaji na mkopeshaji halikadhalika wajibu wao wote katika nafasi zao. Kutokana na ujio wa sheria hii masuala kadhaa katika sheria ya ardhi ya 1999 sambamba na sheria ya mwenendo wa madai sura ya 33 zimelazimika kufanyiwa marekebisho ili kukidhi malengo kadhaa .
3. AMRI YA KUTOUZA NYUMBA YA MKOPO HAIKATIWI RUFAA.
Hapo juu tuliona kuwa awali ilikuwa ni ruhusa kwa mtu kukata rufaa hata kwa amri iliyotolewa kuzuia nyumba/kiwanja cha mkopo kuuzwa. Mahakama ya wilaya ingeweza kutoa amri kuwa nyumba fulani isiuzwe hata kama mkopaji yuko nje ya makubaliano kwasababu kadha wa kadha.
Hata hivyo ilikuwa ni haki ya mkopeshaji ambaye ndiye hutaka kuuza nyumba kukata rufaa na kupinga amri hiyo. Kama amri hiyo ingetolewa mahakama ya wilaya au ya hakimu mkazi basi mkopeshaji angeweza kukata rufaa kwenda mahakama kuu. Na huko ingewezekana kutolewa uamuzi uleule au uamuzi mpya ambapo pengine amri ya kutouzwa ingebatilishwa na kuruhusu uuzaji kuendelea.
Kwa sasa kutokana na sheria hii ya masuala ya ukopeshaji fedha na rehani kifungu hiki kimefanyiwa marekebisho na sasa ni kuwa amri ya mahakama iwe ya wilaya au mahakama kuu ikishapita na kutoa zuio la kutouzwa nyumba ya mkopaji basi huwezi tena kukata rufaa kupinga jambo hilo. Amri hiyo ikishatolewa basi inakuwa imetolewa. Ni kutokana na hilo kichwa cha makala haya kimekuwa , amri ya kutouza nyumba ya mkopo haikatiwi rufaa.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241 bashiryakub@ymail.com
No comments:
Post a Comment