Wednesday, July 22, 2015

HESHIMA NA TABIA NJEMA HUJENGEKA KWENYE NYOYO ZA WATU- DR.SHEIN

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif, Waziri wa Habari,utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Said Ali Mbarouk pamoja na washabiki wa Tamasha wakimshangiria Kiongozi wa Ngoma ya Utamaduni ya Lelemama akifanya vitu vyake wakati wa uzinduzi wa Tamasha la Utamaduni wa Mzanibari.
 Vazi lenye asili ya watu wa Kitumbatu walilokuwa wakilitumia wakati wakielekea mashambani huku mwana Mama anatembea akisuka ukili kuashiria ufundi wa utamaduni wa asili.
 Muimbaji mahiri wa Visiwa vya Comoro al anisa Shamsia Sagaf akitumbuiza kwenye uzinduzi wa Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibari hao Bwawani Mjini Zanzibar.
  Kikundi cha akina mama watupu wakitumbuiza ngoma ya asili ya Lelemama kwenye uzinduzi wa Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibari Mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif AlI Iddi kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein.
Hilo ni onyesho la asili la Koti, kanzu na kofia kwa mwanamme na Bui Bui la Kamba lililokuwa likivaliwa na akina mama wa zamani.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein amewakumbusha Wananchi wote Nchini kuelewa kwamba heshima na tabia njema iliyojengeka katika nyoyo za Watu wa Zanzibar kutokana na kupenda, amani na utulivu ni sehemu muhimu ya utamaduni wa Wazanzibar.

Alisema ni muhimu kwa kila Mwananchi kuhakikisha anatoa mchango wake katika kulinda, kuukuza na kuutangaza utamaduni wa Mzanzibari kwa kuzingatia mambo mazuri wanayoyapenda wananchi wenyewe.

Dr. Ali Mohammed Shein  alitoa kauli hiyo wakati akilizindua Tamasha la 20 la Utamaduni wa Mzanzibari katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo katika Ukumbi wa Salama Hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar.

Alisema endapo mkakati wa makusudi utawekwa wa kuwashawishi wageni kuiga mambo ya asili na utamaduni wanaoutembelea bila shaka wageni na watalii hao watavutiwa na kuyapenda na hatimae masuala hayo yatalipatia sifa Taifa hili.

Rais wa Zanzibar Alisema kwamba Zanzibar ina Historia inayowavutia wageni mbali mbali kutokana na Utamaduni wenye mchanganyiko wa mambo mengi jambo ambalo limevipatia heshima ya pekee Visiwa vya Zanzibar.

Alisisitiza jukumu la kila Mwananchi kushiriki kikamilifu katika kuvikataa na kuvipinga vitendo vinavyotia doa,Desturi, mila na Utamaduni ikiwa ni pamoja na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia ambavyo hivi sasa Serikali inaendelea na juhudi mbali mbali za kuvikomesha.

Aidha alitoa wito kwa Wananchi waendelee kuunga mkono kampeni inayofanywa na Serikali Kuu dhidi ya unyanyasaji wa Kijinsia iliyoianzisha Tarehe 6 Disemba mwaka 2014 isemayo Zanzibar bila ya udhalilishaji wa kijinsia inawezekana.

Ujumbe wa Mwaka huu wa Tamasha la 20 la Utamaduni wa Mzanzibar             “ Tudumishe Utamaduni wetu katika hali ya amani, utulivu na Umoja".

No comments: