Monday, June 15, 2015

BODI YA MIKOPO WAASWA KUTOA MIKOPO KWA USAWA.

 Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu na Utawala wa HESB Bi. Nuru Sovella akiongea katika hafla ya kufunga mafunzo kwa watumishi wapya wa Bodi hiyo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. George Nyatega.
 Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. George Nyatega akiwa katika picha kumbukumbu na watumishi wapya wa Bodi hiyo mara baada ya kufunga mafunzo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
 Baadhi ya watumishi wapya wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) wakifuatilia mafunzo yaliyoandaliwa na HESLB kwa ajili yao mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Habari na Utafiti (RAAWU), tawi la Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Bw. Deodatus Mwiliko akiongea na watumishi wapya wa HESLB jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Picha na HESLB.  


Na Mwandishi Wetu
Watumishi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) wametakiwa kusoma na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ili kutoa huduma bora kwa wateja wa Bodi hiyo.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya wiki moja kwa wafanyakazi wapya 24 wa HESLB jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. George Nyatega alisema wateja wa Bodi wanahitaji huduma bora na inayotolewa kwa adabu na kwa kuzingatia kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.

“Wateja wetu, wakiwemo wanafunzi, ni watu wazima na hivyo wanahitaji huduma bora na inayotolewa kwa adabu kutoka kwetu,” alisema Bw. Nyatega na kusisistiza watumishi wote wa Bodi wanapaswa kuzingatia misingi hiyo katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Mambo mliyofundishwa siyo siri, jengeni tabia ya kutafuta, kusoma, kuyaishi na kuyatekeleza kama inavyotakiwa,” alisema Mkurugenzi Mtendaji huyo na kuongeza kuwa Bodi yake itaendelea kutoa mafunzo kwa watumishi wake ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.

Awali akimkaribisha Mkurugenzi Mtendaji kufunga mafunzo hayo, Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu na Utawala wa HESLB Bi. Nuru Sovela alisema watumishi hao wapya wameajiriwa katika mwaka wa fedha 2014/2015 na kuwa mafunzo yaliyotolewa yalihusu huduma kwa wateja; maadili ya utumishi wa umma na utekelezaji wa majukumu ya idara na vitengo mbalimbali vua Bodi hiyo.

HESLB ilianzishwa kwa sheria ya Bunge na 9 ya mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai, 2005 ili, pamoja na majukumu mengine kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji waliodahiliwa katika taasisi za elimu ya juu. Tangu kuanzishwa kwake, Bw. Nyatega amekuwa Mkurugenzi Mtendaji wake.

No comments: