Thursday, September 3, 2015

RAIS KIKWETE KUFUNGUA MKUTANO WA TAKWIMU HURIA KANDA YA AFRIKA

 Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Takwimu Huria Kanda ya Afrika.

Mkutano huo utakaofunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete utafanyika tarehe 4 – 5 Septemba, 2015 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.  Kauli Mbiu ni “Tumia Takwimu Huria  Kuendeleza Afrika” (Developing Africa Through Open Data).

Washiriki takribani 400 kutoka Serikalini, Asasi za Kiraia, Sekta Binafsi, Taasisi za Elimu ya Juu na Washirika wa Maendeleo kutoka ndani na nje ya Nchi wanatarajiwa kushiriki.  

Miongoni mwa washiriki kutoka Serikalini ni pamoja na Wakurugenzi kutoka Idara za Sera na Mipango, Wakuu wa Vitengo vya TEHAMA na Maofisa Takwimu Waandamizi wa Wizara zote.

Mkutano wa Takwimu Huria kwa Kanda ya Afrika ni wa kwanza wa aina yake  Barani Afrika Tanzania ikiwa nchi ya kwanza kuwa mwenyeji.  

Heshima hiyo imetokana na Tanzania kujiunga na Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi (Open Government Partnership – OGP) unaolenga kuifanya Serikali kuwa wazi zaidi na hivyo kuleta uadilifu na uwajibikaji katika kuwahudumia Wananchi. 

Katika utekelezaji wa Mpango wa OGP, Tanzania iliweka kipaumbele katika kuanzisha Tovuti ya Takwimu Huria itakayoweka wazi takwimu mbalimbali za Serikali na Taasisi zake.

Madhumuni ya Mkutano ni kujadiliana kuhusu mfumo wa Takwimu Huria na jinsi utakavyoleta maendeleo hususan kwa nchi za Afrika. 

Mkutano utawawezesha wadau kujadiliana na kubadilishana uzoefu kuhusu mfumo wa Takwimu Huria na kuona jinsi gani Sera za nchi zenye mfumo huo zinavyofanya kazi na kusimamia viwango vya upatikanaji wa Takwimu Huria.

Aidha, Mkutano huo utaihusisha sekta binafsi na wadau wengine katika matumizi ya Takwimu Huria katika kuleta maendeleo ya kasi zaidi Barani Afrika.

Washiriki watajadili jinsi ya kukuza na kuimarisha matumizi ya Mfumo wa Takwimu Huria katika kutoa huduma kwa wananchi hasa katika sekta ya Huduma za Jamii za elimu, afya, maji na kilimo.

Tunaomba ushirikiano wenu ili Mkutano huu ufanyike na kukamilika kwa ufanisi.

Imetolewa na Ofisi ya Rais, Ikulu

No comments: