(Yanatolewa chini ya Kanuni ya 86(6) ya Kanuni
za Bunge, toleo la mwaka 2013)
1. UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
muswada huu ulio mbele yetu kwa malengo yake kama utasimamiwa vyema ni mzuri
kwani utaboresha mifumo ya mauzo ya
mazao ya kilimo na bidhaa zingine kwa kadri mahitaji ya nguvu za soko
yatakavyopelekea. Katika Hotuba ya
Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara ya mwaka 2014/15 alieleza dhamira na
uhitaji wa kuwepo kwa mfumo huu wa soko la bidhaa. Kwani alieleza uwepo wa kitu
kinachoitwa COWABAMA -
(Collective
Warehouse Marketing Systems) na kueleza kuwa huo ni mwendelezo wa kuanzisha
Soko la Mazao na Bidhaa (Commodity Exchange Market).
Mheshimiwa
Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani haina pingamizi na muswada huu wa Sheria ya Commodity
Exchange kwani hili lilikuwa ni hitaji
la wadau ambao wanashiriki katika mfumo mzima wa Stakabadhi za mazao Ghalani.
Tunaamini kwa kiasi kikubwa wahusika katika mfumo huu wameshirikishwa kwa hatua
zote za uandaaji wa muswada huu.
Mheshimiwa Spika, Kambi
ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge lako ikiwa imefanya
jitihada zozote za kuhakikisha kuwa elimu kwa umma hasa kwa wadau wote wa mfumo
wa masoko ya bidhaa inatolewa. Sheria
nyingi zinazoletwa katika Bunge hili zimekua zikilalamikiwa kutowafikia
walengwa na hivyo utekelezaji wake siku zote umekua ukileta migogoro isiyoisha
na mwishowe kusababisha hasara si tu kwa wazalishaji bali pia kwa watumiaji wa
mwisho. Ni mikakati gani imewekwa ili kuhakikisha kuna utoaji elimu endelevu
katika masuala ya masoko ya bidhaa?
Mheshimiwa Spika, hali
ya miundombnu nchini hasa usafiri wa barabara na reli ambao ndio tegemezi kwa
ajili ya usafirishaji wa bidhaa hasa za kilimo ni mbaya na isiyoridhisha. Sote
ni mashahidi kuwa , pamoja na Serikali kujisifu kwa kuweka mtandao mkubwa wa
barabara lakini barabara hizi hazijajengwa kwa ubora na ziinaleta changamoto
kubwa za usafirishaji wa bidhaa hasa kipindi cha mvua. Leo tunapotaka kupitisha
muswada huu wa masoko ya bidhaa, ni kwa kiasi gani tumeandaa mikakati ya
kuimarisha miundombinu ili wauzaji na wanunuzi wa bidhaa wasipate hasara? ikiwa
tutaendelea kuwa na miundombinu mibovu kama ilivyo sasa, ni dhahiri kuwa hata
utekelezaji wa Sheria hii utakua mgumu na hivyo kuwa na Sheria bubu isiyoendana
na mahitaji ya masoko ya bidhaa na hivyo kudidimiza uchumi badala ya kuinua
uchumi .
Mheshimiwa Spika,
maendeleo ya teknolojia katika masoko ya bidhaa ni mojawapo ya sababu
zitakazoweza kufanikisha ama kufelisha utekelezaji wa Sheria hii. Ni kwa kiasi
gani Serikali imeweka mikakati ya kukabiliana na ukuaji wa teknolojia
utakaomwezesha mtumiaji wa masoko ya Bidhaa ya Tanzania kuendana na mtumiaji wa
masoko ya bidhaa mahali pengine duniani?
Mheshimiwa Spika, pamoja
na kuletwa kwa Sheria hii katika Bunge lako, ni dhahiri kuwa ili sheria hii
iweze kutekelezwa kwa kiwango kinachotakikana, kanuni na miongozo yake ni
lazima iwepo. Ikiwa Sheria hii italetwa na kanuni zitachelewa kutungwa, basi
utekelezaji wake hautakua na maana yoyote na hivyo kuchangia kwa migogoro na
migongano ya kisheria
2. MAPITIO YA MUSWADA
Mheshimiwa Spika,
kifungu cha 5 cha muswada kinachohusu malengo ya mdhibiti yanayohusiana na
masoko ya bidhaa. Kambi Rasmi inapenda kupata taarifa ya kina kwani Mdhibiti
ambaye ni CMSA yeye hana bidhaa bali bidhaa zinazotakiwa kuingia katika soko
ambalo liko chini yake ziko chini ya mamlaka zingine ambazo zimeanzishwa
kisheria na zinazo kanuni zake za uendeshaji; mamlaka hizo ni kama vile bodi ya
Korosho, Bodi ya Kahawa, Bodi ya nafaka na
Mazao mchanganyiko: Hivyo basi
kwa kuangalia majukumu ya mdhibiti katika sheria hii ni dhahiri kuwa
taasisi hizo hazitakuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa
sheria zilizozianzisha.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi inaungana na wadau ambao wameliona tatizo hizo la kuziweka pembeni
mamlaka na wakala za Serikali kama ambavyo baadhi yake zilivyoainishwa hapo juu, kwani kuna bidhaa
ambazo zinatakiwa ziingie katika mfumo mzima
au mnyororo wa uongezwaji wa thamani
kabla ya kuwekwa katika soko la bidhaa. Na hapa Wizara mbalimbali
zinahusika, na Waziri aliyetajwa ni Mmoja tu Waziri wa Fedha. Hii inaweza
kukwamisha utekelezaji wa mfumo huu ambao tunaamini kuwa ni kwa faida ya
wazalishaji wa bidhaa hapa nchini.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inataka maelezo kuhusiana na suala hilo la
kutokutambuliwa na sheria kwa watendaji wengine wa Serikali ambao ni nguzo pia
katika kuhakikisha bidhaa inauzwa, au wako karibu na wazalishaji.
Mheshimiwa Spika,
katika kifungu cha 6 kinachohusu majukumu au kazi za mdhibiti, limetumika neno “Institutions” lakini neno hilo
halijatolewa tafsiri, hivyo basi ni muhimu neno hilo likatolewa tafsiri yake ili kuondoa mkanganyiko kwa wadau wa
Sheria hii.
Mheshimiwa Spika,
kifungu cha 8(3) kinasema kwamba
“A company which is
licensed as a commodity exchange shall not appoint any person to the position
of Chief Executive Officer or Managing Director, senior management or the Board
of Directors, change a substantial shareholder or change the organization
structure without obtaining prior confirmation of the Authority”.
Mheshimiwa Spika, ni
vyema Kambi Rasmi ya Upinzani ikapata maelezo ya kina kuhusiana na katazo hilo
kwani kampuni pindi inaposajiliwa kwa mujibu wa sheria za makampuni sura ya
212, inakuwa na bodi yake na inakuwa na mamlaka kamili, na pia katika utendaji
wake wa kazi bodi ndiyo yenye mamlaka ya kuteua nani awe ni mtendaji mkuu wa
kampuni husika kwa vigezo walivyoweka wao.
Mheshimiwa Spika,
Aidha, kulingana na mazingira ya kampuni ni jukumu la kampuni husika au
wanahisa ambao ni wakurugenzi kuingiza mwanahisa au kumtoa kulingana na
Articles of Association (makubaliano yao)
zinavyosema. Sasa kitendo cha kuomba ruhusa kwanza kwa Mdhibiti wa
Uendeshaji wa Soko la Bidhaa ni kuingilia mambo binafsi ya Kampuni husika.
Tukumbuke kuwa Mtendaji Mkuu ni mwajiriwa na si mmiliki pale ambapo mmiliki akiona mtendaji mkuu hafanyikazi wala
kutekeleza majukumu yake kwa maslahi ya wanahisa hivyo ni jukumu la Bodi ya
wakurugenzi kuchukua maamuzi.
Mheshimiwa Spika,
kifungu cha 3 na 4 cha muswada kinatoa ishara kama kwamba (makampuni yote) wale
wote waliopata leseni “licensees” za
soko la bidhaa ni mali ya Mamlaka,
tukumbuke kwamba wadau wakuu wengi ni sekta binafsi hivyo kuiambia sekta
binafsi isibadilishe mfumo wa utendaji kazi na watendaji wake, ni kuingilia
masuala binafsi ya kampuni. Kambi Rasmi ya Upinzani inasema, Jambo hili
halikubaliki kabisa na hivyo basi vifungu hivyo vifutwe kwa lengo la kuleta
tija.
Mheshimiwa Spika,
kifungu cha 9 (1) (b), (c) katika muswada bado vinaingilia mamlaka binafsi ya
Kampuni na pia vinaweka ulinzi ambao utasababisha watendaji kujiona nao ni
wamiliki na hivyo kuathiri utendaji kazi wao. Hoja ya Msingi ambayo Kambi Rasmi
ya Upinzani ingependa kuuliza ni kwanini ulinzi huo wa nafasi ya Mtendaji Mkuu
hadi kuwekwa katika Sheria? Ni kweli kwamba haina ushindani pale wenye kampuni
wanapotaka kufanya mabadiliko ya uongozi? Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali
kufuta vifungu hivyo vya ulinzi wa nafasi hiyo.
Mheshimiwa Spika,
kifungu cha 67 cha muswada ambacho kinaelekeza kutumia maelezo ya kifungu cha
66(c ) cha sheria ya CAPITAL MARKET kuhusiana na tafsiri ya maneno ya mienendo
mbalimbali ambayo hairuhusiwi kwenye biashara ya masoko ya bidhaa. Katika hilo
Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kitendo cha kutumia rejea ya sheria nyingine “cross reference” ya
sheria nyingine kwenye sheria hii ni uzembe, kwani sio mara zote mtumiaji wa
sheria hii atakuwa katika nafasi ya kuwa na sheria nyingine ambayo inafanyiwa rejea.
Aidha,
Mheshimiwa Spika, kifungu hicho
hicho kimetumia maneno “manipulation, rigging Bucketing and
Cornering” lakini kwa bahati mbaya katika kifungu cha 2 cha muswada kinachohusu
tafsiri ya maneno, maneno hayo hayapo. Pia kwa kuwa tunatarajia sheria hii iwe
toshelevu katika matumizi yake. Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka
Serikali kuhakikisha kwamba kila kifungu katika sheria hii kijitosheleze badala
ya kufanya rejea katika kifungu kingine cha sheria nyingine.
Mheshimiwa Spika,
kifungu cha 70 cha muswada kinachohusu “liability
to pay damages” kuwa mtu yeyote atakayekutwa na hatia katika sehemu nzima
ya XIII mbali ya kosa la kijinai kwa kosa husika pia atalazimika kufidia hasara iliyotokea
katika manunuzi. Kambi Rasmi ya Upinzani inashauri kwamba kwa kuwa kitendo
chochote cha kupanga kinachopelekea hasara kwa bidhaa hasa za kilimo. Maana
yake ni kuhatarisha maisha ya mkulima, hivyo basi adhabu kali inatakiwa kutajwa
kwenye sheria hii. Kwani adhabu ilivyowekwa katika muswada huu wa sheria haiko wazi
ili kuwafanya wenye nia ovu kushtuka.
Mheshimiwa Spika,
kifungu cha 82 cha muswada kinachohusu ulinzi “immunity” kuwa mamlaka, afisa au
mtumishi yeyote hatahesabika ametenda kosa kwa kutenda au kutokutenda jambo na
kupelekea hasara wakati akitimiza wajibu wake kwa nia njema, hadi pale itakapo
bainika kuwa alikuwa ana nia mbaya.
Mheshimiwa Spika,
kifungu hiki kama ambavyo kwa sheria nyingine zilizopita Kambi Rasmi ya
Upinzani imekuwa haikubaliani na kifungu cha aina hii kwani kinahalalisha
uzembe. Kwa sekta ya afya, uzembe wowote
unagharimu maisha ya mtu na pia hapa tukiachia sheria kuwa na kifungu hiki,
maana yake tunatoa mwanya wa kutokuwajibika na mwishowe ni hasara na inaweza
leta athari kubwa kwa wanunuzi wa bidhaa
na mara zote hasara inapelekwa kwa mzalishaji hasa mkulima kwa kuwa yeye ndiye
mnyonge katika mfumo wa masoko ya bidhaa za kilimo. Hivyo basi, Kambi Rasmi ya
Upinzani inataka kifungu hiki kifutwe.
Mheshimiwa Spika,
baada ya kuyasema hayo kwa niaba ya
Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.
…………………………………
David Ernest Silinde (Mb)
K.n.y Waziri Kivuli- Wizara ya Fedha
29.06.2015
No comments:
Post a Comment