Tuesday, June 30, 2015

KESI YA MIRATHI YA MALI ZA MWANDISHI WA HABARI MKONGWE NCHINI YAUNGURUMA JIJINI ARUSHA

Mwandishi wa habari mwandamizi marehemu
Betty Luzuka aliyefariki mwezi Agosti mwaka 2013 jijini Arusha.
Mwandishi wetu, 
Arusha
KESI ya kugombea  mirathi ya mwandishi wa habari mkongwe nchini marehemu Betty Luzuka imeibua mapya  mahakamani mara baada ya ushahidi wa njia ya video kumuonyesha mke wa aliyekuwa ofisa mwandamizi wa  jumuiya ya  Afrika Mashariki , Phil Makini Kleruu aitwaye Hilda Kleruu akichukua fedha za marehemu kabla na baada ya marehemu kuaga dunia.
Hilda, ambaye amefunguliwa kesi na kaka wa marehemu, Ssarongo Luzuka, akimtuhumu kujimilikisha mali za marehemu bila kufuata utaratibu wa kifamilia na kimahakama mara baada ya marehemu kuaga dunia Agosti mwaka 2013 katika hospitali ya Shree Hindu ya jijini Arusha baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Kesi hiyo ya mirathi inayovuta hisia za watu mbalimbali jijini Arusha  ipo katika mahakama ya mwanzo ya Maromboso  yenye nambari 222 ya mwaka 2013 inaitaka mahakama hiyo ipitie hukumu yake iliyotolewa Septemba 27 mwaka 2013  na hakimu Prince Gideon iliyompa  ushindi kaka wa marehemu.
Hata hivyo,upande wa mdaiwa umepinga hatua hiyo kwa  kutokuridhishwa na hukumu hiyo kutokana na kudai kuwa ana wosia halali alioachiwa na marehemu uliomilikisha mali zake zote  ambazo ni nyumba tatu zilizopo maeneo ya Njiro,Olmatejoo na Pemba road,mamilioni ya fedha zilizopo katika akaunti mbalimbali  pamoja na shamba lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 3 lililopo eneo la Mkonoo mkoani Arusha.
Katika kesi hiyo iliyopo mbele ya hakimu  wa mahakama hiyo,Moka Mashaga upande wa  wadai  wanaitaka mahakama kutupilia mbali  wosia uliowasilishwa na mdaiwa kwa kuwa ni batili,umepikwa  na kwamba sahihi ya marehemu imeghushiwa.
Ushahidi uliotolewa mahakamani hapo wiki iliyopita kwa njia ya video na upande wa mdai katika kesi hiyo aliiambia mahakama kuwa mdaiwa (Hilda) alikuwa akitoa fedha kwa nyakati tofauti katika benki ya  CRDB tawi la Mapato  jijini Arusha kwenye akaunti ya marehemu huku akitambua kuwa siyo msimamizi halali wa mali za marehemu hali ambayo iliwalazimu wao kufika polisi kutoa taarifa na hatimaye akaunti hizo kuzuiwa hadi kesi hiyo itakapomalizika.
Ssarongo aliiambia mahakama hiyo kwamba yeye na dada yake Jully Luzuka ndiyo waliochaguliwa na familia kuwa wasimamizi wa mali za marehemu kupitia kikao cha familia kilichofanyika Septemba 27 mwaka 2013 na kisha baadaye kuthibitishwa na mahakama bila shaka na wakati hayo yakifanyika hakuna mtu yoyote aliyejitokeza kuonyesha ameachiwa wosia na  marehemu.
 Ssarongo aliiambia mahakama hiyo kwamba mdaiwa alichukua jumla ya kiasi cha sh,milioni 8 kupitia akaunti ya marehemu kwa nyakati tofauti ikiwemo siku ambayo marehemu aliaga dunia ambayo ni Agosti 8 mwaka 2013 ambapo kwa mujibu wa taarifa walizopatiwa na benki ya CRDB zinaonyesha siku hiyo alichukua jumla ya kiasi cha sh,milioni moja.
“Tulikuwa tukijiuliza maswali mengi je kuna hela za marehemu zimeanza kutoka?je kadi zake za benki ziko wapi ,tulihoji hizi laki nne mara laki mbili mara milioni moja kupitia simu yake ya mkononi zinatoka wapi? tukasema hii hapana ndipo tukaenda benki na polisi kuwajulisha kuomba waiblock(waizuie)”Ssarongo aliiambia mahakama hiyo

Ssarongo alienda mbali zaidi na kuiambia mahakama hiyo kwamba walishangaa marehemu dada yao baada ya kufariki, Hilda Kleruu pamoja na mumewe Kleruu ghafla walijichagua kuwa wasimamizi wa mazishi ya marehemu dada yao bila kuwashirikisha ndugu ambapo Hilda alishika nafasi ya mweka hazina huku mumewe ambaye aliwahi kuwa mtumishi katika jumuiya ya Afrika Mashariki  akishika nafasi ya mwenyekiti wa kamati ya mazishi.
Hata hivyo,shahidi mwingine katika kesi  hiyo ambaye ni dada wa marehemu, Jully Luzuka, alijikuta akiangua kilio mahakamani hapo wakati akitoa ushahidi ambapo mbali na kuiomba mahakama hiyo iwatendee haki pia alisema kuwa katika kipindi chote alichougua marehemu hakuwahi kujulishwa na mdaiwa  kwamba marehemu ni mgonjwa mahututi pamoja kwamba alikuwa akimuuguza nyumbani kwake.
Shahidi mwingine ambaye ni mdogo wa marehemu,Theresa Charlote, aliiambia mahakama  kwamba anakumbuka wakati wa kuanua matanga katika kikao cha familia hakuna mtu yoyote aliyejitokeza kusema kwamba ameachiwa wosia na marehemu pamoja na tamko la kumtaka mtu yoyote aliyeachiwa wosia huo kujitokeza.
“Nakumbuka wakati wa kuanua matanga kaka Ssarongo aliuliza je kuna mtu yoyote ameachiwa wosia na marehemu lakini hakuna hata mmoja aliyejitokeza kusema ana wosia huo”Charlote aliiambia mahakama hiyo
Mara baada ya mahakama hiyo kusikiliza ushahidi huo hakimu anayesikiliza kesi hiyo aliamua kuihairisha hadi Julai 6 mwaka huu ambapo mashahidi wanne kutoka upande wa wadai watafika mahakama hapo kutoa ushahidi wao kabla ya mahakama hiyo kupanga  tarehe ya hukumu.

No comments: