Mkuu
wa Wilaya ya Karatu, Mkoani Arusha Omary Kwaang’ (katikati mwenye kaunda suti) akiwa na baadhi ya watumishi
wa wilaya hiyo, akikagua lambo la maji eneo la Endesh, linalotumiwa na
mifugo na binadamu, lililogharimu sh169 milioni kwa ufadhili wa shirika la
World Vision.
Mkuu
wa Wilaya ya Karatu, Mkoani Arusha Omary Kwaang’ (kushoto) akiwa na baadhi ya watumishi
wa wilaya hiyo, akikagua lambo la maji eneo la Endesh, linalotumiwa na
mifugo na binadamu, lililogharimu sh169 milioni kwa ufadhili wa shirika la
World Vision.
WANANCHI
12,082 wa Kata ya Baray Wilayani Karatu Mkoani Arusha wamekabidhiwa miradi nane
ya elimu na afya ambayo imegharimu sh447.8 milioni kwa ufadhili wa shirika
lisilo la kiserikali la World Vision Korea.
Mratibu
wa mradi wa World vision Karatu John Massenza akikabidhi jana miradi hiyo kwa
mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo John Mabula alisema itawanufaika wakazi wa vijiji vitatu vya
Dumbachang, Mbuga Nyekundu na Jobaj.
Massenza
alitaja miradi hiyo kuwa ni madarasa matatu, ofisi ya walimu na choo cha
wanafunzi ya shule ya msingi Mbuyuni iliyogharimu sh83 milioni na madawati 200
kwa ajili ya wanafunzi wa shule hiyo iliyogharimu sh13 milioni.
Alitaja
mingine ni samani na vifaa zahanati ya Endesh sh11 milioni, madawati 100 ya shule
ya msingi Mohedagew Gidamilanda sh13 milioni na vifaa vya vikundi 11 vya hisa
vijiji vya Dumbecha, Jobaj na Mbuga Nyekundu sh5 milioni.
“Mingine
ni lambo kwa matumizi ya binadamu na wanyama sh169 milioni, zahanati na choo
Endesh sh83 milioni, vitabu na vifaa vya ufundishaji 1,570 vya sh11 milioni na
madarasa mawili sh53.9 Endesh,” alisema Massenza.
Alisema
katika wilaya hiyo, World vision ilianza kufanya shughuli zake mwaka 2009
kwenye tarafa za Endabash na Lake Eyasi ambapo imekuwa ikitekeleza miradi
mbalimbali ya maendeleo kwenye sekta tofauti.
“Miradi
hiyo iliyotekelezwa ni ya upande wa sekta ya elimu, afya, kilimo, maji na
ufadhili wa watoto kwa kushirikiana na halmashauri ya wilaya ya Karatu na wana jamii
wa eneo hili,” alisema Massenza.
Kwa
upande wake, mkuu wa wilaya ya Karatu Omary Kwaang’ alipongeza shirika la World
vision kwa kufanikisha ujenzi wa miradi hiyo ya thamani ya sh447.8 milioni
ambayo itanufaisha jamii ya wafugaji na wakulima.
Kwaang’
aliwataka wananchi wa kata hiyo kuhakikisha kuwa wanaitunza miradi hiyo ili iwe
endelevu na kudumu kwa faida ya kizazi kilichopo na kijacho, kwani shirika la
World vision limetumia gharama kubwa kufanikisha miradi hiyo.
Alisema
kwenye suala la zahanati wilaya ya Karatu imepiga hatua kwenye kutekeleza sera
ya wizara ya afya inayotaka kila kijiji kiwe na zahanati kwani wamejenga
zahanati kwenye vijiji 45kati vijiji 58 hivyo vimebaki vijiji 13.
“Nawapongeza
viongozi na wananchi wa wilaya ya Karatu kwa kupiga hatua kwenye ujenzi wa zahanati,
ila tujitahidi kwenye elimu kwani vyumba vya madarasa vinahitajika 1,109 na
vilivyopo ni 875,” alisema Kwaang’.
Alisema
kwenye ujenzi wa nyumba za walimu kuna hitajika 694 na zilizopo ni 578 na
matundu ya choo yanahitajika 1,221 na pungufu ni matundu 975 hivyo wajitahidi
kumalizia mapungufu yote wakishirikiana na serikali ya wilaya hiyo.
No comments:
Post a Comment