TAARIFA KWA
VYOMBO VYA HABARI
CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kitatoa tuzo kwa Rais
Jakaya Kikwete pamoja na wanamichezo 10 waliofanya vizuri zaidi katika miaka 10
akiwa Rais wa Tanzania.
Tukio hilo ambalo pia litahudhuriwa na Rais Kikwete, litafanyika Oktoba
8, mwaka huu ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam likiwa na lengo la
wanamichezo kumuaga Rais Jakaya Kikwete.
TASWA itakabidhi tuzo maalum kwa Rais ikiwa ni kuthamini mchango wake kwa
maendeleo ya michezo wakati wa miaka 10 ya uongozi wake na imebariki tukio hilo
kama ‘JK na Wanamichezo’.
Licha ya kutoa tuzo kwa Rais na wanamichezo 10 waliofanya vizuri zaidi,
pia TASWA itatoa vyeti maalum kwa kampuni mbalimbali zilizosaidia kwa kiasi
kikubwa kudhamini michezo katika miaka 10 ya Rais Kikwete.
Maandalizi muhimu yamekamilika kuhusiana na tukio hilo, ambapo
wawakilishi kutoka vyama vyote vya michezo hapa nchini pamoja na wanamichezo
wataalikwa kuhudhuria tukio hilo la kihistoria.
TASWA inamshukuru Rais Kikwete kwa kukubali kujumuika nasi siku hiyo ili
kuagana na wanamichezo, ambao wameshuhudia mambo mazuri akiwafanyia katika
uongozi wake, ambao utafikia tamati baada ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na
Madiwani utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Pia TASWA inaishukuru Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa
ushirikiano mkubwa iliotoa kuhakikisha tukio hilo linafanikiwa.
Tayari wadhamini mbalimbali wamejitokeza kusaidia na tunaomba wengine
watuunge mkono, ambapo Jumanne Oktoba 15, TASWA itafanya mkutano na waandishi
wa habari kutangaza mdhamini mshiriki mmoja, mkutano utakaofanyika ukumbi wa
City Sports Lounge, Dar es Salaam.
TASWA imeona kuna haja ya wanamichezo
kuagana
na Rais Kikwete na kumpa tuzo kutokana na masuala mbalimbali aliyofanya kwa
miaka yake 10 katika kusaidia kukuza michezo na sanaa hapa nchini.
Baadhi
ya mambo hayo ni serikali yake ilivyolipia makocha wa michezo ya soka, netiboli na ngumi
na pia serikali ilipeleka wanariadha wetu China, Ethiopia na New Zealand kwa
maandalizi ya mashindano ya kimataifa.
Pia tutamkumbuka Rais Kikwete kwa uamuzi wa
kurejesha michezo shuleni pamoja na mashindano ya michezo kwa shule za msingi
na sekondari (UMISHUMTA na UMISETA).
Yapo mambo mengi ambayo tukiyataja yote aliyofanya
kuhusu michezo yatachukua nafasi kubwa, hivyo tuna kila sababu wanamichezo
kujitokeza na kuagana na Rais wetu.
Ahsanteni,
Juma Pinto
Mwenyekitii TASWA
11/09/2015.
No comments:
Post a Comment