Na Fredy Mgunda,iringa
MWENYEKITI wa Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), Leonce Marto amechukua fomu ya kuwania ubunge katika jimbo la Iringa kupitia chama chake hicho.
Amechukua fomu hiyo siku moja tu baada ya Rais Jakaya Kikwete kulihutubia na hatimaye kulivunja bunge la 10 la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo uhai wake utakoma Agosti 20, mwaka huu.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, jimbo la Iringa Mjini limekuwa likiongozwa na Mchungaji Peter Msigwa ambaye pia alichaguliwa kupitia Chadema katika uchaguzi wa 2010.
Kwa kupitia taarifa yake aliyoisambaza kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii jana, Marto alisema; “nawasalimu nyote wenye mapenzi mema na Taifa letu la Tanzania na wapenda mabadiliko na demokrasia za ushindani ndani ya vyama vya siasa kwa minajili ya katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 .”
“Nianze kwa kuwashukuru watu wote ambao kwa muda wa uhai wangu wameshiriki kwa namna moja ama nyingine kuniwezesha kufika hapa nilipo . Pili nawashukuru viongozi , wanachama , wafuasi wa Chadema, ndugu, jamaa na marafiki ambao kwa wingi wenu sitaweza kuwataja wote,” alisema.
Marto alisema ameamua kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Mchungaji Msigwa baada ya kupata msukumo wa ndani na nje ya chama.
Alisema kwa haraka katika fahamu zake aliona jambo hilo ni zito na la hatari kulinganisha na watu wanavyosema kwasababu kazi ya umma ni kazi inayohitaji dhamira safi, uadilifu, umahiri, weledi, kujali ya maisha ya watu na maendeleo yao na zaidi sana kupenda na kutathmini Taifa na watu wake.
Marto alisema ilimchukua muda kujiridhisha pasipo shaka na jambo hilo kama anaweza kubeba wito huo wa kuwatumikia wananchi wa Iringa Mjini.
“Baada ya kutafakari kwa kina nilijipa mtihani wa kwanza wa kuzunguka nchi yetu na kukutana na jamii za watanzania. Kwa mantiki hiyo ninayafahamu kwa undani na kwa uhalisia wake maswala na matatizo muhimu yanayowakabili watanzania na wana Iringa Mjini,”alisema.
Marto alisema kwa kuwa anakidhi vigezo vya kikatiba, na kwa kuwa anaamini Mungu amempa karama ya uongozi ambayo watu wameiona na kumuomba agombee ubunge na kwa kuwa anayajua matatizo yanayowakabili watanzania na wana Iringa anayajua na yamemchosha kama yalivyowachosha watanzania wengine:
Na kwa kuwa Chadema kimejengwa kwenye mhimili na msingi mkuu wa Demokrasia pamoja na itikadi na falsafa yake ya Nguvu ya Umma na kwa kuwa anaamini viongozi bora wanapatikana kwa ushindani, kwa ujasiri wote aliopewa na Mwenyezi Mungu anatangaza rasmi kuomba ridhaa ya chama chake kugombea ubunge katika jimbo hilo.
No comments:
Post a Comment