Wednesday, September 30, 2015

IGP MANGU AHIMIZA UCHAGUZI WA AMANI TARIME.

 Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Ernest Mangu akisalimiana na Maofisa wa Polisi katika Kanda Maalumu ya Tarime na Rorya jana wakati alipokuwa katika ziara ya kikazi katika mkoa huo wa Kipolisi.Kushoto ni Kamanda wa Polis Kanda Maalumu Tarime na Rorya, Lazaro Mambosasa.
 Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Ernest Mangu akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Hosteli ya Polisi Kanda Maalumu ya Tarime na Rorya jana wakati alipokuwa katika ziara ya kikazi katika mkoa huo wa Kipolisi.
 Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Ernest Mangu akizindua Hosteli ya Polisi katika mkoa wa Kipolis Kanda Maalumu ya Tarime na Rorya jana wakati alipokuwa katika ziara ya kikazi katika mkoa huo wa Kipolisi
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Ernest Mangu akizungumza na wadau wa Polisi (hawapo pichani) wakati alipokuwa  katika ziara ya kikazi mkoa wa Kipolisi Tarime na Rorya ambapo alitumia kikao hicho kuwaasa kufanya uchaguzi kwa amani na utulivu.(Picha na Frank Geofray-Jeshi la Polisi)

Na Frank Geofray-Jeshi la Polisi, Tarime.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Ernest Mangu amewataka Viongozi wa Vyama vya Siasa katika Wilaya za Tarime na Rorya kufanya Kampeni za Kistaarabu ili kufanikisha Uchaguzi Mkuu pamoja na kuimarisha Amani na Usalama Wilayani humo.
IGP Mangu aliyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na Wadau wa Polisi wakiwemo Viongozi mbalimbali, Vyama vya Siasa pamoja na Wagombea wa Viti vya Ubunge na Udiwani, wakati alipokuwa katika Ziara ya Kikazi katika Kanda Maaalum ya Polisi Tarime na Rorya.

Alisema ili uchaguzi wa mwaka huu uweze kufanyika kwa amani, Viongozi wa Vyama vya Siasa na Wagombea hawana budi kuwashawishi wafuasi wao kufuata Maadili ya Uchaguzi ikiwemo kutotoleana lugha za Matusi.

IGP Mangu alisema baada ya Uchaguzi maisha yataendelea kama kawaida hilo ni jukumu la Wananchi wote wa Tarime kuondoa Uhasama wao katika mambo ya Siasa kwa kuwa Siasa siyo Uhasama.

Aidha, aliwashauri Wagombea Ubunge na Udiwani katika Majimbo ya Tarime Mjini, Vijijini, na Rorya kukutana mara kwa mara ili kujenga kuaminiana na kutatua changamoto zinazojitokeza katika kipindi hiki cha kampeni na hatimaye siku ya uchaguzi Mkuu.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Polisi Tarime na Rorya, kamishna Msaidizi wa Polisi, ACP Lazaro Mambosasa, aliwahakikishia Wadau wote kuwa Jeshi la Polisi limejipanga vyema kukabiliana na vitendo vyote vya vurugu vitakavyojitokeza, pamoja na kuhakikisha kila Mwananchi aliyejiandikisha anapata fursa ya kupiga kura bila vitisho vya aina yoyote.

Naye Mgombea Ubunge katika Jimbo la Rorya kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi, Lameck Airo alisema katika jimbo analogombea hakuna vurugu kwa kuwa wamekuwa wakiheshimiana katika Kampeni ili kuepusha vurugu kwa Wagombea na Wafuasi wao.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wakiwemo Viongozi wa Dini,Vyama vya Siasa, Wafanyabiashara, Asasi zisizo za Kiserikali, Wazee wa Kimila pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Tarime.

No comments: