KUSOMA ZAIDI links goes to sheriayakub.blogspot.com
Na Bashir Yakub.
KISHERIA haizuiwi kuweka rehani nyumba ya makazi kwa ajili ya kupata mkopo kutoka taasisi yoyote ya fedha. Jambo la msingi sana ni kuwa watoa mkopo wajiridhishe na umiliki wa nyumba hiyo hasa kwa kuangalia ikiwa ni mali ya familia au hapana ili wachukue hadhari za kisheria.
Nyumba ya makazi ni ipi. Nyumba ya makazi ni ile nyumba ambayo inatumiwa na binadamu kuishi lakini zaidi wanaoishi mle ndani iwe ni familia ya mchukua mkopo. Yawezekana nyumba ikawa ni ya makazi kwa watu wengine lakini ni ya biashara kwa mchukua mkopo. Kwa mfano nyumba za kupanga ambapo mwenye nayo anaishi kwingine na nyumba iko kwingine ikiwa na watu wengine.
Nyumba ya namna hii haitaingia kwenye nyumba ya makazi kwa tafsiri hii. Hata hivyo haitarajiwi mchukua mkopo kuhamia kwenye nyumba ambayo sio ya makazi kwa makusudi na kuifanya ya makazi akilenga kuhadaa ili kupata upendeleo wa mahakama. Akifanya hili atakuwa amedanganya na ni kosa kama tutakavyoona.
1.MAKOSA YA KISHERIA KWA MKOPAJI.
( a ) Sheria ya masuala ya rehani ya 2008 inamtaka mkopaji kutofanya udanganyifu wa aina yoyote kwa taasisi inayotarajia kumpa mkopo. Moja ya udanganyifu ni kama ilivyoelezwa hapo juu lakini pia upo udanganyifu mwingine mwingi ambao hufanywa na wakopaji. Kwa mfano kuweka rehani nyumba moja kwa taasisi tofauti, kudanganya nyumba sio ya familia wakati ni ya familia na udanganyifu mwingine mwingi ambao hulenga kumnufaisha mkopaji.
2. ADHABU YA KUTENDA KOSA LA UDANGANYIFU KATIKA KUCHUKUA MKOPO.
Kisheria tendo likishakuwa kosa ni lazima iwepo adhabu yake. Vivyo hivyo mkopaji kumdanganya mkopeshaji nalo ni tendo ambalo huadhibiwa. Sheria inasema kuwa hatia ya udanganyifu wa mkopaji inapotangazwa basi adhabu yake ni kulipa faini ambayo ina thamani ya nusu ya mkopo aliokuwa amechukua. Hii ina maana kuwa, kama alichukua mkopo wa milioni 200 basi faini yake ni milioni 100 halikadhalika kama alichukua milioni kumi basi faini yake ni milioni tano.
Ikiwa hana hizo hela basi itatakiwa kwenda jela kutumikia kifungo kisichopungua miezi kumi na mbili. Kifungo kisichopungua miezi kumi na mbili maana yake kinaweza kuzidi miezi kumi na mbili kutegemea na ukubwa wa tatizo lenyewe. Hivyo wakopaji wajihadhari na kutoa taarifa za uongo hasa kudanganya kuwa mali si ya familia au kutumia mali moja kuchukulia mkopo sehemu zaidi ya moja n.k.
3. UPENDELEO KWENYE NYUMBA YA MAKAZI
( a ) Sheria inasema kuwa iwapo itabainika kuwa nyumba iliyowekwa rehani ni ya makazi na mkopaji analeta zuio la kutouzwa nyumba hiyo basi mahakama ikijiridhisha na hilo inaweza kukubali ombi hilo.
Mahakama itakubali ombi hilo la kuzuia nyumba kuuzwa kwa kuzingatia kiwango cha hela kilichosalia yaani kile kiasi ambacho mkopaji ameshindwa kulipa. Mara kadhaa hutokea kuwa mkopaji amelipa kiasi kikubwa na kusalia na deni la kiasi kidogo ambacho kwa akili ya kawaida tu na kutokana na mazingira yaliyopo akipewa muda mwingine anao uwezo wa kulipa na kumalizia kabisa deni. Ni katika mazingira haya zuio la kutouzwa nyumba ya makazi litakubaliwa.
( b ) Hili litakwenda sambamba na kuangalia iwapo wajibu wa mkopaji uliowekwa katika mkataba wa mkopo unaweza kuzungumzika. Ikiwa mkopaji alikuwa mgonjwa sana na ushahidi upo na hivyo alishindwa kuendelea na biashara na hivyo kutokurejesha, na sasa ana afya njema na anaweza kufanya biashara na kurejesha, basi wajibu wake ikiwa unaweza kurekebishika kwa namna hiyo au namna nyingine mahakama inaweza kutoa zuio ili kutoa nafasi nyingine kwa mkopaji.
( c ) Pia ikiwa mahakama itajiridhisha kuwa nyumba husika ina thamani kubwa kiasi kwamba hata mkopaji akiongezewa muda mwingine bado akishindwa kulipa huko mbeleni nyumba husika ikiuzwa mtoa mkopo hatakuwa na hasara ataweza kurejesha hela yake yote pamoja na riba, basi zuio la kutouza linaweza kutolewa kwa kulizingatia hilo.
Izingatiwe kuwa zuio katika mazingira haya niliyoeleza linawezekana ikiwa nyumba ilyowekwa rehani ni ya makazi.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241 bashiryakub@ymail.com
No comments:
Post a Comment