Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Hatua
thabiti za utekelezaji wa maazimio ya mkutano wa Nane wa Baraza la
Biashara la Taifa (TNBC) zinatarajiwa kujulikana wiki chache zijazo.
Maazimio hayo yanalenga hasa kuimarisha mazingira ya biashara nchini na sekta ya utalii.
Akiongea
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa
TNBC, Bw. Raymond Mbilinyi (Pichani) alisema hatua za utekelezaji maazimio
mbalimbali ya kuimarisha sekta hizo zitajulikana katika mkutano wa 9 wa
baraza hilo unaotarajiwa kufanyika tarehe 2 mwezi ujao (Oktoba).
“Mapendekezo
mengine ni ya kiutawala zaidi ambayo ni rahisi lakini kuna maswala
mengine yatahitaji mabadiliko ya sheria mbalimbali na haya yatatakiwa
kufuata taratibu zinazotakiwa,” alisema Bw. Mbilinyi na kumshukuru Rais
Kikwete kwa kuendesha mkutano huo.
Akielezea
baadhi ya maeneo yanayohitaji kuboreshwa alisema kuwa pamoja na kuwa na
kitengo maalum cha kuhakikisha watanzania wanashiriki kikamilifu katika
ujenzi wa uchumi.
“Hii ina maana kuwa watanzania wasibaki kuwa watazamaji tu bali wawe washiriki katika shughuli za uchumi,” alifafanua.
Alisema
eneo lingine linaloshughulikiwa ni kuwa na eneo au kituo kimoja ambacho
kitarahisisha wafanyabiashara kulipia leseni za biashara na kuwa tayari
kuna kikosi kazi kinachoangalia swala hilo litatekelezwaje.
“Kikosi
kazi hiki kitaangalia jinsi bora ya kutekeleza hili na ikiwezekana
kutumia njia ya mtandao ili kufanya mambo kwa kisasa zaidi,” alifafanua.
Mapendekezo
mengine yanayofanyiwa kazi ni pamoja na kuvutia utaalamu kutoka nje
ambao hauko hapa nchini ili kuwezesha vyuo vikuu hapa nchini kutoa
wahitimu wenye sifa zinazotakiwa na soko la ajira.
Kwa
mujibu wa Bw. Mbilinyi, wadau wa mkutano huo pia walishauri kutumia
vyema swala la soko la nyumba linalokua kwa kasi hapa nchini kwa
kuangalia uwezekano wa kuruhusu wawekezaji toka nje kumiliki nyumba.
Mkutano huo pia wa tarehe 2 Oktoba utaangalia jinsi bora ya kutumia ardhi kwa maendeleo ya wengi.
“Tanzania
tuna ardhi kubwa lakini haijapimwa…hili litafanyiwa kazi,” alisema na
kuongeza kuwa mpango wa MKURABITA ni muhimu ukapewa kipaumbele.
Kwa
upande wa sekta ya utalii, alisema washiriki wa mkutano walipendekeza
kutumiwa kwa utaratibu wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi
katika kuendeleza sekta hiyo kwa mfano katika ujenzi miundombinu kama
viwanja vya ndege.
“Wadau
pia wanataka sekta hii iunganishwe kwenye mpango wa Matokeo Makubwa
Sasa ili kuipa msukumo mkubwa zaidi kimaendeleo…hili pia litazingatiwa
na kufikishwa katika mkutano ujao,” alisema.
Mapendekezo hayo yatafanyiwa kazi na wataalamu wa sekta ya umma na binafsi.
No comments:
Post a Comment