KISAKALE CHA BIBI NYAMIHEMBE WA WAZARAMO NI CHIMBUKO LA UTANI WA WAZARAMO NA WANYAMWEZI.
Benjamin Sawe-WHVUM
HADITHI moja ya ajabu inayosimuliwa na wazee wa kizaramo ni ile ya Nyamihembe aliyolewa Unyamwezi,msimulizi mmoja alisema haikuwa Hadithi ya kweli, nayo ni hii, ( Hii ni Tanzu ya Fasihi simulizi)
Mzee mmoja wa Kizaramo alikuwa na binti mzuri aliyeitwa Nyamihembe, mtoto wa kiti cha kwanza,(Mtoto wa kiti ni mwana Nyang’iti, ni utambulisho wa Mila na Desturi za baadhi ya Makabila ya Pwani, hutumika katika shuhuri zote za kimila za kurithisha vijana katika kundi la utu uzima) Baada ya kuvunja ungo akatokea Mnyamwezi mmoja akamposa, na kufunga pamvu(Harusi), kisha akapewa Bibi huyo akaishi naye.
Lakini Yule Mnyamwezi baadae alipendelea kurudi kwao unyamwezi pamoja na mke yule, basi akataka idhini kwa wazazi akakubaliwa,akaondoka Uzaramo na mkewe hadi kwao Unyamwezini.
Walipokuwa kule wakajaaliwa watoto wengi wa kiume na wakike, waliishi kule Unyamwezi kwa miaka mingi hadi wale watoto wakawa watu wazima, wakaoa na kuolewa, wakazaa watoto kadha wa kadha waliokua wajukuu wa Nyamihembe.
Lakini watoto na wajukuu wa
Nyamihembe hawakupata bahati ya kufika Uzaramo tangu kuzaliwa kwao ila kila mara bibi Nyamihembe alikuwa akiwasimulia habari za Uzaramo kama hadithi tu.
Nyamihembe aliishi kule hata akawa mzee (ajuza), maana hata wale wajukuu walizaa kisha wakajukuu, akawa na virembwe kadha wa kadha,wakati ule yule Mzazi mwezake Mnyamwezi Uzee ulimkithiri akafariki Dunia.
Nyamihembe akawa anatunzwa na wanawe na wajukuze, nae kila mara aliwausia akisema, ‘mimi nikifa msinizike hapa, mnipeleke kwetu Uzaramo mkanizike huko’.
Mwanamke huyo aliishi kwa miaka mingi hata wale wanae wengine wakafariki dunia, yeye akabaki kama Mzimu, macho yake yalikwisha nguvu ya kuona akawa kipofu, nyama za mwili zikamkauka akabakiwa na mifupa na ngozi ikakunjana kunjana, hakujimudu kutembea, mvi zake zikapukutika zote, akabaki na Upara.
Ajabu nyingine iliyotokea mwilini mwake ziliota Pembe mbili zilizotokeza katika paji la uso, baada pembe hizo zikakua zikawa ndefu zilizo inama chini, Umbo alilokua nalo liliwaogofya watu, ila wale wajukuu zake ndio waliokuwa wakimuhudumia, maana ilibidi kila asubuhi kumuinua na kumtoa nje aote jua na jioni ni kumrejesha ndani na kumlaza kitandani.
Alipokuwa anakalishwa chini zile pembe zilikuwa zinagusa ardhi na kujichomeka kama mikuki,wajukuu walipata taabu sana kwa kumtunza ajuza huyo,baadaye mauti yalimkuta na kumuondolea taabu zake.
Nyamihembe akaifariki Dunia.
Basi, walipokuwa wakitangaza tanzia na kutayarisha mambo ya mazishi wale wajukuu hawakujali ule usia wake aliousia kwamba akifa akazikwe kwao Uzaramo,waliona nijambo lisilowezekana, maana kutoka Unyamwezi mpaka Uzaramo ni mwendo wa miezi miwili.
Basi wakatayarisha mahali pa kuoshea maiti lakini walipojaribu kumuinua mfu yule wakashindwa kabisa kwa maana alikuwa mzito sana wala hawakumudu kumjongeza hata kidogo, walifanya bidii kwa nguvu zao zote wake kwa waume wakashindwa wakashangazwa na muujiza ule.
Lakini baadae kidogo mjukuu mmoja alikumbuka usia na wimbo aliofundishwa na Bibi yake wakati wa uhai, maana mara mbili tatu Nyamihembe alimfundisha wimbo Mjukuu wake akamuhusia kuwa atakapokufa wanaomzika waimbe wimbo huo, naye atawaongoza njia ya kwendea Uzaramo katika nchi aliyozaliwa akazikwe huko.
(Umuhimu wa kujiandikia Tarijima).
Basi Yule mjukuu akawaeleza habari ile watu waliokuwapo nao wakanena, ‘Natujaribu kuimba wimbo huo na tutazame matokeo yake yatakuaje! lakini wengine wakasema, ‘pengine huenda Mfu akainuka kweli na kutuongoza njia ya kwenda kwao uzaramo, nasi wajibu wetu kumfuata, basi si bora kama tutatayarisha Chakula kwa matumizi yetu ya njiani kabla hatujaimba wimbo wenyewe’ kwa shauri hilo, wote wakakubaliana kutayarisha masurufu ya njiani.
Basi siku Ile wakalala bila kuigusa tena ile maiti, hata asubuhi yake kulipokucha tu wakakusanyika watu wengi waliokuwa na shauku ya kujua mazishi ya bibi Nyamihembe, yule mjukuu akawafundisha kiitikio cha Wimbo na yeye mwenyewe akaanza kuimba:
‘Nyamihembe tuhilike ukaye gwee!’
Nawenzake wakaitikia wimbo,
‘Tuhilike kumwetu Zaramo’
Na maana yake:’Ewe Nyamihembe tuongoze nyumbani!’
Na waitikiao husema:’ Tuongoze kwetu Uzaramo.’
Wimbo ule ulipoanza kuimbwa tu, ibra (ajabu) ikaanza tena kutokea, zile pembe zikaanza kunywea kidogo kidogo mpaka zikatoweka kabisa,kisha mwili wa Mfu ukaanza kutikisika, halafu mfu mwenyewe akasimama wima, watu wengine waliogopa wakaanza kukimbia lakini wale wajukuu na ndugu wengine walibaki pale wakiendelea kuimba ule wimbo.
Mara Nyamihembe naye akaimba :
‘Mowana silawile behi niye,
Silawile behi m-m-m,
Ndawa Zaramo’.
Na maana yake, ni (Tafsiri yake ‘Enyi watoto sikutoka karibu mimi, nimetoka Uzaramo.’) Nyamihembe alipokuwa akiimba hivyo mara akaanza kutembea kwa miguu yake kama kwamba mtu mzima mwenye nguvu.
Wajukuu na jamaa wengine wakamfuata, Msafara ukaanza pale kuelekea Uzaramo, ndugu wa marehemu, mume wa Nyamihembe waliuandama msafara huo,wengi wao walifuata ili kujua mwisho wa miujiza ile.
Lakini hakuna aliyesadiki kama mfu yule atawaongoza mpaka Uzaramo,basi Wimbo uliendelea kuimbwa na Nyamihembe aliendelea kuujibu Wimbo huo hali akiwa kiongozi wa msafara, alikuwa Kipofu, lakini ajabu kwamba alikuwa Kiongozi mwenye mwendo wa haraka bila kupotea njia.
Siku ile ya kwanza walisafiri mpaka Mchana upatao saa saba, kwa ghafla Nyamihembe akaanguka kando ya njia akajilaza kifudifudi akawa mfu tena,watu wakajua kuwa sasa ndio mwisho wa ajabu wa uhai wake, wakafanya shauri ya kumwinua ili wamchukue na kumrudisha nyumbani walikotoka ili wakamzike.
Lakini walipojaribu kumwinua, wakashindwa kabisa maana alikuwa ameambatana na ardhi wala hawakuweza kumjongeza, kwa kuwa wote walikuwa wamechoka kwa njaa wakatua pale na kupika vyakula vyao wakala.
Hata wakati wa alasiri, wakashauriana kuimba tena Wimbo ule labda Nyamihembe atainuka,basi walipoimba tu, Nyamihembe akasimama na kuimba wimbo wake mara akaongoza tena msafara,wakamfuata katika hali hiyohiyo ya kuimba mpaka jua lilipokuchwa Nyamihembe akaanguka kando ya njia akajilaza kifudifudi. Wafuasi nao walichoka kwa ule mwendo wa kutwa, basi wakafanya kambi mahali pale wakalala.
Asubuhi kulipokucha, wale waliofuata msafara kwa upelelezi wa kujua mwisho wa ajabu ile wakarejea makwao. Lakini Wajukuu wa Nyamihembe pamoja na ndugu wachache wa mume wa Bibi Nyamihembe waliendelea katika safari. Nyimbo zikaimbwa kama kawaida na Nyamihembe akaongoza msafara.
Mambo yaliendelea hivyo kama siku ya kwanza, nao walisafiri katika hali hiyo kwa muda wa Mwezi na nusu, hata safari ilipobaki mwendo wa siku tatu Nyamihembe hakufanya kituo tena wakati wa mchana isipokuwa alifululiza kusafiri na jioni akafanya kituo.
Asubuhi moja waliposafiri hata mnamo saa tatu hivi wakatokea katika Kijiji chenye nyumba nyingi pamoja, kwa ghafla Nyamihembe akajitupa katikati ya Uga, lakini badala ya kulala kifudifudi alilala chali.
Watu wa Kijiji kile walistaajabishwa sana kuona Kizee ajuza kikifuatwa na jeshi la watu, kisha kimejitupa uwanjani kwao wale waliokuja na Nyamihembe waliendelea kuimba ule wimbo, lakini Nyamihembe hakuinuka tena, akawa kama mfu wa kawaida, maana amekwisha fika nyumbani kwake Uzaramo.
Watu wa Kijiji wakakusanyika na kuwauliza habari wale wageni,wageni wakasimulia habari zote za Nyamihembe na jinsi hapo zamani alipopata kuolewa na Mnyamwezi, habari za wosia wake aliousia wakati alipokuwa hai na jinsi walivyo pata kuja naye mpaka pale.
Basi kutokana na maelezo yale, Wazee wengi wa Kijiji kile walikumbuka nasaba yake, wengine wakasema,’huyu ni Shangazi yetu,’ wengine wakasema,’ huyu ni Nyanya yetu’ mradi Kijiji kile kilijaa ukoo wote wa bibi Nyamihembe.
Baada ya hivyo wakaleta kitanda wakaichukua maiti bila ya taabu yoyote, wakailaza juu ya kitanda na kuipeleka ndani, na wengine wakashughulika kuwapokea wageni waliotoka Unyamwezi.
Siku ile watani wakaarifiwa na majirani wengine wakapelekewa Tanzia (Habari ya kifo inayopelekwa kutoka mbali) kuwa Nyamihembe Mwanamhembe alieishi Unyamwezi amerudi katika hali ya umauti na mazishi yake yatakuwa kesho,hapakuwa na kilio wakati ule, maana Nyamihembe alikuwa Tagala (mzee, kikongwe sana), mpaka Magharibi Bendebende (Ngoma ya kuashiria kifo cha mtu mkubwa) ikapigwa kuashilia kilio.
Wacheza Songwa na uzunguli (Ngoma zinazochezwa wakati wa maziko ya mtu mkubwa) wakahudhuria kama desturi hata Siku ya pili maandalizi ya mazishi yakafanyika, Nyamihembe akazikwa kwa heshima kubwa.
Makala haya yanatufundisha kwamba fahari ya mtu ni kwao, (Makala haya yana vionjo vyote vya kidiaspora, yanatukumbusha ugenini ni matembezi, kwako ni maskani),yameandikwa kwa ushirikiano wa Idara ya Utamaduni Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.
Fanani wa Hadithi ni Mwaruka Ramadhani (1965)
No comments:
Post a Comment