ASILIMIA 46 ya wananchi wameripoti kuwa sera ndio kigezo muhimu watakachokitumia kumchagua Rais. Vigezo vingine vilivyotajwa na wananchi wengi ni uadilifu na maadili (17%). Hakuna mtu hata mmoja aliyetaja dini au utajiri kama kigezo muhimu cha kumchagua Rais na kigezo cha umri kilitajwa na asilimia moja tu ya wananchi.
Matokeo haya yametolewa na Twaweza kwenye muhtasari wa utafiti wenye jina la Je, Wanajua? Takwimu kuhusu uelewa wa wapiga kura. Muhtasari umetokana na Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaofanyika mara kwa mara kwa njia ya simu za mkononi. Matokeo yametokana na takwimu zilizokusanywa kwa wahojiwa 1,335 kutoka Tanzania Bara (Zanzibar haikuhusishwa) kati ya tarehe 12 na 26 mwezi Juni 2015.
Aidha, wananchi wanaamini kuwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 utakuwa huru na wa haki - asilimia 82 wanaamini kwamba maamuzi yao yataheshimiwa. Hata hivyo, asilimia 18 wanafikiri kuwa viongozi walio madarakani watavunja sheria ili washinde.
Asilimia 65 ya wananchi wanaamini kwamba mgombea mwenye sera nzuri atamshinda yule mwenye pesa nyingi.
Katika suala la vyombo vya habari, asilimia 76 ya wananchi wanaamini kwamba vyombo hivyo vitaripoti kwa usahihi masuala yanayohusu uchaguzi mkuu, wakati asilimia 24 wanafikiri kuwa vyombo vya habari vitakuwa na upendeleo kwa sababu ya motisha ya fedha.
Pamoja na matumaini haya, wananchi wana wasiwasi kuhusu uwezekano wa machafuko na vurugu wakati wa uchaguzi mkuu. Hili ni jambo linalowatia shaka asilimia 54 ya wananchi (Twaweza haikukusanya takwimu kuhusu nani anaweza kuwa chanzo cha vurugu hizo). Asilimia 18 walishawahi kushuhudia vurugu kwenye vituo vya kupigia kura wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa mwishoni mwa mwaka 2014 (Sauti za Wananchi, awamu ya 30, uliofanyika mwezi Februari-Machi 2015).
Wananchi wanafahamu sheria muhimu zinazosimamia mwenendo wa vyama vya siasa wakati wa kampeni. Asilimia 75 ya wananchi wanafahamu kwamba wagombea hawaruhusiwi kugawa fedha kwa wapiga kura ili wawachague. Na asilimia 79 wanaelewa kwamba wagombea hawaruhusiwi kutoa vyakula na vinywaji katika mikutano ya kampeni. Hata hivyo, asilimia 60 ya wananchi hawajui kuwa wagombea vinatakiwa kutunza kumbukumbu za fedha na michango walizopokea na jinsi zilivyotumika.
Pia, asilimia 62 wananchi wanaijua Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kupitia kazi zinazofanywa na tume hiyo. Hata hivyo, asilimia 51 wanaamini NEC ina uwezo wa kusimamia uchaguzi huru na wa haki mwaka 2015. Vile vile walipoulizwa kuhusu vipengele mahususi vya utendaji wa NEC kwenye uchaguzi wa mwaka 2010, nusu ya wananchi waliridhishwa na utoaji elimu kwa wapiga kura (49%), usahihi wa matokeo (54%) na mwenendo wa wafanyakazi wa tume (52%).
Aidan Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza alisema "Kuna mengi ya kufurahia kuhusu uelewa wa wananchi juu ya wajibu wao wa kiraia kama wapiga kura. Kwanza, ni dhahiri kabisa kwamba Watanzania wanalenga sera zaidi kuliko haiba ya wagombea. Pili, wananchi wana matumaini kuwa uchaguzi utafanyika katika hali ya uhuru na haki, ingawa wana wasiwasi kwamba vurugu inaweza kutokea. Tatu, ni jambo la kufurahisha zaidi kuona wananchi wakifahamu kuwa kupewa fedha, chakula au vinywaji ili wamchague mgombea ni kosa.
Ujumbe unaotolewa hapa kwa wagombea ni kwamba, ni lazima wajenge hoja kwa wapiga kura zinazolenga kuboresha huduma za jamii, badala ya kujikita kwenye tabia za watu binafsi. Wananchi wanataka mijadala makini kuhusu sera mbadala, ili waweze kufanya maamuzi sahihi kati ya sera hizo zinazoshindana. Hii ni changamoto mpya na inayotia hamasa kwa kila mtu –wagombea, waandishi wa habari na wananchi wenyewe kama wapiga kura."
No comments:
Post a Comment