Monday, September 14, 2015

MFUKO WA VYOMBO VYA HABARI TANZANIA KUADHIMISHA MIAKA NANE YA MAFANIKIO

 Afisa Mawasiliano wa Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF), Fausta Msokwa akiongea na waandishi wa habari  mapema leo asubuhi jijini Dar es Salaam juu ya maadhimisho ya miaka nane ya mafanikio ya TMF. Pembeni ni Mkurugenzi wa TMF, Ernest Sungura na Afisa Mafunzo wa TMF, Radhia Mwawanga.
Mkurugenzi wa Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF), Ernest Sungura akiongea kwenye mkutano na waandishi wa habari kutangaza tukio hilo, alisema Tarehe 22 Septemba, 2015 tutakuwa na tukio la madhimisho ambayo yatajumuisha maonyesho kwa ajili ya waandishi wa habari waliowezeshwa na misaada ya TMF kuonyesha kazi zao na jinsi gani zimechangia kuleta uwajibikaji na pia kuonyesha kazi ambazo zimepandisha kiwango cha mijadala ya umma katika masuala husika hususani utawala bora na haki za binadamu pamoja na sherehe ya utoaji tuzo kwa waandishi waliowezeshwa na TMF na kazi zao kuweza kuleta mabadiliko chanya.
Waandishi wa habari wakichukua tukio. --- Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) utaadhimisha miaka nane ya mafanikio katika kuongeza uwajibikaji kwa kuimarisha sekta ya habari nchini Tanzania kupitia tukio ambalo litafanyika jijini Dar es salaam.

 Tukio hilo litawaleta pamoja waandishi wa habari na wanataaluma wengine ambao wamewezeshwa na misaada ya TMF, wafadhili, wadau wa sekta ya habari pamoja na taasisi za kiraia na serikali. Akiongea kwenye mkutano na waandishi wa habari kutangaza tukio hilo, Mkurugenzi wa TMF, Ernest Sungura alisema: “Tarehe 22 Septemba, 2015 tutakuwa na tukio la madhimisho ambayo yatajumuisha maonyesho kwa ajili ya waandishi wa habari waliowezeshwa na misaada ya TMF kuonyesha kazi zao na jinsi gani zimechangia kuleta uwajibikaji na pia kuonyesha kazi ambazo zimepandisha kiwango cha mijadala ya umma katika masuala husika hususani utawala bora na haki za binadamu pamoja na sherehe ya utoaji tuzo kwa waandishi waliowezeshwa na TMF na kazi zao kuweza kuleta mabadiliko chanya. 

 Vile vile kutakuwa na mjadala utakaohusisha wataalamu wa habari na wanaharakati kutoka asasi za kiraia katika kujadili changamoto mbalimbali kama vile kuwajengea uwezo wanahabari na pia kuweka mazingira endelevu na uhuru wa habari. 

Sasa ni miaka nane tangu TMF ilipoanzishwa na tumetoka mbali. Maadhimisho haya yatatupatia fursa ya kutafakari kwa pamoja tulipotoka, mambo tuliyoyafanya na pia tutapeana changamoto kufikiri zaidi jinsi ambavyo sekta ya habari nchini Tanzania inaweza kubadilishwa ili kukuza uwajibikaji.”   Tangu ilipoanzishwa mwaka 2008, TMF imetoa misaada na kuwawezesha waandishi wa habari zaidi ya 570 na zaidi ya taasisi za habari 120.
  Katika kipindi hiki, TMF imehusika na kuunga mkono jitihada za wadau wengine wa habari na asasi za kiraia katika kukuza uhuru wa habari. Mtandao wa TMF umevuka jiji la Dar es salaam na kufikia pembe zote za nchi na unawagusa viongozi waandamizi wa vyombo vya habari pamoja na waandishi waliopo maeneo yote ya nchi.   Uchambuzi wa TMF kuhusu taarifa mbalimbali zinazotolewa na vyombo vya habari unaonyesha kwamba habari ambazo zimefadhiliwa na TMF zimegusa masuala ya vijijini kwa kiwango kikubwa. Asilimia 82 ya misaada ya TMF uelekezwa ukilinganisha na asilimia 25 iliyoelekezwa kwenye habari za mijini. 

Vilevile uchambuzi umeonyesha kwamba taarifa zilizofadhiliwa na TMF huwa na ubora wa hali ya juu ukilinganisha na taarifa za kawaida zinazoandikwa au kutangazwa na vyombo vya habari nchini. Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa TMF, maadhimisho hayo pia yatatumika kuzindua Tanzania Media Foundation, taasisi mpya ambayo itachukua nafasi ya Tanzania Media Fund ambao ni mradi ulioanzishwa na wafadhili. 

 “TMF mpya itakuwa ni mpango ulioanzishwa na Watanzania na kufanya kazi katika misingi ile ile kama mradi wa TMF lakini itaelekeza nguvu zaidi katika kuhakikisha yanakuwepo mazingira endelevu kwa ajili ya ukuaji wa TMF pamoja na wanahabari wanaosaidiwa na TMF. 

Tutaanzisha upya mpango wa kuwezesha upatikanaji wa habari ambazo zina maslahi makubwa ya taifa. Tutafanya kazi na wazalishaji vipindi ili kuongeza habari za ndani ili kuvisaidia vituo vya televisheni kutimiza wajibu wa kisheria kama ilivyoagizwa na TCRA ya kuwa na vipindi asilimia 60 vinavyohusu masuala ya ndani.

 Tunataka kuhakikisha vituo vya habari vinatoa habari za kukidhi mahitaji mbalimbali.” "Tanzania Media Foundation itaanza kazi kwa kukutana na wadau mbalimbali wa habari nchi nzima na itafanya nao kazi ili kutambua habari ambazo zitaleta mabadiliko chanya katika jamii.”

No comments: