Homa ya michuano ya Kagame inazidi kupamba moto kufuatia vilabu mbalimbali zinazoshirki michuano hiyo kuanza kuwasili jijini Dar es salaam zikiwa na vikosi vyao kamili kwa lengo la kusaka Ubingwa wa michuano hiyo.
APR ya Rwanda tayari imeshawasili jijjini Dar es salaam, pamoja na timu za Al Shandy ya Sudan, KMKM ya Visiwani Znzibar, huku timu za Al Malakia ya Sudan Kusini na mabingwa mara tano wa michuano hiyo Gor Mahia wakitarajiwa kuwasili leo saa saa 10 jioni kwa ndege ya Kenya (KQ).
Kueleka mchezo wa ufunguzi kati ya Yanga dhidi ya Gor Mahia, wenyeji timu ya Yanga (watoto wa Jangwani) wameendelea kujifua katika uwanja wa Polisi Ufundi chini ya kocha wake mholanzi Hans Van der Pluijm na msaidizi wake Mkwasa kuhakikisha wanafanya vizuri katika mechi hiyo.
Gor Mahia ambayo inafundishwa na kocha Frank Nutal raia Skotilandi, inawasili ikiwa na kikosi chake cha kwanza kamili kilichocheza michezo 17 ya Ligi Kuu nchini Kenya bila kufungwa, ikishinda michezo minne na sare michezo mitatu.
Wasifu wa Azam:
Klabu ya Azam ilishiriki kwa mara ya kwanza kwenye michuano ya kombe la Kagame mwaka 2012 lakini walishangaza wengi kwa kumaliza kama washindi wa pili baada ya kufungwa na Yanga mabao 2-0 kwenye mchezo wa fainali.
Mwaka jana ilishiriki kwa mara ya pili na kuishia hatua ya robo fainali baada ya kutolewa na Al Merriekh kwa mikwaju ya penati.
Kundi ililopo:
Azam iko kwenye kundi C ikijumuishwa na KCCA ya Uganda, Adama City ya Ethiopia na, Azam inapewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri mwaka huu ikiundwa na wachezaji wengi waliokaa pamoja kwa muda mrefu.
Wachezaji wa kuangaliwa.
Kwa upande wa ushambuliaji inawategemea wachezaji kama Kipre Tchetche, Didier Kavumbagu.
Nahodha mzoefu wa Azam, John Bocco bado anaweza kuwa na mchango mkubwa. Mlinzi mahiri, Pascal Wawa anatarajiwa kuhakikisha ngome ya Azam haipitiki kwa urahisi. Brian Majwega, Salum Abubakar na Michel Bolou ni wachezaji wengine ambao ni nyota na muhimu kwenye timu hii.
Benchi la Ufundi:
Benchi la ufundi la Azam lipo chini ya usimamizi wa kocha Muingereza, Stewart Hall. Ni mara ya tatu kwa kocha Stewart Hall kuifundisha Azam.
Bila shaka, kocha Hall atakuwa na malengo ya kupiga hatua moja Zaidi baada ya kukaribia kubeba taji la Kombe la Kagame miaka mitatu iliyopita.
Rekodi Kombe la Kagame:
Azam inashiriki Kombe la Kagame kwa mara ya tatu. Mafanikio yake makubwa ni kufika fainali mnamo mwaka 2012 ilipolazwa mabao 2-0 na Yanga.
Wasifu wa KCCA:
Klabu hii inayomilikiwa na halmashauri ya jiji la Kampala ni moja ya timu kubwa Uganda ikichuana na timu maarufu Zaidi nchini humo, SC Villa na Express.
Wakati vigogo Sc Villa na Express wakionekana kusuasua, KCCA imeendelea kutoa makucha kwenye ligi ya Uganda licha ya kupoteza ubingwa wao msimu uliopita.
KCCA iliyowahi kufundishwa na Kocha msaidizi wa Azam, George Nsimbe inasifika kwa kucheza soka la kasi, ikishambulia Zaidi kutokea pembeni.
Baada ya kupoteza ubingwa walioshikilia mara mbili mfululizo, KCCA imejipanga upya kwa kusajili wachezaji wapya 11 na kutema idadi kama hio ya wachezaji walionekana kuwa mzigo.
Kundi Ililopo:
KCCA iko Kundi pamoja na Azam, Adama City ya Ethiopia, Malakia ya Sudani Kusini. Itakuwa miujiza KCCA kushindwa kufuzu kwa hatua ya robo fainali kutoka kundi hili.
Wachezaji wa kuangaliwa:
Tom Masiko ni kati ya viungo wanaotarajiwa kung’ara kwenye Kombe la Kagame. Walinzi Saka Mpima na Habib Kavuma ni kati ya walinzi wanaosifika kwa kushambulia licha licha ya kuwa kazi ya kulinda lango lao.
Mtanzania, Shaban Kondo aliyesajiliwa kwa ajili ya msimu huu mpya, anatarajiwa kuwa moja ya mchezaji atakayetazamwa kuona nini miguu yake inaweza kufanya akiwa dimbani.
Benchi la ufundi:
KCCA wanaonekana kuwa na benchi la ufundi pana Zaidi kuliko timu nyingi kwenye mashindano yam waka huu. Benchi lao la ufundi linajumuisha makocha saba chini ya usimamizi mkuu wa Mike Mutebi akisaidiwa na kocha Sam Ssimbwa
Rekodi Kombe la Kagame:
Ni mabingwa mara moja wa michuano hii wakiwa wamebeba kombe hilo mwaka 1978. Mwaka walifika katika hatua ya fainali lakini hawakubahati kupata ushindi mbele ya Al Merriekh ya Sudani.
NB: Kesho siku ya ijuma saa 5 kamili asubuhi, kutakua na mkutano na waandishi wa habari katika ukumbi wa TFF uliopo Karume. Rais wa CECAFA, Rais wa TFF na makatibu wakuu wa TFF na CECAFA watakuwepo.
Waandishi wa habari mnaombwa kuhudhuria bila kukosa.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment