Thursday, July 9, 2015

Baraza la Uwezeshaji lakubaliana na mpango wa ujasiriamali wa chuo cha Cambridge

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Bi. Beng’i Issa (kulia) pamoja na Rais wa Cambridge Development Initiative (CDI), Bw. Ravi Solanki wakitia saini makubaliano ya kuimarisha elimu ya ujasiriamali kwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini jana jijini Dar es Salaam. Wanaoshuhudia ni Afisa Mwandamizi wa uwekezaji, NEEC, Bw. Oswald Karadisi (kulia) na Mkurugenzi Ujasiriamali wa CDI, Bi. Georgia Ware.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Bi. Beng’i Issa (kulia) akipongezana na Rais wa Cambridge Development Initiative (CDI), Bw. Ravi Solanki (kushoto) baada ya kutia saini makubaliano ya kuimarisha elimu ya ujasiriamali kwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini jana jijini Dar es Salaam. katikati ni Mkurugenzi wa Ujasiriamali wa CDI, Bi. Georgia Ware.

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) limefikia makubaliano na Cambridge Development Initiative (CDI) ili kuimarisha mafunzo ya maswala ya ujasiriamali kwa wanafunzi wa vyuo vikuu hapa nchini.

CDI ni mpango ulioasisiwa na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Cambridge cha nchini uingereza ambapo wanafunzi wenye vipaji toka chuo hicho na vyuo vikuu hapa nchini wanakutana, kubadilishana uzoefu ili kutatua changamoto mbalimbali.

Mkataba wa makubaliano hayo umetiwa saini na Katibu Mtendaji wa NEEC, Bi. Beng’i Issa wakati Rais wa mpango huo, Bw. Ravi Solanki aliwakilisha wenzake.

Akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam baada ya kutia saini mkataba huo, Bi. Beng’i alisema elimu na maarifa ya ujasiriamali ni muhimu sana kwa sasa ambapo changamoto ya ajira ni kubwa dunia nzima, Tanzania ikiwa mojawapo.
“Mzingatie sana maarifa mnayopata hapa…yatawasaidia katika maisha yenu,” aliwaasa wanafunzi hao.

Kwa sasa jumla ya wanafunzi 36 kutoka vyuo mbalimbali hapa nchini wanaendelea na mpango huo wa ujasiriamali yanayoitwa DAREnterprisers kwa muda wa miezi miwili yanayofanyika katika kituo cha Ujasiriamali cha chuo kikuu cha Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Ujasiriamali wa mkakati huo, Bi. Georgia Ware alisema ni imani ya mradi huo kuwa wanafunzi wanaweza kubadilisha dunia na kuwa sehemu bora ya kuishi.

“Wote hawa wana ujuzi na vipaji vyao, na kwa umri wao mdogo bado wana uwezo wa kujifunza mambo mengi,” alisema.
Alisema kama kila mmoja wa wanafunzi hao wanaopata mafunzo hayo akimshawishi mwenzake kufanya ujasiriamali basi jiji la Dar es Salaam linaweza kubadilika kwa kiwango kikubwa katika miaka mitano ijayo.

Katika mafunzo yanayoendelea, wanafunzi hao wanafundishwa kuhusu umeme mbadala, usafi wa maji na taka ngumu na jinsi ya kutunza miji.

Rais wa mpango huo, Solanki amesema mbali ya kuwapatia maarifa wanafunzi hao yatakayowawezesha kuwa wajasiriamali, pia program hiyo inalenga kuwafanya vijana kutatua changamoto katika jamii zao.

Mmoja wa wanaofaidika na mafunzo hayo, Katera Ahad amesema wanatarajia kupata maarifa yatakayowawezesha kujinoa katika mambo wanayotaka kutekeleza kama wajasiriamali.

Mpango huo ulianza mwaka 2013 ambapo wanafunzi 20 hapa nchini walifaidika na wanaendelea na miradi yao mbalimbali.    
Hivi karibuni NEEC ilizindua mwongozo wa Taifa wa Ufundishaji Ujasirimali (NETF) katika shule na vyuo ili kuwawezesha vijana wa kitanzania na wananchi kwa ujumla kuwa na elimu hiyo na kuchochea maendeleo.

Inatarajiwa kuwa vijana na wananchi watakaopata mafunzo hayo watakuwa na ujuzi unaotakiwa katika soko sekta binafsi na umma.  

No comments: