Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi (Mb), akihutubia
wananchi wa Kigamboni katika Uzinduzi wa Mpango Kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni
Katika Uwanja wa Tangamano - Mnadani Vijibweni.
Mkurugenzi
Msaidizi wa Idara ya Mipango Miji, Bibi Immaculata Senje akitoa taarifa fupi ya
Mpango Kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni wakati wa Uzinduzi wa Mpango huo.
Wasanii
wa kikundi cha Ngoma za kitamaduni wakiburudisha wakati wa Uzinduzi Mpango
Kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni.
Mkuu
wa Wilaya ya Temeke Bibi Sophia Mjema akizungumza na wananchi wa Kigamboni
katika Uzinduzi wa Mpango Kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni, kulia ni Katibu
Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bwn. Alphayo Kidata.
Aliyekuwa
Mbunge wa Kigamboni Faustine Ndugulile akizungumza na wananchi wa Kigamboni
katika Uzinduzi wa Mpango Kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni, nyuma yake ni
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ,William Lukuvi (Mb), Katibu
Mkuu Bwn. Alphayo Kidata na Mkuu wa Wilaya ya Temeke Bibi Sophia Mjema.
Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi (Mb) akikata utepe
kuzindua Mpango Kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni, kulia ni Naibu wake Bibi Angela
Kairuki (Mb), wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Temeke Bibi Sophia Mjema na aliyekuwa
Mbunge wa Kigamboni Faustine Ndugulile.
Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi (Mb) akionesha
vitabu vya Mpango Kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni.
Wananchi
mbalimbali ambao ni wakazi wa Mji wa Kigamboni wakisilikiza maelezo mbalimbali
kutoka kwa viongozi katika mkutano wa hadhara wakati wa Uzinduzi wa Mpango
Kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni.
Picha
za Mji Mpya wa Kigamboni.
HOTUBA
YA MGENI RASMI, WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI, MHE. WILLIAM V.
LUKUVI, KATIKA UZINDUZI WA MPANGO KABAMBE WA MJI MPYA WA KIGAMBONI TAREHE 12 SEPTEMBA 2015 KATIKA UWANJA WA
TANGAMANO – MNADANI VIJIBWENI
Mhe. Waziri wa Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa
Mhe. Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi,
Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Temeke,
Makatibu Wakuu,
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa
ya Temeke,
Wageni waalikwa,
Mabibi na Mabwana,
Ndugu Wananchi,
Napenda kuchukua fursa hii kwa niaba
ya Serikali kuwashukuru wananchi wa Kigamboni kwa kuitikia wito wa kuhudhuria
mkutano huu wa uzinduzi wa Mpango Kabambe “Master
Plan” wa Mji Mpya Kigamboni ambao tumeusubiri kwa muda mrefu.
Ndugu Wananchi,
Kama nilivyowahi kuwaeleza siku za
nyuma dhana ya Mji Mpya wa Kigamboni iliasisiwa na Rais wa Jamhuri wa Muungano
wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete mara baada ya kuingia madarakani.
Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
alitoa agizo hilo kwa Wizara mwaka 2006 na baadaye kuingizwa kwenye Ilani ya CCM
ya mwaka 2010-2015 ambayo ilikusudia kuinua hadhi ya Jiji
la Dar es Salaam na Taifa kwa ujumla katika kuleta ustawi wa wananchi
kiuchumi na kijamii. Agizo hilo limetekelezwa kwa kuandaa Mpango Kabambe wa Mji
Mpya Kigamboni ambao umezingatia hatua muhimu kwa mujibu wa sheria na mahitaji
ya wadau.
Ndugu Wananchi,
Matokeo
yanayotarajiwa katika utekelezaji wa mpango ni pamoja na:
i.
Kuwa na maeneo ya uwekezaji yatakayotoa
fursa za ajira kwa wananchi na kuleta
ustawi wa kiuchumi na kijamii na hivyo kuwezesha kupanda kwa viwango vya uchumi kwa mtu mmoja moja na
Taifa kwa ujumla;
ii.
Kuwa na mji uliopangwa vizuri na wenye mazingira mazuri yanayokidhi viwango vya usalama vya kimataifa
hivyo kutoa fursa kwa wazawa na wageni
kutoka nje ya nchi kuishi kwa amani na utulivu;
iii.
Kuwa na mji wenye mfumo wa kisasa wa njia za mawasiliano na
miundombinu ya kuiunganisha
nchi yetu na mataifa mengine kiutandawazi na hivyo kumudu ushindani
wa kimataifa katika masuala ya
kiutandawazi;
iv.
Kuwa na mji wenye huduma za kisasa za ofisi,
na kumbi za mikutano, maeneo ya
biashara, hoteli za kitalii zenye fukwe nzuri katika hadhi ya kimataifa;
v.
Kuwa
na mji uliojengwa kwa viwango vya kimataifa vinavyozingatia mazingira safi,
miundombinu inayoendana na shughuli za kiuchumi hivyo kuimarisha afya za
wananchi.
Ndugu Wananchi,
Zimekuwepo
jitihada mbalimbali zilizofanywa na
serikali kwa kushirikiana na ninyi wananchi na wadau wengine katika uandaaji wa Mpango huu. Naomba nitumie fursa
hii kuwashukuru wananchi wa Kigamboni na
wadau walioshiriki kwa namna mbalimbali
katika kufanikisha ukamilishaji wa Mpango huu. Baadhi yenu mlitoa maoni na
mapendekezo kuhusu Mpango, kupitia na kuboresha nyaraka mbalimbali
zilizohusiana na Mpango na kuzihuisha kwa lengo la kuboresha na kuukamilisha
Mpango kwa maslahi ya umma.
Mojawapo ya masuala
yaliyoshughulikiwa ni pamoja na kupunguza eneo la Mpango kutoka hekta 50,934
hadi 6,494, kutoka Kata tisa (9) na kubaki sita (6). Kurekebisha
matangazo ya zamani na kutayarisha matangazo mapya ambayo ni Namba 257, 258 ya tarehe 17/7/2015
na Tangazo Namba 301 la tarehe 24/7/2015.
Mchakato huu ulifuata misingi ya
utawala bora kwa njia ya ushiriki na ushirikishwaji wa wadau wote.
Ndugu
wananchi,
Kwa mujibu wa
dhana mpya, uendelezaji wa Mpango Kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni utafanyika
kwa namna kuu tatu:
i.
Wamiliki wa ardhí kuendeleza maeneo yao
kulingana na Mpango;
ii.
Wamiliki wa ardhí kuingia ubia na
waendelezaji wengine na kuendeleza maeneo yao kulingana na Mpango; na,
iii.
Wamiliki wa ardhí kuuza ardhí yao kwa
bei ya soko na wanunuzi kuiendeleza kulingana na Mpango.
Maeneo yote
yanayopitiwa na miundombinu na huduma za kijamii yatatwaliwa na Serikali na
wananchi kulipwa fidia stahili kwa mujibu wa Sheria za nchi.
Ndugu Wananchi,
Hatua iliyopo
mbele yetu sasa ni kuutekeleza Mpango kwa kuanza na shughuli zifuatazo: kutambua
na kupima maeneo ya miundombinu tukianza
na miundombinu ya barabara kubwa zenye viwango vya upana wa mita 70 na 140 zilizopo
kwenye eneo la Mpango; Kufanya uthamini wa maeneo yanayopitiwa na barabara na
kuaadaa mipango ya kina. Zoezi hili litaanza rasmi leo mara baada ya uzinduzi
wa Mpango. Wale wote watakaopitiwa na miundo mbinu ya barabara, watalipwa
vizuri kwanza kabla ya ujenzi wa miundo mbinu yenyewe. Kwa hiyo ni marufuku kwa mtu kuondolewa na
kuvunjiwa nyumba yake bila kulipwa fidia stahiki.
Nichukue fursa
hii tena kuwashukuru kwa namna ya pekee wananchi wa Kigamboni kwa uvumilivu
wenu na ushiriki wenu uliotuwezesha kwa pamoja kufikia hatu hii ya leo; ambayo imetuwezesha
kuandika historia kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Baada ya kusema
hayo natamka kuwa Mpango Kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni umezinduliwa rasmi
leo tarehe 12 Septemba, 2015.
KARIBUNI SANA!
RISALA
FUPI YA UZINDUZI WA MPANGO KABAMBE WA
MJI
MPYA WA KIGAMBONI
Mhe. Mgeni Rasmi,
Awali ya yote tunapenda kukushukru kwa kukubali
kutoa muda wako na kuja katika tukio hili muhimu la kihistoria tukizingatia
kwamba unayo majukumu mengi ya kitaifa yanayokukabili.
Mhe. Mgeni Rasmi,
Mpango Kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni
ulianza kuandaliwa mwaka 2008 baada ya kusudio la kuandaa Mpango kutangazwa
katika Gazeti la Serikali Na. 229 la tarehe 18/10/2008.
Mhe. Mgeni Rasmi,
Mchakato wa Uandaaji wa Mpango Kabambe
wa Mji Mpya wa Kigamboni ulipitia hatua mbalimbali kulingana na Sheria ya
Mipangomiji Na. 8 ya mwaka 2007. Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kufanya uhamasishaji wa wadau mbalimbali na
kutoa elimu kupitia warsha na mikutano.
Mhe. Mgeni Rasmi,
Mpango Kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni
umeainisha matumizi mbalimbali ya ardhi katika Kanda kuu tano (5)
Kanda hizo ni:
(i)
Eneo la Kitovu cha Mji (CBD) ambalo ni
maalum kwa shughuli za biashara
(ii)
Eneo la Makazi
(iii)
Eneo la Viwanda na Utafiti
(iv)
Maeneo ya Taasisi zikiwemo za elimu
(v)
Eneo la Utalii na Burudani.
Maeneo haya yote yanaunganishwa na mitandao ya
Barabara, Reli na usafiri wa majini.
Mhe. Mgeni Rasmi,
Hatua iliyofikiwa leo katika utekelezaji
wa Mpango wa Uendelezaji Mji Mpya wa Kigamboni ni mafanikio makubwa
yaliyotokana na juhudi zako katika kuhakikisha kwamba wanakigamboni wananufaika
na mpango huu. Ushirikiano wa wadau mbalimbali hususan wananchi wa Kigamboni
kupitia wawakilishi wao umechangia kwa kiasi kikubwa katika kufikia
ukamilishaji wa maandalizi ya Mpango huu.
Mhe. Mgeni Rasmi,
Uzinduzi wa Mpango huu ni mwanzo wa
utekelezaji wake kwa kuanzia na ufunguzi wa barabara kuu zenye upana wa mita
140 na mita 70. Ufunguaji wa barabara hizi kuu utasaidia kutambua maeneo
yaliyotengwa kwa matumizi ya mbalimbali ya ardhi kama yalivyoainishwa hapo juu.
Kabla ya kuanza kwa upimaji wa barabara hizi kuu wananchi wanaopitiwa na
miundombinu hii watatambuliwa, kufanyiwa uthamini wa mali zao na kulipwa fidia
stahiki.
Kazi nyingine inayotarajiwa kuanza mara
tu baada ya uzinduzi huu ni utayarishaji wa mipango ya kina ambapo baada ya
kuidhinishwa itawezesha upimaji wa maeneo mengine yaliyotengwa kwa matumizi
mbalimbali. Hii itawapa fursa wananchi kuanza kuendeleza maeneo yao kulingana
na mpango.
Hitimisho
Mhe. Mgeni Rasmi,
Naomba kuhitimisha kwa kusema kwamba
tukio la leo linafungua ukurasa mpya katika uendelezaji wa Mji Mpya wa
Kigamboni.
Tunakushukuru sana.
No comments:
Post a Comment