Thursday, September 24, 2015

CCM WAKUBALI MDAHARO WA WAGOMBEA URAIS JIJINI DAR LEO

 Mjumbe wa Halmashauli Kuu ya Taifa na Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya (CCM) January Makamba akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani juu ya kufanya mambo mapya  yenye tija ambayo hayajawahi kufanyika ikiwemo mdahalo wa wagombea Urais ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaaam katika ofisi ndogo za Chama cha Mapinduzi CCM.
Wanahabari wakimsikilaza Mjumbe wa Halmashauli Kuu ya Taifa na ni Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya (CCM) January Makamba leo katika Ofisi ndogo ya chama cha mapinduzi  jijini Dar es Salam.
(Picha na Emmanuel Mssaka)





TAARIFA KWA UMMA

Chama cha Mapinduzi kinapenda kutoa taarifa kuhusu masuala kadhaa.
Mwenendo wa Kampeni
Kwa kifupi, Mgombea Urais, Ndugu John Pombe Magufuli na Mgombea-Mwenza Ndugu Samia Suluhu Hassan, wanaendelea vizuri na kampeni. Kila mmoja anafanya mikutano na wananchi kati ya 8 hadi 11 kwa siku na kukutana na maelfu kwa maelfu ya wananchi. Tunawashukuru wananchi wanaokuja kwenye mikutano yetu. Tunawashukuru pia makada wa CCM wanaojitolea kwa hali na mali kukipigania Chama cha Mapinduzi na kumtafutia kura Ndugu Magufuli.
Tunaridhika sana na mwenendo wa kampeni yetu. Katika nusu hii ya pili ya kampeni tutaongeza kasi na msukumo wa kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa mbinu na mikakati mipya.
Midahalo ya Wagombea
Tumeshangazwa na kauli ya Ndugu Kajubi Mukajanga, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania kwamba CCM haijathibitisha kushiriki mdahalo. CCM ilipokea mwaliko wa MCT na kuijibu kwa barua ya tarehe 13 Septemba 2015 yenye kumbukumbu CMM/OND/M/190/132 iliyosainiwa na Ndugu Stephen Msami, Msaidizi wa Katibu Mkuu. Barua hiyo ilipelekwa na kupokelewa kwa dispatch ambayo nakala yake tunayo. Baada ya hapo, Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Abdulrahman Kinana, alifanya kikao na wawakilishi wa MCT katika Ofisi Ndogo ya CCM Lumumba ili kutaka kujua zaidi na kutoa maoni ya CCM kuhusu utaratibu mzima wa mdahalo. Katika kikao hicho, ambapo MCT iliwakilishwa na Afisa wake, Ndugu Allan Lawa, pamoja na Ndugu Tido Mhando, CCM ilithibitisha tena kushiriki mdahalo. Tatu, tarehe 16 Septemba 2015, CCM ilitoa kauli rasmi, iliyosainiwa, ikithibitisha kushiriki mdahalo. Kauli ya Ndugu Mukajanga inalenga kuwasaidia kisiasa wale ambao hawajathibitisha au hawana nia ya kuthibitisha kushiriki. Kwa msingi huu, tunaamini ni vyema mdahalo huu ukaandaliwa na ushirika wa taasisi mbalimbali zilizokuwa na nia ya kuandaa midahalo, (kama vile CEO Roundtable, UDASA, Twaweza) ili kuiondolea uwezo taasisi moja, au kikundi cha watu wachache, kuhodhi na kuwa na ukiritimba kwenye jambo hili kubwa na muhimu.
CCM inapenda kusisitiza yafuatayo:
1. Ndugu Magufuli amekubali kushiriki mdahalo wa wagombea Urais
2. Mdahalo uwashirikishe wagombea wenyewe na sio wawakilishi wao.
3. Wagombea wote, hasa wa vyama vikuu, wawepo na washiriki.
Tunapozungumzia mabadiliko katika nchi maana yake ni utayari wa kufanya mambo mapya yenye tija ambayo hayajawahi kufanyika, ikiwemo mdahalo wa wagombea Urais. Wanaohubiri mabadiliko huku wakiogopa kushiriki mdahalo wanahubiri mabadiliko hewa.
Utafiti wa TWAWEZA
CCM haikushangazwa na matokeo ya utafiti wa taasisi huru ya Twaweza yaliyotangazwa jana ambayo yanatoa ushindi wa asilimia 65 kwa Ndugu John Pombe Magufuli dhidi ya asilimia 25 za Mgombea wa UKAWA. Hatukushangazwa na matokeo ya utafiti huu kwasababu tano:
1. Siku UKAWA walipomteua Ndugu Edward Lowassa kuwa mgombea wao ndio siku CCM ilipohakikishiwa ushindi katika uchaguzi wa mwaka huu. CCM hatukumteua kwasababu tuliamini hakuna namna ambapo Watanzania wengi watamchagua.
2. Katika uchaguzi wa mwaka huu CCM tunafanya utafiti wetu wa ndani wa kisanyansi kila wiki kujua mwenendo na mwelekeo wa kampeni na maeneo yanayohitaji nguvu mahsusi. Tangu tuanze utafiti wetu mwishoni mwa mwezi Agosti, karibu kila wiki asilimia za ushindi wa CCM hazijawahi kushuka chini ya asilimia 60 na zimekuwa zinapanda.
3. Kazi kubwa anayofanya mgombea wetu, Ndugu John Pombe Magufuli, na mgombea-mwenza, Ndugu Samia Suluhu Hassan, kuzunguka nchi nzima kwa barabara na kuongea moja kwa moja na wapiga kura inazaa matunda. Wanawafikia wapiga kura wengi, hasa wa vijijini, na wapiga kura hao wanawaelewa.
4. Kampeni kubwa zinazofanywa na wagombea Ubunge na Udiwani wa CCM na makada na viongozi wa Chama katika ngazi zote nchi nzima kila siku kumuombea kura Magufuli nazo zinazaa matunda.
5. Tunaamini pia migogoro ndani ya UKAWA katika kipindi hiki cha uchaguzi iliyopelekea mitafaruku katika kuachiana majimbo na, baadaye, kutokana na uteuzi wa Mgombea Urais wa UKAWA, kupelekea kujiuzulu kwa viongozi wa muda mrefu na maarufu wa UKAWA, Profesa Ibrahim Lipumba na Dr. Wilbrod Slaa, na migongano ndani ya NCCR-Mageuzi, yote haya yamepunguza imani ya wananchi kuhusu uwezo wa vyama hivi kushika dola.
Lakini vilevile matokeo ya utafiti huu ni ishara kwamba Watanzania wamempokea na kumuelewa Ndugu Magufuli na wako tayari kumkabidhi nchi.
Sisi kama CCM kuna baadhi ya mambo tumeyachukua katika utafiti huu na tutayafanyia kazi ili kujihakikishia ushindi.
Tumeshangazwa na taharuki, hasa kutoka miongoni mwa wasomi na wanaharakati, kuhusu matokeo ya utafiti huu. CCM ilitegemea kwamba jamii ya wasomi na wanaharakati ingefurahia utamaduni wa tafiti za kisiasa unaoanza kujitokeza hapa nchini ili siku zijazo tujikite katika kurekebishana kwenye kanuni za utafiti na ithibati na uhakiki wa ubora. Tunasikitika kwamba yanawekwa mazingira ya kutisha na kukatisha tamaa (atmosphere of intimidation) kwa watu wanaotaka kufanya tafiti za kisiasa nchini.
Utafiti ni sayansi. Matokeo ya utafiti hupingwa kwa matokeo ya utafiti mwingine, sio kwa kuponda tu au kwa matusi na vitisho. Ni vyema tukajifunza kupokea habari mbaya bila taharuki.
Itakumbukwa kwamba, mwezi Agosti 2010, taasisi ya utafiti ya kimataifa ya Synovate ilitoa utafiti ikionyesha kwamba CCM itashinda Uchaguzi Mkuu wa 2010 kwa asilimia 61. Baadhi ya wana-CCM hawakufurahishwa na matokeo ya utafiiti huo kwasababu waliamini kwamba ushindi wetu ulikuwa ni mkubwa zaidi. Wapinzani waliwalaani, kuwatukana na hata kutaka kuwashtaki Synovate. Kwenye matokeo halisi ya kura, CCM ilipata asilimia zilezile 61 zilizotabiriwa na Synovate.
Ni vyema kuweka akiba ya maneno kwenye masuala haya.
Imetolewa na:
January Makamba
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa
Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM
23.09.2015

BONYEZA HAPA KUSOMA ILANI YA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)

      

CHAMA CHA MAPINDUZI
Sanduku La Posta: 50047
Dar Es Salaam, Tanzania

You received this email as part of our network.

No comments: