Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe Dkt.Martin Msokela akiongea na watumishi wa hospitali ya wilaya ya Kisarawe kabla ya kupokea msaada wa mashuka ya wagonjwa wilayani humo leo. Mashuka hayo yametolewa na chuo cha Elimu ya Biashara Dar es Salaam (CBE).
Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam(CBE) Prof.Emanuel Mjema(kushoto) akikabidhi msaada wa shuka 176 kwa Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe Dkt.Martin Msokela (kulia) leo. Mashuka hayo yametolewa na chuo hicho kusaidia wodi ya Wazazi ya Hospitali hiyo iliyokuwa ikikabiliwa na uhaba wa mashuka.
Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam(CBE) Prof.Emanuel Mjema(katikati), Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya wilaya ya Kisarawe Dkt.Martin Msokelo(kulia) na Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Mohamed Mzige kwa pamoja wakitandika sehemu ya msaada wa mashuka 176 yaliyotolewa na CBE kwenye wodi ya Wazazi ya hospitali hiyo.
Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam(CBE) Prof.Emanuel Mjema(wa pili kushoto), Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya wilaya ya Kisarawe Dkt.Martin Msokelo(kushoto ) na Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Mohamed Mzige (kulia) na baadhi ya watumishi wa hospitali ya Kisarawe wakielekea lilipo jengo la wodi ya wazazi.
Wauguzi wa Hospitali ya wilaya ya Kisarawe wakifurahia msaada wa mashuka yaliyotolewa kwa wagonjwa na Chuo cha Elimu ya Biashara, CBE leo.
Picha/Aron Msigwa - MAELEZO.
TAASISI, MASHIRIKA NA MAKAMPUNI YAASWA KUTUMIA SEHEMU YA FAIDA WANAYOPATA KUSAIDIA HUDUMA ZA AFYA.
Aron Msigwa -MAELEZO.
26/9/2015. Kisarawe,PWANI.
Wito
umetolewa kwa Taasisi, mashirika na makampuni kote nchini kujenga
utamaduni wa kutumia sehemu ya faida wanayoipata katika kuisaidia jamii
kupitia sekta ya afya ambayo inakabiliwa na changamoto mbalimbali.
Wito
huo umetolewa leo mjini Kisarawe na Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara
Dar es salaam Prof.Emanueli Mjema wakati akikabidhi msaada wa shuka 176
zilizotolewa na chuo hicho kusaidia wodi ya Wazazi ya Hospitali ya
wilaya ya Kisarawe, mkoani Pwani.
Amesema CBE
mwaka huu imetimiza miaka 50 toka kuanzishwa kwake mwaka 1965, hivyo
ukongwe na umri wake nchini Tanzania umekua ukiendana na mabadiliko ya
kiuchumi yanayotokea ndani na nje ya nchi ili kukidhi mahitaji na
matarajio ya watanzania.
"CBE tukiwa chuo
kikongwe nchini tumefanya mengi yenye manufaa kwa uchumi wa nchi yetu na
jamii ya watanzania,kwa kuwathamini wananchi tunaowahudumia tuna
utaratibu wa kurudisha sehemu ya faida tunayoipata kwa jamii na mwaka
huu tulitenga kiasi cha shilingi milioni 9 kusaidia wodi za wazazi
katika hospitali zetu" Amesisitiza.
Ameeleza
kuwa ndani ya miaka 50, CBE imewanufaisha wananchi na kutoa mchango
mkubwa katika maendeleo ya taifa kupitia Fani za Biashara, Ugavi na
manunuzi, Vipimo, TEHAMA , Utawala katika biashara pamoja na kutoa
huduma mbalimbali kwa jamii.
Amesisitiza
kuelekea miaka 50 ijayo chuo chake kimeelekeza nguvu katika kuwekeza
kwenye ubora na ujuzi wa kumuwezesha muhitimu kuitumia elimu aliyoipata
kuleta manufaa na mabadiliko katika jamii inayomzunguka.
“Sisi
kama chuo cha Elimu ya Biashara tumeona uhitaji uliopo nchini wa kukosa
wataalam wenye ujuzi wa Biashara ndio maana tumeanza kufuandisha
wanafunzi wa Shahada ya Elimu katika Biashara ili tupate wahitimu bora
watakaokidhi mahitaji ya soko” Amesisitiza.
Kwa
upande,Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya Dkt. Martin Msokela akizungumza mara
baada ya kupokea msaada huo kwa niaba ya Mkurugenzi wa wilaya hiyo,
ameushukuru uongozi wa CBE kwa kuwakumbuka wagonjwa wa Hospitali ya
wilaya ya Kisarawe.
Amesema msaada uliotolewa
na chuo hicho umepunguza uhitaji wa mashuka waliokuwa nao kwani
Hospitali hiyo inakabiliwa na tatizo la uhaba wa mashuka kwenye vitanda
vya wagonjwa.
Dkt.Msokela amewaomba wadau
wengine kujitokeza kwa wingi kuisaidia hositali hiyo kama walivyofanya
CBE ili kuboresha afya za wagonjwa wanaofika hospitalini hapo kutibiwa.
"
Nawaomba wadau wengine wajitokeze kusaidia kama walivyofanya CBE, licha
ya hili la mashuka ukiangalia Jiografia ya Kisarawe,Hospitali yetu
imekua na tatizo la upatikanaji wa maji na uchakavu wa mitambo"
Amebainisha.
Aidha katika hatua nyingine
Dkt.Msekela ameeleza kuwa hali ya ugonjwa wa Kipindupindu wilayani humo
inaendelea kudhibitiwa kupitia timu ya wataalam iliyoundwa kukabiliana
na tatizo hilo na kuongeza kuwa hospitali hiyo imepokea mgonjwa mmoja
mwenye tatizo hilo.
No comments:
Post a Comment