Monday, August 17, 2015

NYAMAGANA DC AFUNGUA AIRTEL RISING STARS MWANZA

 Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Baraka Konisaga akikagua timu wakati wa uzinduzi wa Airtel Rising Stars mkoa wa Mwanza jana.
 Mkuu wa wilaya ya Nyamagana Baraka Konisaga akiongea wakati wa uzinduzi wa Airtel Rising Stars mkoa wa Mwanza jana.

MKUU wa Wilaya ya Nyamagana Baraka Konisaga jana Jumapili (Agosti 15) alifungua mashindano ya Airtel Rising Stars mkoa wa Mwanza na kuwambia vijana kuwa wanalo jukumu la kubadilisha matokeo ya timu za Tanzania hasa katika mashindano ya kimataifa ambapo Tanzania imekuwa haifanyi vizuri.

Akifungua mashindano ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Airtel Rising Stars katika mkoa wa Mwanza, Konisaga alisema anaamini kuwa mkoa wa Mwanza umejaliwa kuwa na wachezaji wenye vipaji vya soka na ndio maana mwaka juzi uliibuka bingwa wa Airtel Rising Stars kwa upande wa wavulana. Amekitaka chama cha soka mkoa wa Mwanza (MZFA) kutumia mashindano ya Airtel Rising Stars kubaina wachezaji wazuri na kuwaendeleza.

Mkoa wa Mwanza ulivuma sana miaka ya themanini kupitia timu ya Pamba ambayo wachezaji wake kama vile Joram Mwakatika, Madata Lubigisa, John Mhina, Beya Simba, Raphael Paul na wengine wengi walikuwa moto wa kuotea mbali.

Mheshimiwa Konisaga ameipongeza kampuni ya simu za mkononi ya Airtel kwa kuona umuhimu wa kuwekeza sehemu ya raslimali yao kwenye maendeleo ya mchezo wa soka kwa vijana. “Mashindano ya Airtel Rising Stars ni fursa nzuri. Ni vema timu mbalimbali za soka zikayatumia kupata vijana wenye vipaji na kuwaendeleza”, alisema.

Alisema mbali ya kuwa jukwaa la kutumia kubaini wachezaji wenye vipaji, Airtel Rising Stars pia yanawahamasisha vijana kushiriki mazoezi hivyo kuwa na afya njema na kuhudhuria darasani kama kawaida.

Konisaga aliwaambia vijana kwamba kwa dunia ya leo mpira ni chanzo cha ajira ya kutumainiwa kwa mamilioni ya vijana ambao wanaishi maisha mazuri kwa kuwa wanalipwa mishahara mizuri.

Aliwataka viongozi wa chama cha soka mkoa wa Mwanza kuchagua wachezaji wenye vipaji kuunda kombaini ya mkoa itakayoshiriki kwenye fainali za Taifa za Airtel Rising Stars jijini Dar es Salaam ambazo zinatarajia kuanza mwezi ujao.

Naye mwenyekiti wa kamati ya soka la vijana (TFF) Ayoub Nyenzi aliwataka viongozi wa soka kuzingatia kanuni za mashindano hayo has suala la umri.  Mwenyekiti wa MZFA Jackson Songora amejinasibu kwamba mkoa wake una vijana wenye vipaji ambao bila shaka watatwaa ubingwa wa taifa mwaka huu.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Ofisa Masoka wa Airtel Tanzania Mkoa wa Mwanza Emmanuel Raphael amewashukuru wadau wote wa soka kwa kuyaunga mkono mashindano ya Airtel Rising Stars na kuyapa umuhimu yanaostahili.

No comments: