Tuesday, June 16, 2015

Vijana waridhishwa na mswada uliopitishwa bungeni wa kuanzishwa baraza la vijana la Taifa

Na Mwandishi wetu

Vijana wameridhishwa na mswada uliopitishwa bungeni wa kuanzishwa baraza la vijana la Taifa na kudai kuwa hiyo ndio njia mojawapo vijana wanaweza kuendeleza shughuli zao za maendeleo .

Wamedai kuwa katika mswada huo vijana wanangazi zao za uongozi kutoka vijijini hadi kitaifa na hali hiyo inakuwa ni rahisi vijana kuwa na uwezo wa kuelezea changamoto zinazowakabili .

Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es salaam na shirika la Restless Development Tanzania – ICS) linalojishughulisha na kuwaweka vijana kuwa mstari wa mbele katika kufikia maendeleo mara baada ya kumalizika kwa sherehe ya kutoa vyeti kwa vijana wakujitoea ambao wanasoma katika vyuo vikuu .

Mkurugenzi wa ICS bibi Margareth Mriwa alisema wamefurahishwa na mswada wa baraza la vijana kupitishwa bungeni na kudai kuwa wanaamini kwamba katika muswada huo kuna mikakati inayofaa kabisa ya kuwaelekeza vijana kufikia maendeleo .

‘’ Kwasasa hivi waliowengi nchini Tanzania ni vijana na wanauwezo wa kuchangia maendeleo na tunaomba wapewe fursa hiyo katika ngazi mbali mbali za maendeleo . Jambo la kwanza ni kwamba vijana wamejitenga kidogo katika jamii zao na hawapati nafasi wanazopenda kuchaguliwa ‘’ alisema bibi Margareth .

Ameongeza kuwa kuanzia mwaka 2013 kuna vijana wengi wameingia katika nafasi za uongozi na maamuzi kutoka ngazi ya vijiji hadi Taifa jambo linaloeta matumaini .

‘’ Sisi tunawapa vijana uwezo wa kufanya maamuzi na viongozi wapate kuchanganua sera ambazo zimetolewa na vijana kujiamulia kiongozi gani anaweza kusimamia masuala ya vijana zaidi’’ aliongeza

Amesema vijana wanachangamoto nyingi kwa hiyo hii ni fursa ya muafaka ya kuweza kuwashirikisha vijana katika mikakati inayokuja mipya ikiwemo ule wa malengo endelevu ya maendeleo na kuangalia jinsi gani vijana wanaweza kupewa nafasi sio tu kuzifanyia kazi sera bali pia kuchangia katika utekelezaji wa sera hizo.

Katika uchaguzi mkuu mwezo oktoba mwaka huu ametoa wito kwa vijana kujiandikisha kwa wingi katika daftari la kudumu la wapiga kura na kufanya maamuzi sahihi ya kuwachagua viongozi bora na pia kujitokeza kugombea nafasi za uongozi .

Kwa upande wake bwana Ridhione Juma , mratibu wa miradi ya ajira kwa vijana wa Restless Development Tanzania amesema walianzisha mradi wa uchaguzi ujulikanao kama fahamu , ongea na sikilizwa katika mikoa 18 nchini na katika mradi wa katiba ambao ni mwendelezo wa mradi huo walibaini kwamba vijana hawakuwa na taarifa sahihi kuhusu katiba na kwasasa wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu wengi hawana taarifa kwamba wakitaka kugombea ni hatua gani wazifuate .

Ameongeza kuwa umri usiwe kigezo cha vijana kugombea nafasi ya uraisi kwa vijana kwamba uraisi ni taasisi na sio mtu binafsi na vijana wengi licha ya kuwa na umri mdogo lakini wanamaono ya kusaidia kuongoza nafasi hiyo na kutoa mfano wa wabunge wengi vijana ambao wameibua mambo makubwa kuliko wabunge wazee .

Kwa upande wao wahitimu wa mafunzo Alen Charles kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam na Justus Tutus kutoka chuo cha Ardhi wametaka serikali itakayoingia madarakani kuwapa kipaumbele vijana katika kushiriki kufanya maamuzi katika jamii .

‘’ Sisi kilio chetu hasa ni fursa . Tunachotaka ni serikali ijayo kuweza kuweza kusimamia maslahi ya vijana katika misingi kutengeneza fursa a ambazo zitamuhusisha kijana moja kwa moja katika kujikwamua kimaendeleo ‘’ Nchi yetu inautajiri mwingi na kunaile hali ya kuamini kwamba vijana uwezo wa kutumia fursa zao kujiendeeza ‘’ alisema Alen .

Amesema kuwa wanataka serikali itakayotambua umuhimu wa vijana kwa kuwahusisha katika ngazi mbali mbali za maamuzi na itakayotambua kuwa kijana anao wajibu wa kutimiza majukumu mbali mbali ya nchi katika kuhakikisha jamii inakuwa na maendeeo .

‘’ Unajua Tanzania kuna vijana ambao hawajatumika kwahiyo inabidi zitengenezwe sera na mikakati ambayo itatumia akili na maarifa ya vijana katika kuleta maendeleo ya Taifa na vijana kupewa kipaumbele katika kushiriki kwenye maamuzi yanayofanyika katika jamii ‘’ alisema Justus Tutus

Amewaomba vijana wenzake kujitokeza kupiga kura kwakuwa kura zao ndizo zitaweza kubalisha mstakabali wa Taifa .

Katika sherehe hiyo vijana kutoka chuo cha Dar es saalam na chuo cha ardhi wametunukiwa vyeti baada ya kutambua mchango wao katika kuelimisha wenzao kuhusu ajira , ujasiriamali , afya ya uzazi pamoja na ushiriki wa kiraiya na pia wengine walishiriki katika mafunzo ya TEHAMA kwa ajii ya maendeleo ambapo walifundishwa matumizi ya elimu ya mawasiliano katika sehemu za kazi na matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii katika kuleta maendeleo ya biashara na kuhamasisha vijana kwenye masuala mbali mbali .

No comments: