Friday, July 24, 2015

RAIS JAKAYA KIKWETE MGENI RASMI MAADHIMISHO YA KUMBUKUMBU YA MASHUJAA

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Saidi Meck Sadiki akizungumza na waandishi wa habari kuhusu sherehe za maadhimisho ya kumbukumbu ya Mashujaa zitakazofanyika kitaifa katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam.
Askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakiwa katika mazoezi katika viwanja vya Mnazi Mmoja leo jijini Dar es salaam ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mwisho ya sherehe za Kumbukumbu ya Mashujaa. Picha na Aron Msigwa - MAELEZO.

Na.Aron Msigwa - MAELEZO.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Jakaya Kikwete anatarajia kuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa itakayofanyika Julai 25, 2015  Katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam.

Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa maandalizi ya maadhimisho hayo leo jijini Dar es salaam,Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Meck Sadiki amesema maadhimisho hayo kitaifa yatafanyika jijini Dar es salaam kuwakumbuka na kuwaenzi mashujaa waliojitoa muhanga kupigania uhuru na ukombozi wa Taifa la Tanzania,kulinda na kudumisha amani na utulivu wa nchi.

Amesema Maadhimisho hayo yatapambwa na Gwaride la Kumbukumbu litakaloandaliwa na vikosi vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),Polisi ,Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Aidha, amesema  kutakuwa na  Mizinga salama itakayopigwa, uwekaji wa silaha za asili na maua kwenye mnara wa kumbukumbu, Kutakuwa na sala na Dua kutoka kwa viongozi wa Madhehebu mbalimbali ya dini hapa nchini.

Bw. Sadiki amefafanua kuwa shughuli zote katika viwanja vya Mnazi Mmoja zitaanza saa mbili Asubuhi na kumalizika saa sita mchana ambapo wananchi watakaohudhuria kumbukumbu hiyo watapata fursa ya kushuhudia matukio yatakayokuwa yananendelea uwanjani hapo kupitia Luninga kubwa zitakazokuwepo katika maeneo yote muhimu ya uwanja.
  
Ameongeza kuwa siku hiyo baadhi ya barabara katika jiji la Dar es Salaam zikiwemo  Lumumba ,Uhuru na Bibi Titi zitafungwa kwa muda ili kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara hizo watakaohudhuria maadhimisho hayo .

Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ametoa ufafanuzi kuhusu changamoto zinazoendelea kujitokeza za kusuasua kwa zoezi uandikishaji wa wananchi katika daftari la kudumu la wapiga kura katika mfumo wa BVR jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kushirikiana na Wakurugenzi wa Manispaa za jiji la Dar es Salaam wanaendelea kushughulikia matatizo mbalimbali yaliyojitokeza katika siku ya kwanza na ya pili katika baadhi ya vituo hususani baadhi ya mashine za BVR kushindwa kufanya kazi vizuri.

Akizungumzia baadhi ya malalamiko yanayotolewa na wananchi hasa tatizo la uchelewaji wa waandikishaji kufika katika vituo walivyopangiwa kwa wakati amesema kuwa Serikali ianaendelea kuchukua hatua ili kukomesha tabia hiyo.

Amewaagiza Wakurugenzi wa Manispaa zote za jiji la Dar es Salaam kuwachukulia hatua watumishi hao wazembe kwa kuwafuta kazi ili kuepusha madhara na vurugu zinazoweza kuepukika na uongeza kuwa kazi ya uandikishaji wananchi inatakiwa kuanza saa 2 asubuhi mpaka saa 12 jioni kila siku kwa tarehe zilizopangwa.

Kuhusu taarifa za uwepo wa baadhi ya watendaji kuwaingiza waandikishaji wasiohusika kusimamia zoezi hilo Mkuu wa Mkoa huo amewataka watendaji hao kuacha mara moja tabia hiyo ili kuepuka kuvuruga zoezi hilo na kwamba hatua kali za kisheria  zitachuliwa dhidi yao.

Pia amevitaka Vyama vya siasa kuacha kutumia mwanya huo kuweka bendera au kuvaa mavazi yanayoashiria kampeni za siasa ili kuepusha vurugu.

No comments: