Kamishna Msaidizi – Ukaguzi wa Migodi, Mhandisi Ally Samaje kutoka Wizara ya Nishati na Madini (Kushoto) akijadiliana jambo na Mtaalam mwelekezi kutoka Taasisi ya Sayansi na Mazingira ya Nchini India, Sujit Kumar Singh (Kulia) kwenye mafunzo yaliyoshirikisha wakaguzi wa migodini nchini yaliyofanyika mjini Bagamoyo mkoani Pwani.
Sehemu ya washiriki wa mafunzo yaliyoshirikisha wakaguzi wa migodini nchini yaliyofanyika mjini Bagamoyo mkoani Pwani wakishiriki katika zoezi la kuandaa mpango wa mazingira kwa vitendo katika mafunzo hayo.
Na Greyson Mwase, Bagamoyo
Taasisi ya Sayansi na Mazingira kutoka nchini India (Centre for Science and Environment) kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati na Madini, imekamilisha mafunzo ya siku nne yaliyoshirikisha wakaguzi wa migodi nchini ambapo wakaguzi walijifunza jinsi ya kuandaa miongozo mbalimbali kwa ajili ya kutumika kwenye ukaguzi wa mazingira kwenye migodi.
Akizungumza katika mahojiano maalum wakati wa mafunzo hayo, Kamishna Msaidizi – Ukaguzi wa Migodi, Mhandisi Ally Samaje alisema lengo la mafunzo hayo lilikuwa ni kuwapa uelewa wakaguzi wa mazingira na migodi nchini wa kuandaa, kuchambua na kupitia taarifa za athari kwenye mazingira kutokana na shughuli za uchimbaji wa madini.
Mhadisi Samaje alisema kuwa uelewa huu utawapa uwezo wakaguzi wa migodi kuchangia kikamilifu taarifa za athari kwa mazingira zinazowasilishwa na wawekezaji katika sekta ya madini kupitia Baraza la Mazingira la Taifa (NEMC).
Mhandisi Samaje ambaye pia ni Mkaguzi Mkuu wa Migodi aliendelea kusema kuwa mbali na kuwapa wakaguzi wa migodi uelewa wa kupitia taarifa za athari kwenye mazingira kutokana na shughuli za uchimbaji wa madini nchini, mafunzo hayo yanawapa uwezo zaidi wa kukagua shughuli za utunzaji wa mazingira katika migodi kwa kuzingatia masharti ya mpango wa utunzaji wa mazingira ili kuhakikisha kuwa mazingira yanatunzwa ipasavyo.
Alisema nchi ya Tanzania inahitaji miongozo mbalimbali iliyo bora katika usimamizi wa mazingira, na kusisitiza kuwa ili kukidhi haja hiyo, Wizara ya Nishati na Madini imekuwa ikiandaa mafunzo yanayohusiana na ukaguzi wa mazingira kwenye migodi ili kuhakikisha kuwa uchimbaji madini unakuwa ni salama.
“ Kama Serikali tunataka kuhakikisha kuwa mbali na wachimbaji madini nchini kunufaika na kipato kutokana na shughuli za uchimbaji madini, tunataka wafanye kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za usimamizi wa mazingira,” alisema Mhandisi Samaje.
Alisisitiza kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na taasisi nyingine nchini katika kuhakikisha kuwa mazingira hususan kwenye maeneo ya migodi yanatunzwa ipasavyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti washiriki wa mafunzo hayo, walisema mafunzo hayo yaliwapa uelewa mpana katika usimamizi na ukaguzi wa mazingira kwenye migodi.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Mhandisi Migodi Jones Mushi kutoka Idara ya Madini, Wizara ya Nishati na Madini alisema kuwa mafunzo hayo yamewawezesha kujifunza jinsi ya uandaaji wa taarifa za mazingira, pamoja na vigezo vinavyotumika katika kuchambua taarifa za mazingira.
Mhandisi Mushi alisema mafunzo hayo yamewawezesha kufanya kazi kwa kujiamini kutokana na uzoefu walioupata kutoka nchi ya India ambao utawawezesha kuboresha utendaji kazi wao.
Naye Mhandisi Migodi kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Cuthbert Cyprian aliongeza kuwa mbali na kujifunza uandaaji wa miongozo mbalimbali katika ukaguzi wa mazingira kweye migodi, wamejifunza namna ya uandaaji wa hadidu za rejea kwa ajili ya kuandaa tathmini ya athari za mazingira.
Mhandisi Cyprian alisema mafunzo hayo yaliwawezesha kujifunza jinsi ya kukabiliana na athari za mazingira kwenye migodi pamoja na ulipaji fidia kwa waathirika pindi migodi mipya inapoanzishwa.
“Zoezi la ulipaji fidia lina changamoto zake, lakini uzoefu tulioupata kutoka nchi ya India kupitia mafunzo haya ninaamini utatuwezesha sisi kama wataalam kuboresha maeneo yenye kuhitaji maboresho ili kumaliza changamoto hizo,” alisema Cyprian.
Cyprian aliiomba Serikali kuendelea kutoa mafuzo zaidi katika ukaguzi wa mazingira kwenye migodi pamoja na uboreshaji wa sheria na kanuni za mazingira ili kuhakikisha kuwa wachimbaji madini wanafanya shughuli zao katika mazingira ambayo ni bora na salama.
Naye Mhandisi Migodi kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Fadhili Kitivai alisema kuwa mafunzo hayo yaliwawezesha kujifunza mikakati mbalimbali ya utunzaji wa mazingira hasa baada ya shughuli za madini kumalizika.
Alisema mara nyingi baada ya shughuli za uchimbaji madini kumalizika nchini, migodi mingi imekuwa ikijitahidi kurudisha maeneo yake katika uasilia wake na kusisitiza kuwa kupitia mafunzo hayo, walijifunza mbinu mbadala za kuendeleza maeneo yaliyoachwa na migodi.
No comments:
Post a Comment