Friday, July 24, 2015

CAG AONGOZA KIKAO CHA BODI YA UKAGUZI YA UMOJA WA MATAIFA

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa, Bw.Mussa Juma Assad akizungumza wakati wa hitimisho la mkutano wa siku mbili wa Bodi hiyo uliofanyika hapa Umoja wa Mataifa kuanzia Julai 22-23. Kushoto kwake ni Bw. Fransis Kitauli, Mkurugenzi wa Ukauzi wa Nje na Mwenyekiti wa Kamati ya Operesheni za Ukaguzi ( AOC) Akiwa Mwenyekiti wa AOC Bw. Kitauli ambaye alishika nafasi hiyo tangu mwaka 2012 amefanikisha utoaji wa ripoti za ukaguzi za Umoja wa Mataifa kwa miaka mitatu mfululizo.
Wajumbe wa Bodi ya Ukaguzi kutoka kushoto, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ya India, Bw. Shashi Kant Sharma, Sir Amyas Morse, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kutoka Serikali ya India na Bw. Mussa Juma Assad, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kutoka Serikali ya Tanzania wakitia saini zao katika ripoti 28 za ukaguzi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa zilizorejewa na kupitishwa na Bodi hiyo wakati wa mkutano wake wa siku mbili. ripoti hizo ni matokeo ya kazi kubwa ya Bodi hiyo.
Picha ya pamoja ya wajumbe wa Bodi wakiwa pamoja na wataalamu wao na wajumbe kutoka Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa.
Ujumbe wa Bodi ya Uingereza ukiongozwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu Sir Amyas Morse.
Ujumbe wa Bodi ya India ukiongozwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu Bw. Shadhi Sharma.
Ujumbe wa Bodi ya Tanzania ambao ni kutoka kushoto Jerome Francis, Naibu Mkurugenzi ukaguzi wa Nje, Bw. Salhina Mkumba, Naibu Mkurugenzi, Ukaguzi wa Nje na ambaye amefanya kazi kwa karibu sana na Bw. Fransis Kitauli tangu Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ilipoteuliwa kuingia kwenye Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa wa mwisho ni Bw. Athuman S. Mbuttuka, Naibu Mkaguzi Mkuu.

Na Mwandishi Maalum, New York

Bodi ya Ukaguzi wa Hesabu za Mashirika ya Umoja wa Mataifa , imemaliza mkutano wake wa siku mbili kwa kurejea na kupitisha taarifa 28 za ukaguzi.

Taarifa 22 kati ya hizo zitawasilishwa mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na sita zitawasilishwa kwa Mamlaka na vyombo vingine.

Mkutano huo umefanyika hapa Umoja wa Mataifa chini ya Uenyekiti wa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bw. Mussa Juma Assad.

Wajumbe wengine wa Bodi ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kutoka Serikali ya Uingereza Sir Amyas Morse na Bw. Shashi Kant Sharma, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kutoka Serikali ya India.

Akizungumza mara baada ya kutia saini taarifa hizo, jukumu lililofanywa kwa pamoja na wadhibiti na Wakaguzi hao watatu, Bw. Mussa Juma Assad amewashukuru wajumbe wenzie kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wameifanya katika siku hizo mbili pamoja na ushirikiano mzuri waliompatia.

“ Nichukue fursa hii kuwashukuru sana kwa kazi hii nzuri na ushirikiano mkubwa mlionipatia, ushirikiano ambao umetuwezesha kukamilisha kazi hii kwa wakati na muda muafaka”, akasema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali Bw. Assad.

Wakijibu shukrani hizo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kutoka Serikali ya Uingereza, Sir Amyas Morse alimshukuru Mwenyekiti kwa uongozi wake na upeo mkubwa ikiwa ni pamoja na ushirikiano wake kwa wajumbe wenzie.

Akatumia pia fursa hiyo kumpongeza na kumshukuru kwa moyo wa dhati, Bw. Fransis Kitauli ambaye kwa miaka mitatu akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Operesheni amefanikiwa kutolewa kwa ripoti za ukaguzi bila kukosa.

Sir Morse amemuelezea Bw. Kitauli kama Mkurungezi na Mwenyekiti ambaye ameonyesha weledi mkubwa na kujituma kwa hali ya juu katika utekelezaji wa majukumu yake amekuwa Mkurugenzi anayemwakilisha Mkaguzi Mkuu hapa Umoja wa Mataifa kwa uadilifu wake, na weledi mkubwa katika utekelezaji na usimamizi wa majukumu yake na akamtakia kila la kheri arejeapo Tanzania.

Kwa upande wake Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali ya India, Bw. Shashi Sharma, pamoja na kumshukuru Mwenyekiti kwa uongozi wake mahili naye alimpongeza na kumshukuru Bw. Fransis Kitauli kwa uhodari wake, kujituma na kazi kubwa aliyoifanyia katika utekelezaji na usimamizi wa majukumu ya Bodi hiyo.

No comments: