Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwamuwakilisha Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein, katika ufunguzi wa mkutano wa Kimataifa wa muziki kwa nchi za jahazi, inaofanyika chuo cha muziki Forodhani Zanzibar.
Mkurugenzi wa Chuo cha Muziki Zanzibar bibi Fatma Kilua, akimkaribisha mgeni rasmi Maalim Seif katika ufunguzi za mkutano huo.
Muandaaji wa mkutano huo Profesa Raymond Vogals, akizungumza machache kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi.
Baadhi ya washiriki wa mkutano huo wa kimataifa wa muziki, wakisikiliza hotuba ya mgeni rasmi Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad kwa niaba ya Dkt. Shein.
Mwanafunzi wa Diploma katika chuo cha muziki Zanzibar Gora Mohamed (kulia), akitumbuiza katika hafla ya ufunguzi wa mkutano huo.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akisalimiana na baadhi ya washiriki wa mkutano huo wa muziki, baada ya kuufungua rasmi huko chuo cha muziki Forodhani Zanzibar.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa mkutano wa kimataifa wa muziki unaofanyika chuo cha muziki Forodhani Zanzibar. (Picha na Salmin Said, OMKR)
Na: Hassan Hamad (OMKR)
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein, amesema sanaa ya muziki ina nafasi kubwa ya kuendeleza amani na maelewano duniani.
Amesema kupitia sanaa hiyo wanamuziki kutoka pembe tofauti za dunia wamekuwa wakikutana kubadilishana uzoefu na kusoma tamaduni za kila upande, jambo ambalo husaidia pia kuzitangaza nchi na tamaduni zao katika ramani ya dunia.
Dkt. Shein ameeleza hayo huko chuo cha muziki Forodhani, katika hotuba yake iliyosomwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, wakati akifungua mkutano wa kimataifa wa siku nne wa muziki kwa nchi za jahazi.
Amesema Zanzibar ikiwa nchi yenye historia ya muziki hasa wa Taarab, imekuwa ikijifunza kutoka kwa wanamuziki wa nchi nyingi duniani zikiwemo India, Misri na nchi za Afrika kama vile Nigeria, Congo na Comoro, jambo ambalo limeifanya Zanzibar kuwa na uhusiano wa karibu wa kiutamaduni na nchi hizo.
Amefahamisha kuwa Zanzibar inakusudia kuibua na kuendeleza vipaji vya wanamuziki wachanga, na kwamba mkutano huo utatoa fursa kwa wanamuziki wa Zanzibar kujifunza mbinu mbali mbali za muziki zitakazosaidia kukuza vipaji vyao.
Katika hotuba hiyo Dkt. Shein amewataka washiriki wa mkutano huo kuijadili kwa uwazi maudhui ya mkutano huo, ili kufikia malengo ya kukuza muziki wa Afrika ambao ni muhimu katika kukuza maelewano miongoni mwa nchi na wananchi wa mataifa hayo kwa ujumla.
Ameeleza kuwa Zanzibar inajivunia historia ya muziki wa taarab asilia iliyopata umaarufu mkubwa kutokana na mwimbaji wake wa mwanzo marehemu Siti Bin Saad kuanzia miaka ya 1920’s, hatua ambayo imepelekea kuibuka kwa muziki wa kisasa wa taarab “modern taarab”, ambayo imekuwa ikipendwa na vijana wengi wa ndani na nje ya nchi.
Naye Mkurugenzi wa Chuo cha Muziki Zanzibar bibi Fatma Kilua, amesema kufanyika kwa mkutano huo hapa Zanzibar ni fursa pekee kwa wanamuziki wa Zanzibar kujifunza na kuitangaza katika fani hiyo.
“Kama chuo tumefarijika sana kuwa mwenyeji wa mkutano huu wa kimataifa ambao utatoa fursa kwa vijana wetu kujifunza mbinu mbali za muziki”, alieleza bi. Kilua.
Kwa upande wake muandaaji wa mkutano huo Profesa Raymond Vogals amesema, sanaa ya muziki imekuwa ikipata maendeleo makubwa duniani, na tayari wanamuziki kadhaa wameshahitimu shahada ya uzamivu (PHD) katika fani hiyo wakiwemo pia kutoka bara la Afrika.
“Muziki ni taaluma ambayo imekuwa ikipata mafanikio makubwa duniani, kwa hivyo tusome muziki wa Kiafrika ili kuendeleza taalum hii ambayo pia husaidia kutoa ajira”, alisisitiza Prof. Raymond.
No comments:
Post a Comment