Benki ya Dunia Kanda ya Afrika imesema imeridhishwa na maboresho ya miundombinu yanayofanywa na Bandari ya Dar es Salaam kwa vile yatanufaisha Tanzania na nchi jirani ambazo zinatumia bandari hiyo kusafirisha mizigo kwenda nchini mwao.
Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika, Bw. Makhtar Diop alisema hayo wakati alipofanya ziara ya kutembelea bandari hiyo kujionea miradi wanayoifadhili na maboresho yote ya miundombinu inayolenga kuleta ufanisi wa kazi.
“Tunatambua kuwa maboresho haya muhimu kwa Tanzania na kwa mataifa jirani yanayotumia bandari hii,”alisema.
Bw. Diop alisema katika ziara hiyo aliambatana na Mwakilishi Mkazi mpya wa Benki Dunia Tanzania, Bella Bird na aliyekuwa Mwakilishi Mkazi wa Benki hiyo nchini, Bw. Philippe Dongier na maofisa wengine.
Alisema wote kwa pamoja wameridhika na hatua za maendeleo zinazochukuliwa na bandari hiyo katika kuboresha miundombinu yake.
Pia alisema mwakilishi huyo anayeondoka alikuwa akishirikiana vyema na serikali ya Tanzania na anatumaini mwakilishi mpya ataendeleza nyayo zake.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dkt. Shaaban Mwinjaka alisema maboresho hayo yataleta ufanisi wa kazi na bandari hiyo kuwa moja ya bandari nafuu zaidi na shindani ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika.
“Bandari yetu ipo katika hatua nzuri na Benki ya Dunia inatusaidia kufanya maboresho haya,” tunategemea bandari hii itakuwa shindani zaidi na nafuu, aliongeza kusema.
Alisema ujumbe huo kutoka benki hiyo ulikuja kuona miradi inayofanyika kwa ushirikiano na serikali na walifanya ziara katika gati namba moja hadi saba na barabara inayolenga kuondoa msongamano wa magari ndani ya bandari.
Alifafanua kwamba kiujumla kwa sasa mizigo inayopitia bandari hiyo imeongezeka kufikia tani milioni 14.7 ukilinganisha na miaka ya nyuma.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Bw. Awadh Massawe alisema benki hiyo inafadhili upanuzi wa mlango wa kuingilia meli ili uweze kupanuliwa zaidi kutoka mita 140.
“Hili linaenda sambamba na kuchimba kina cha maji kutoka mita 9.5 hadi mita 13 meli kubwa ziweze kuingia,”alisema.
Pia uongezaji kina cha maji kufikia mita 13 katika magati ya bandarini kuwezesha pia meli kubwa kutia nanga.
Mkurugenzi Mkuu anayeshughulikia Miundombinu katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Bw. Alois Matei alisema kazi ya upanuzi na kuchimba inaendelea vizuri na wanatarajia mwazoni mwa mwaka ujao kazi ya kuchimba itaanza.
“Kwa upande wa magati tayari mkandarasi amepatikana na hatua za mwisho zinaendelea,” alisema.
Bandari ya Dar es Salaam ipo katika hatua muhimu ya uboreshaji wa miundombinu yake kuwezesha ufanisi wa kazi na kuifanya bandari kuwa shindani
No comments:
Post a Comment