Thursday, July 9, 2015

BARAZA LA MADIWANI KINONDONI LAVUNJWA, RAIS MWINYI ALIMWAGIA SIFA

Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda akizungumza na madiwani na watendaji wa Manispaa hiyo wakati wa kikao maalum cha kuahirisha Baraza hilo kilichofanyika jana Dar es Salaam. Wengine ni Naibu Meya, Songoro Mnyonge na Mkurugenzi wa Manipss hiyo, Eng. Mussa Nati (kulia).
Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda akimtambulisha Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi kwa Madiwani wa Manispaa hiyo baada ya kuwasili kwenye ofisi za Manispaa hiyo kuhudhuria hafla maalum ya kuahirisha Baraza hilo Dar es Salaam jana.
Ofisa Kilimo (Umwagiliaji na Ushirika) wa Manispaa ya Kinondoni, Salehe Hija Mohamed akimelezea Rais Mstaafu alhaj Ali Hassan Mwinyi kuhusu mazao ya kilimo alipotembelea maonesho ya miradi mbalimbali ya Manispaa hiyo.
Rais Mstaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi akimvisha nishani Diwani wa Hananasif, Abbas Tarimba wkati wa hafla ya kuliahirisha Baraza la madiwani hao, Dar es Salaam jana. Wanaoshuhudia ni Meya wa Manispaa hiyo, Yusuph Mwenda, Naibu Meya, Songoro Mnyonge (kushoto), Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Raymind Mushi na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Eng. Mussa Nati.
Rais Mstaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi akimkabidhi cheti chake mmoja wa watumishi wa Manispaa hiyo, Deborah wakati wa hafla ya kuliahirisha Baraza la Madiwani hao jana. Wanaoshuhudia ni Meya wa Manispaa hiyo, Yusuph Mwenda, Naibu Meya, Songoro Mnyonge (kushoto), Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Raymind Mushi na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Eng. Mussa Nati.
Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda akionesha cheti cha Freeman alichokabidhiwa na Rais Mstaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi (kushoto kwake) katika hafla hiyo. Cheti hicho kinachotolewa na Baraza la Madiwani hutolewa mara chache kwa Meya aliyefanikiwa kutekeleza miradi ya wananchi kwa kiwango kikubwa na kina maana ya ‘Raia Huru’. Kushoto ni Naibu Meya, Songoro Mnyonge na Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Raymond Mushi.
Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda akimkabidhi jezi ya timu ya Soka ya Kinondoni (KMC FC) Rais Mstaafu alhaj Ali Hassan Mwinyi baada ya kukabidhiwa kuwa Mlezi wa klabu hiyo kwenye hafla hiyo.

RAIS Mstaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kwa mafanikio iliyoyapata katika kusimamia na kutekeleza miradi yake kwa kiwango kikubwa.

Rais Mwinyi alisema kuwa Manispaa hiyo ni ya mfano kutokana na kusimamia vema miradi yake na kuitekeleza kwa kiwango kikubwa jambo ambalo ni tofauti na Manispaa nyingine nchini.

Alisema kuwa ongezeko la makusanyo kwa asilimia 360 kutoka shilingi Bilioni 10 hadi kufikia Bilioni 36 kwa mwaka na kuifanya kuwa Halmashauri ya kwanza kuweza kusimamia miradi yake kwa fedha zake zenyewe pasipo kutgmea ruzuku ya Serikali.

Rais Mwinyi aliyasema hayo wakati wa hafla ya kuliahirisha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Kinondoni iliyofanyika kwenye ofisi za Manispaa hiyo, Dar es Salaam jana.

Aidha aliipongeza Manispaa hiyo kwa kuweza kuwahamasisha wananchi wake wapende usafi na hivyo kubadilisha kwa kiasi kikubwa mazingira ya usafi kwa maeneo mbalimbali ya Manispaa hiyo.

 “Nawashukuruni sana ndugu zangu, mmenifanyia mengi sana mtaani kwangu, nyumba yangu ilizungukwa na msitu, takataka, vumbi na kadhalika lakini leo nipo katikati ya Barabara safi za lami, Napata hewa safi mimi na bibi yenu.” Alisema kwa utani huku akicheka.

Kwa upande wake Meya wa Manispaa hiyo, Yusuph Mwenda aliwaahidi wananchi wa Manispaa yake kuendelea kushirikiana nao katika kuyaendeleza yale yote waliyoyafanya kwa kushirikiana na Madiwani na Watendaji wa Manispaa hiyo hata pale itakapotokea hawatarudi tena kwenye nafasi zao mwakani.

Aidha alisema kuwa anajivunia mafanikio makubwa yaliyoipata Manispaa hiyo katika kipindi cha uongozi wake ikiwemo kuongoza kati ya Halmashauri zote nchini na pia kung’ara katika Majiji ya Kati.

Hata hivyo Meya huyo aliwataka wananchi kuendeleza kampeni ya uwekaji safi mazingira ya Manispaa hiyo ili kupuka maradhi mbalimbali yanayosababishwa na uchafu.

“Haiwezekani Kinondoni kuwa safi kama wewe mwananchi haupo msafi. Ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha anasimamia vema maendeleo tuliyoyapata kwa faida yetu na vizazi vyetu.” Alisema Meya Mwenda.

Hafla ya kuliahirisha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ilikwenda sambamba na utoaji wa vyeti na tuzo kwa Madiwani, watendaji na maafisa wa idara mbalimbali za Halmashauri hiyo na kuhudhuriwa na viongozi wa ngazi za juu Serikalini, Wawakilishi wa madhehbu mbalimbali ya kidini, Wanasiasa na wananchi.

Katika hatua nyingine, Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni limemtunuku Meya wa Manispaa hiyo, Yusuph Mwenda cheti cha heshima cha Raia Huru ‘Freeman’ kwa kutambua mchango wake mkubwa katika kuiletea maendeleo Manispaa hiyo.

Meya huyo amekuwa ni wa kwanza kutunukiwa cheti hicho tangu kuanzishwa kwa Halmashauri hiyo ambacho kinamfanya sasa kuwa raia huru na kumtambua kama mtu aliyeleta mafanikio makubwa katika Manispaa hiyo na wananchi wake kwa ujumla.

No comments: