Friday, September 11, 2015

MAFANIKIO SIYO AJALI SEHEMU YA KWANZA.

WATU wengi wanafikiri mafanikio ni kitu ambacho kinatokea tuu kama ajali lakini mafanikio sio ajali wala sio bahati mafanikio ni mipango dhahiri ambayo inapangwa na mtu anayeyataka na ayenuia kutoka katika vilindi vya moyoni mwake kwamba anataka kutoka katika sehemu moja kwenye maisha ambayo inakuwa ni duni na kwenda sehemu nyingine ambayo ni ya hadhi nzuri.

Wengi wamekuwa wakijidanganya kwamba ipo siku moja watafanikiwa (watatoboa)lakini hawana mpango wowote wa kuwawezesha kufanikiwa katika iyo siku moja na nataka niwaambie kwamba iyo siku moja haitakaa itokee kama hauna mpango dhahiri wa kupata unachokitaka katika maisha yako.

Unatakiwa kuwa na picha halisi ya kitu unachokitaka kwanza ndipo uende ukakitafute, kumbuka kumiliki kunaanzia kwenye akili kwanza acha kusema nahitaji nyumba nzuri,gari zuri,biashara nzuri, wakati hujapata picha halisi katika akili yako kile unachokihitaji unataka kiweje. Vijana wengi wamekuwa wakimaliza chuo Kikuu na kusema nipo tayari kufanya chochote huu ni ujinga na kutokuwa na maono hivi kweli kama upo tayari kufanya chochote nkikuambia ukachimbe vyoo utachimba? Be definate (unataka nini kwanza) na hicho unachokitaka hakikisha una picha yake kwenye akili yako jinsi kitakavyokuwa ndipo unaanza jitihada zote zitakazokupelekea kupata kile unachohitaji.

Jambo hili limekuwa likisumbua watu wengi sana la kukosa  picha halisi ya kile wanaachokihitaji na hivyo wamejikuta wakifanya vitu ambavyo hawavihitaji zikiwemo kazi wanazozifanya na kadhalika. Na hii pia ni mpaka kwenye kuoa/kuolewa kuwa na picha halisi ya mtu unaemtaka na sifa zake unataka aweje ndipo unapomuomba Mwenyezi Mungu sasa wewe unatafuta bila kujua unachokitafuta unataka kiweje? Weka hili katika akili yako litakusaidia sana.

Pindi utakapopata picha halisi ya kile unachokihitaji jicho lako lisiangalie nyuma, achana na hao marafiki wanaokuambia haiwezekani, maadamu akili yako imeweza kuwa na picha ya hiko kitu inamaanisha unao uwezo wa kukimiliki, watu wengi wameacha kufuata ndoto zao kwa kusikiliza maoni ya watu wengine ambao wamewakatisha tamaa na wakaacha kufanya kile walichokuwa wanataka kufanya.Hili naomba lisitokee kwako kabisa hakuna anaejua kile ambacho una uwezo wa kukifanya hata mzazi wako hajui unao uwezo mkubwa sana wa kufanya mambo makubwa na ya ajabu ni kiasi cha wewe kujiamini na kutenda tuu.

Anza kupambana fanya juhudi zote zitakazokupelekea kupata kile ulichonacho katika akili yako kama ni kuna masomo ya ziada inakubidi ukasome hakikisha unasoma hayo masomo, kama kuna watu fulani unatakiwa uwaone hakikisha unawaona hao watu kwa sababu siri ni hii huwezi kufanikiwa katika maisha haya pasipo msaada wa watu/mtu fulani, niliwahi kusema hivi na ninasema tena leo kwa mara nyingine achana na huu msemo nitafanikiwa mwenyewe (natoboa )itakuchukua muda mrefu na pia utatumia nguvu nyingi sana. 

Ili kufanikiwa inakubidi SAA zingine utafute waliofanikiwa wakushike mkono. Mfano hebu jenga taswira kwenye akili yako kuna watu wawili wote wamekaa chini kwenye sakafu ninachotaka hapa ni kwamba mmoja amuinue mwingine aliekaa nae kwa kumvuta mkono,Je hilo zoezi litawezekana wakati wote wamekaa chini? 

Bila shaka haliwezekani kadhalika na kwenye mafanikio huwezi ukainuliwa na mtu ambaye yupo sawa kiuwezo wa kufikiri,kiutendaji,na kiuchumi kama wewe tafuta aliekuzidi katika nyanja hizo au ambaye anaweza kukushauri,au ambaye tayari kashasimama ndipo atakapokunyooshea mkono na kukuvuta kisha utainuka.

IMEANDALIWA NA HUMPHREY MAKUNDI NA ALLARD MINJA

No comments: