Friday, September 11, 2015

RUKSA WACHIMBAJI WADOGO KUMILIKI LESENI KADRI WAWEZAVYO

 Ofisa Madini Mkazi wa Kahama, Bibi Sophia Omar, akifungua mafunzo kwa wachimbaji wadogo na wamiliki wa leseni za madini kuhusu matumizi ya huduma mpya ya utoaji wa leseni za madini kwa njia ya mtandao. Mafunzo hayo yamefanyika leo Septemba 11, 2015 mjini Kahama ikiwa ni mwendelezo wa mafunzo yanayotolewa na Wizara ya Nishati na Madini kwa wachimbaji wadogo nchi nzima.
 Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini Mkoani Shinyanga (SHIREMA), Bibi Bahati Kalekwa akitoa neno la shukrani kwa Wizara ya Nishati na Madini kuandaa na kuendesha mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini kote kuhusu matumizi ya mfumo mpya wa utoaji leseni za madini kwa njia ya mtandao. Wilayani Kahama, mafunzo hayo yamefanyika leo, Septemba 11, 2015.
 Mtaalamu kutoka Kitengo cha Leseni, Wizara ya Nishati na Madini, Juma Masoud akiwasilisha mada kwa wachimbaji wadogo na wamiliki wa leseni wilayani Kahama, kuhusu mfumo mpya wa huduma za utoaji leseni za madini kwa njia ya mtandao. Semina hiyo imefanyika Septemba 11, 2015 mjini Kahama ikiwa ni mwendelezo wa mafunzo yanayotolewa na Wizara husika kwa wachimbaji wadogo na wamiliki wa leseni za madini nchini kote.
Mtaalamu kutoka Kitengo cha Leseni cha Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Nuru Shabani, akiwasilisha mada kwa wachimbaji wadogo na wamiliki wa leseni wilayani Kahama, kuhusu mfumo mpya wa huduma za utoaji leseni za madini kwa njia ya mtandao. Semina hiyo imefanyika Septemba 11, 2015 mjini Kahama ikiwa ni mwendelezo wa mafunzo yanayotolewa na Wizara husika kwa wachimbaji wadogo na wamiliki wa leseni za madini nchini kote.

Na Veronica Simba - Kahama
Serikali imesema wachimbaji wadogo wa madini wanaruhusiwa kumiliki idadi yoyote ya leseni za madini ilimradi waweze kuzifanyia kazi.

Hayo yamesemwa leo Septemba 11, 2015 mjini Kahama na Mtaalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Kitengo cha Leseni, Mhandisi Nuru Shabani wakati akiwasilisha mada kwa wachimbaji wadogo wa madini kuhusu matumizi ya mfumo mpya wa utoaji leseni za madini kwa njia ya mtandao, wakati wa semina iliyofanyika mjini humo.

“Mchimbaji mdogo anaruhusiwa kumiliki idadi yoyote ya leseni anazoweza kumudu kuzifanyia kazi. Kwa upande wa wachimbaji wakubwa, wao wanaruhusiwa kumiliki leseni zisizozidi 20 lakini pia sheria inawataka wawe na uwezo wa kuzifanyia kazi,” amesema Mhandisi Shabani.

Mhandisi Shabani ametoa ufafanuzi huo kufuatia swali lililoulizwa na mmoja wa washiriki wa semina hiyo, ambaye alitaka kufahamu idadi ya leseni anazopaswa kumiliki mchimbaji mdogo wa madini.

Akifafanua zaidi kuhusu umuhimu wa wamiliki wa leseni kuzifanyia kazi, Mhandisi Shabani amesema, kwa yeyote anayemiliki leseni na kuliacha eneo husika pasipo kulifanyia kazi, sheria inaelekeza kuwa mtu huyo anyang’anywe leseni yake.

Amesema, mfumo mpya wa utoaji leseni za madini kwa njia ya mtandao umeweka mazingira wezeshi kwa mmiliki wa leseni ambaye hafanyii kazi eneo lake, kutambulika kwa urahisi na hivyo hakuna namna ambayo mhusika anaweza kufanya udanganyifu kwa Serikali kwa kuhodhi eneo pasipo kulifanyia kazi.

Wizara ya Nishati na Madini ilizindua mfumo wa kutoa huduma za leseni kwa njia ya mtandao mapema mwezi Juni mwaka huu mjini Dodoma ili kutoa huduma za haraka, kuongeza uwazi na kumuwezesha mteja kusimamia leseni zake mwenyewe.

Ni kwa kuzingatia umuhimu wa matumizi ya mfumo huo mpya kwa wadau wa sekta ya madini nchini, Wizara kupitia Kitengo cha Usimamizi wa Leseni inaendesha zoezi nchi nzima kuwaelimisha wadau hao namna mfumo huo unavyofanya kazi.

No comments: